Usiku kama mchana JNIA mapokezi ya Yanga

Mashabiki mbalimbali wa soka waliojitokeza Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Mwalimu Nyerere (JNIA) kuipokea klabu ya Yanga.

Dar es Salaam. Usiku kama mchana, neno pekee ninaloweza kulitumia kuelezea namna mambo yanavyoendelea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), hivi sasa ni saa 3. 38 usiku lakini harakati zinazofanyika hapa kama saa 8 mchana.

Vikundi mbalimbali vya hamasa vipo hapa kuwasubiria Yanga, watoto wadogo wapo hapa, wazee na vijana wapo hapa wanaimba kwa furaha na bashasha kuisubiri timu hii ambayo imeshika nafasi ya pili katika Kombe la Shirikisho la Afrika (CAFCC), huu ni usiku kama mchana.

Kila shabiki aliyefika hapa ana bashasha ya kuziona medali za fedha (silver) ambazo mabingwa hawa wa kihistoria (Yanga) wamezitwaa jana Jumamosi Juni 3, 2023 baada ya kuifunga klabu ya USM Alger bao 1-0 na kuhitimisha michezo ya fainali kwa bao 2-2 huku Yanga ikiwa nyuma kwa kuruhusu mabao mengi ya ugenini, bado huu ni usiku kama mchana.

Kama unahisi mamia yaliyojitokeza kuipokea klabu hii yenye makazi yake mtaa wa jangwani wametosha na hawataongezeka basi umekosea kwani barabara ya uwanja wa ndege imejaa foleni ya magari, pikipiki na watembea kwa miguu wanaokuja kuwapokea mabingwa hawa, huu ni usiku kama mchana.

Unaujua wimbo wa kivumbi na jasho? Basi hapa JNIA usiku huu unaimbwa kama tupo Uwanja wa Benjamini Mkapa tunaisubiri mechi ya watani wa jadi, kweli huu ni usiku kama mchana.

Usiku kama mchana hapa JNIA ambapo ni Km 6.3 kufika Gongo lamboto, Km 9.8 kutoka Tabata na Km 40.5 kutoka Bunju lakini pameonekana karibu na mamia ya Watanzania wapo hapa.