Utata mama akidaiwa kumteka mwanaye kisa fedha

Dar es Salaam. Watuhumiwa watatu wametiwa mbaroni na Jeshi la Polisi mkoani Mbeya, wakihusishwa na tuhuma za kumteka mtoto mwenye umri wa miaka mitano, lengo likiwa kushinikiza kujipatia fedha kwa njia udanganyifu.
Watuhumiwa hao waliomteka mtoto huyo kwa siku tisa ni pamoja na Mama mzazi wa mtoto huyo, Agnes Jacob Mwalubuli. Wengine ni Hamida Gaudence Njuu, Wilfred Martin Komba, wote hao wanaendelea kushikiliwa na Polisi kwa ajili ya kukamilisha taratibu ili wafikishwe mahakamani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Mei 24, 2024 na Jeshi Polisi Tanzania kupitia kwa msemaji wake, David Misime , Mei 15, mwaka huu saa 11 jioni walipata taarifa za kupotea mtoto huyo ambaye ni mwanafunzi wa shule ya awali Isaiah Samaritan.
"Baada ya tukio hilo kuripotiwa, baba mzazi wa mtoto aitwaye Layson Mkongwi, alipokea simu kutoka kwa mtu asiyefahamika na kumweleza kuwa hatampata mtoto wake hadi atakapomtumia Sh20 milioni," amesema Misime
Amesema Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, walianza ufuatiliaji wa kina ili kufanikisha upatikanaji wa mtoto huyo akiwa salama, na baadaye wataalam wa upelelezi kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai waliongeza nguvu.
"Mei 24, 2024 majira ya saa 4 walifanikiwa kumkamata Winfred Martin Komba, miaka 36, Mngoni, Mkazi wa Vingunguti Dar es Salaam aliyekuwa akimpigia simu baba mzazi wa mtoto akimtishia asipotoa kiasi hicho hatampata mtoto wake," amesema.
Misime amesema baada ya kukamatwa Wilfred na kuhojiwa alieleza ni kweli walikula njama na mama mzazi wa mtoto huyo aitwaye Agnes Mwalubuli mkazi wa Isyesye Mbeya, ya kujipatia kiasi hicho cha fedha kutoka kwa baba mzazi wa mtoto huyo.
"Ameeleza kuwa walifahamiana na mama huyo walipokuwa wakiishi katika nyumba moja ya kupanga huko Forest ya zamani jijini Mbeya," amesema.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mtuhumiwa huyo katika mahojiano hayo, ameeleza baada ya kupanga njama hizo, alifanikiwa kumchukua mtoto huyo Mei 15, 2024 na kwenda kumficha kwa rafiki yake aitwaye Hamida Gaudence Njuu anayeishi Jijini Mbeya.
"Ufuatiliaji ulifanyika na Mei 24, 2024 saa saba kasoro usiku, mtoto huyo alikutwa nyumbani kwa Hamida Gaudence Njuu huko Simike Mbeya," imesema taarifa.
Polisi wamesema tukio hilo limechukua muda mrefu kutokana na kila ambalo Polisi walikuwa wakipanga kwa kumshirikisha mama mzazi wa mtoto, kumbe yeye alikuwa akimfikishia taarifa mtuhumiwa mwenzake hivyo kumfanya aendelee kukimbia kimbia na kujificha.
"Watuhumiwa hawa watatu ambao ni Wilfred Martin Komba, Agnes Jacob Mwalubuli na Hamida Gaudence Njuu wanaendelea kushikiliwa na Polisi kwa ajili ya kukamilisha taratibu zingine ili wafikishwe mahakamani," imesema taarifa hiyo.