Utafiti: Asilimia 21 Kilimanjaro hawana huduma rasmi za kifedha
Meneja ufuatiliaji na upimaji wa matokeo kutoka Mfuko wa kuendeleza sekta ya fedha(Finscope), Emmanuel Mwamakula akizungumza wakati mwingine a uwasilishwaji wa matokeo ya utafiti wa Finscope wa mwaka 2023 kwa wadau wa sekta ya fedha. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Tafiti za Finscope zinaonyesha asilimia 21 ya wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro wenye umri wa kuanzia miaka 16 hawana huduma rasmi za kifedha na hutegemea taasisi zisizo rasmi kupata huduma hizo.
Moshi. Takwimu za utafiti wa huduma za fedha (Finscope) zinaonyesha asilimia 21 ya wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro wenye umri wa kuanzia miaka 16 hawana kabisa huduma rasmi za kifedha.
Badala yake, wanategemea taasisi zisizo rasmi, hali inayosababisha baadhi yao kuingia katika mikopo inayowaumiza na kuwazidishia umaskini.
Hayo yameelezwa leo Jumatano, Desemba 18, 2024 na Emmanuel Mwamakula, meneja wa ufuatiliaji, upimaji na matokeo wa Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha (FSDT), wakati wa uwasilishaji wa matokeo ya utafiti wa Finscope wa mwaka 2023.
Mkutano huo ulihudhuriwa na mameneja wa takwimu wa mikoa kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na wataalamu wa sekta ya fedha.
"Kwa Mkoa wa Kilimanjaro, asilimia 21 ya wakazi wenye umri wa miaka 16 na kuendelea hawana kabisa huduma za kifedha. Wengi wanapata huduma hizi kutoka kwa taasisi zisizo rasmi kama mikopo ya kausha damu au kukopa kutoka kwa ndugu, jamaa na marafiki," amesema Mwamakula.
Amesema tangu kutolewa kwa takwimu hizo, kumekuwa na juhudi za kufanya tafiti ndogo kuhusu matumizi ya huduma za kifedha katika benki na kampuni za simu.
“Matokeo yake, bidhaa 13 za kifedha zimeboreshwa, na bidhaa nne mpya zimeanzishwa sokoni kutokana na takwimu hizo,” amesema.
Kwa upande wake Salim Kimaro, ofisa mwandamizi mkuu wa Idara ya Usimamizi wa Fedha, Wizara ya Fedha amesema tafiti hizo zimebainisha mikoa yenye ujumuishwaji mdogo wa huduma za kifedha.
Kwa mujibu wa Kimaro, programu maalumu ya elimu ya fedha ilianzishwa kati ya Mei hadi Septemba 2024 na wananchi wapatao 33,000 kutoka mikoa 12 wameshapatiwa mafunzo ya matumizi sahihi ya fedha.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema matokeo ya utafiti huo yatasaidia kuleta maendeleo licha ya changamoto za mikopo isiyo rasmi.
"Wananchi wengi hawana uelewa kuhusu benki na huduma rasmi za kifedha, hivyo wanakimbilia mikopo ya kausha damu. Hali hii imewaathiri hata baadhi ya walimu wengi ambao mara nyingi hukopa bila mpango na nyumba zao huishia kupigwa mnada," amesema RC Babu.
Mkuu huyo wa mkoa amesema tafiti kama hizo ni muhimu kufanyika mara kwa mara ili zisaidie kutoa mwongozo wa kukabiliana na changamoto zilizopo.
"Tunapaswa kushirikiana kuhakikisha tunafanikisha malengo yaliyokusudiwa," amesema Babu.