BoT yaja na mfumo kushughulikia malalamiko ya wateja taasisi za fedha

Ofisa wa Benki Kuu Tanzania kutoka Kurugenzi ya Ustawi na Huduma Jumuishi ya Fedha, Bondo David akitoa elimu kwa maofisa wa huduma za kifedha jijini Mwanza. Picha na Anania Kajuni
Muktasari:
- Mfumo huo wa mpya upo kwenye majaribio, unatarajia kuanza kutumika katikati ya Januari 2025 ukitarajiwa kurahisisha ufuatiliaji wa malalamiko na kutatuliwa kwa uharaka.
Mwanza. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeanzisha mfumo maalumu wa kielektroniki mahususi kwa ajili ya kushughulikia changamoto na malalamiko ya wateja, kuhusu huduma za kibenki.
Mfumo huo ambao haujapatiwa jina rasmi upo kwenye majaribio ukitarajiwa kuanza kutumika katikati ya Januari 2025, pamoja na mambo mengine, utarahisisha ufuatiliaji wa malalamiko na kutatuliwa kwa uharaka.
Akizungumza leo Desemba 18, 2024 jijini Mwanza kwenye semina ya watoa huduma za kifedha kuhusu mfumo huo, Mkurugenzi wa Tawi la BoT Mwanza, Gloria Mwaikambo amesema lengo la kuja na mfumo huo ni kurahisisha utatuzi wa malalamiko ya wateja ambayo baadhi yalikuwa yakichukua muda mrefu.
"Kutokana na changamoto ambazo wateja walikuwa wakipata kutokana na kushughulikiwa changamoto zao, tunafikiria kuanzisha mfumo wa kielektroniki ambao utaenda kuondoa au kutatua matatizo yao," amesema.
Amesema awali mteja alikuwa anatakiwa aandike barua ya malalamiko yake aipeleke ofisi za Benki Kuu ili yashughulikiwe, “lakini pia kulikuwa na changamoto katika ufuatiliaji wa hatua gani utatuzi wa tatizo lake umefikia wapi.”
Hivyo, amesema mfumo huo sasa utasaidia hata utunzaji wa kumbukumbu na kufanya rejea kwenye mfumo.
"Malalamiko yote ya wateja yatakuwa kwenye mfumo, itakuwa rahisi pia kufanya rejea kwenye mfumo kuliko kwenye makaratasi, kwa hiyo tunaamini kwa mfumo huu, huduma za kifedha kwa wateja zinaenda kuboreshwa zaidi, kujenga ujasili na uaminifu kwa watumiaji na watoaji wa huduma za kifedha," amesema Mwaikambo.
Hata hivyo, amesema kwa kuwa bado wapo kwenye majaribio, mfumo huo haujaupata jina rasmi.
Naye Meneja Huduma kwa Wateja Benki ya Africa Tanzania (BOA), Baraka John amesema matarajio yao ni kuona mfumo huo unaenda kutatua changamoto na malalamiko ya wateja kwa wakati.
"Matarajio yetu mfumo huu unaenda kumaliza changamoto za wateja kwa uharaka zaidi lakini pia tunaona unaenda kurahisisha ushirikiano baina ya Benki Kuu na watoa huduma za fedha," amesema Baraka.
Akiunga mkono hoja hiyo, Neema Thomas kutoka Benki ya Diamond Trust (DTB) amewaomba wadau na watoa huduma za fedha kuchangamkia fursa ya kujifunza mfumo huo ambao unaenda kuwa mwarobaini wa malalamiko ya wateja.
"Mfumo huu ni mzuri kwa namna walivyotueleza, ina maana matumizi ya karatasi ambayo yalikuwa yanatumia muda mwingi tunaondokana nao na tuenda kwenye mfumo ambao utaokoa muda na kushughulikia matatizo kwa uharaka," amesema Neema.