Upungufu wa watumishi wachelewesha utatuzi wa migogoro ya ardhi Lindi

Muktasari:
- Idara ya Ardhi Mkoa wa Lindi inakabiliwa na upungufu wa watumishi lakini inaendelea kushughulikia migogoro ya mipaka kati ya vijiji. Serikali imeahidi kulitatua tatizo hilo kwa kuajiri watumishi wapya. Huko Ruangwa, elimu ya matumizi bora ya ardhi imesaidia kudhibiti migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
Lindi. Idara ya Ardhi mkoani Lindi inakabiliwa na upungufu wa watumishi, hali inayochangia kuchelewesha utatuzi wa migogoro ya ardhi kwa wakati, licha ya juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali.
Akizungumza leo, Jumatano Mei 14, 2025, katika kikao kazi kilichofanyika kwenye ukumbi mdogo wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Lindi, Geofrey Mugisha, amesema hadi sasa idara hiyo ina jumla ya watumishi 41 pekee, hali inayokinzana na mahitaji halisi ya zaidi ya watumishi 100 kwa ngazi ya mkoa na halmashauri.
“Ofisi ya ardhi ya mkoa ina watumishi 15 tu wakati inahitaji angalau 30, na halmashauri zote zinahitaji watumishi 73, lakini waliopo ni 26.
“Huu ni upungufu mkubwa unaoturudisha nyuma katika azma ya kumaliza migogoro ya ardhi kwa wakati,” amesema Mugisha.
Amesema kuwa, pamoja na changamoto hiyo, idara yake inaendelea kushughulikia migogoro hasa ya mipaka kati ya vijiji, huku akiiomba Serikali kuharakisha ajira mpya ili kuimarisha utendaji.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Zuwena Omary, amesema Serikali imelipokea kwa uzito suala hilo na italifanyia kazi ili kupunguza changamoto hiyo kwa wakati.
“Tatizo hili nimelipokea rasmi, na nitawasiliana na mamlaka husika kuhakikisha tunapata nyongeza ya watumishi.
“Lakini pia nawaomba watendaji wote kufanya kazi kwa bidii na kujitambua, maana mafanikio ya mkoa wetu yanahitaji mshikamano na ushirikiano,” amesema Omary.
Akizungumzia hali ya migogoro ya ardhi wilayani Ruangwa, Ofisa Ardhi wa wilaya hiyo, Jarome Fakii, amesema changamoto kubwa ilikuwa kati ya wakulima na wafugaji, lakini kwa sasa hali imetulia baada ya elimu ya matumizi bora ya ardhi kutolewa kwa wananchi.
“Tulitenga maeneo kwa ajili ya wakulima na wafugaji, tukatoa elimu, na sasa migogoro ya ardhi kati ya makundi hayo imepungua kwa kiasi kikubwa. Ushirikiano kati ya Serikali na jamii umekuwa chachu ya mafanikio haya,” amesema Fakii.