Mahakama yapiga ‘stop’ uwekezaji bandari za Mombasa, Lamu

Dar es Salaam. Mahakama Kuu nchini Kenya imesitisha kwa muda mpango wa Serikali wa kubinafsisha Bandari za Mombasa na Lamu, baada ya kuwasilishwa kwa ombi la wakazi wa eneo hilo wanaodai uamuzi huo ni mbinu za kuchukua udhibiti wa menejimenti na mali ya Mamlaka ya Bandari Kenya (KPA).

Kwa mujibu wa Mtandao wa Daily Nation, amri hiyo imetolewa Novemba 27, 2023 na Jaji Chacha Mwita, ambaye ameipa Serikali siku tatu za kujibu ombi hilo.

Jumuiya ya Taireni ya Mijikenda iliwasilisha ombi Jumatatu Novemba 27, wakiomba mahakama itoe amri ya zuio dhidi ya mpango wa Serikali wa kubinafsisha kwa gati namba moja na gati za maegezo namba 11 – 14 katika Bandari ya Mombasa, lakini pia gati namba moja hadi tatu za bandari ya Lamu.

Mwaka 2019, Jumuiya hiyo pia iliwahi kutafuta zuio la mahakama ili kuzuia ubinafsishwaji wa gati ya makasha namba mbili (CT2) katika Bandari ya Mombasa.

Kwa mujibu wa ‘watetezi’ hao wa rasirimali za Kenya, mpango wa ubinafsishaji wa Bandari ya Mombasa, ni mpango “mchafu” wa baadhi ya watumishi katika Serikali na mashirika yake, kutaka kuchukua udhibiti na usimamizi wa KPA.

Imeelezwa kuwa kuwa hatua ya kwenda mahakamani kwa jumuiya hiyo, kunatokana na juhudi za kutaka mazungumzo na Serikali kugonga mwamba, baada ya KPA kutangaza zabuni hiyo Oktoba 17 mwaka huu.

“Ombi hili linataka kutolewa kwa amri ya zuio ili kusimamisha au kusitisha notisi ya zabuni ya Oktoba 17, 2023, iliyotolewa na Mamlaka ya Bandari ya Kenya kuhamisha/kutoa mali ya umma inayosimamiwa kwa niaba ya umma, kwa wawekezaji binafsi ambao inadaiwa wamealikwa kuziendesha na wakifanikiwa, itakuwa kinyume na katiba na Sheria,” walalamikaji wamesema katika ombi lao.


Uvunjwaji wa Katiba

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa umoja huo, Peter Ponda, mchakato wa ubinafsishaji wa bandari za Mombasa na Lamu ulikuwa na ukiukwaji wa haki za kikatiba.

Amesema gati zilinazolengwa kubinafsishwa ni zile ambazo zilifanyiwa maboresho na kwa kutumia fedha za umma na kwamba zinafanya kazi vizuri.

“Serikali, kupitia kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari ya Kenya, imeanza kujiondoa katika Bandari za Mombasa na Lamu kupitia Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, 2022. Ni wazi kuwa umma umechagia katika uboreshwaji wa gati hizo ambazo wawekezaji waliotajwa, wanakuja kuzichukua,” amesema.

Amesema kuwa kwa kuwa kuna mtaji wa umma, Sheria ya Manunuzi ya Umma na Uondoaji Mali ya mwaka 2015 ilitakiwa kutumika na kwamba serikali pamoja na KPA wameshindwa kuzingatia vifungu vya Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi.

Ponda amesema matumizi ya Sheria hiyo ya ubia ya mwaka 2022 na Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2015, ni lazima yawekwe wazi ili Serikali isiitumie ndivyo sivyo na hivyo kuleta mgongano wa kikatiba.

Mwenyekiti huyo amesema KPA pia imeajiri takriban wafanyakazi 10,000 ambao wanaiwezesha kutimiza wajibu wake kwa umma na kampuni nyingine za biashara kwa nchi za Afrika Mashariki kama vile Uganda, Rwanda, Burundi, Kongo DRC, na Sudan Kusini huku ikitengeza faida ya hadi KSh30 bilioni kwa mwaka.

Ponda amesema: "Inakadiriwa kuwa gati namba 16-18 katika CT2 kwenye bandari ya Mombasa, ujenzi wake umegharimu KSh30 bilioni, ilhali zilizojengwa hivi majuzi huko Lamu, zimegharimu hadi KSh60 bilioni fedha za walipa kodi," alisema.

Kwa upande mwingine, Mahakama Kuu nchini humo ilizuia utekelezwaji wa baadhi ya vifungu vya Sheria ya fedha vinavyoipa Serikali Mamlaka ya kukata kodi ya majengo kutoka kwa Wafanyakazi wa Sekta ya umma wenye mishahara.

Sheria hiyo ya fedha ya mwaka 2023 vifungu vyake vimetenguliwa kutokana na kukiuka katiba ya nchi hiyo kifungu 10, 2(a).

Mahakama pia hiyo ilizuia utekelezwaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa kuwa baadhi ya vifungu vyake vinakiuka Katiba ya nchi hiyo kwa kuweka masharti yanayowaondolea wananchi haki ya msingi ya kupata huduma za Serikali.