Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mangi Marealle akimbilia Mahakama Kuu

Muktasari:

  • Hii ni mara ya pili Frank anashindwa shauri hilo, kwani Mei 5,2023 Baraza hilo kupitia kwa Mwenyekiti, Reginald Mtei lilitamka ardhi hiyo ni mali ya Ackley Marealle aliyekuwa akitetewa na wakili Julius Semali wa mjini Moshi.

Moshi. Mfanyabiashara mashuhuri na Mangi wa Wachaga wa Marangu mkoani Kilimanjaro, Frank Marealle ameanzisha mchakato wa rufaa kupinga hukumu ya Baraza la Ardhi na Nyumba Moshi, lililokataa maombi yake aliyoyafungua mwaka 2020.

Marealle aliomba Baraza litoe amri kwamba ardhi yenye mgogoro ni mali yake na ya kufukuliwa kwa kaburi na kuondoa jeneza lenye mwili wa Veronica Mlang’a kwa ajili ya kuzikwa katika ardhi yake iliyopo eneo la Pata.

Pia Marealle aliomba Mahakama itoe amri kwa mjibu maombi, Ackley Marealle anayemtuhumu kuingia kimakosa katika eneo lake, alipe gharama za kesi hiyo ambayo imekuwa ikifuatiliwa na wakazi wa ndani na nje ya mkoa Kilimanjaro.

Hata hivyo, alishindwa shauri hilo kupitia hukumu ya kwanza iliyotolewa Mei 5,2023, akakata rufaa Mahakama Kuu ambayo iliamuru sehemu ya shauri hilo isikilizwe upya, lakini hata iliposikilizwa tena, bado uamuzi ulibaki kama awali.

Kupitia barua ya leo  Mei 12, 2025, wakili wake, Modestus Njau wa kampuni ya uwakili ya Demo Lawa Associates ya mjini Moshi, amewasilisha katika Baraza hilo, kusudio la Mangi Marealle la kukata rufaa kupinga hukumu hiyo ya Mei 9, 2025.

“Muombaji (Frank Marealle) baada ya kuhuzunishwa na kutoridhika na hukumu na amri zilizotolewa na Mwenyekiti wa Baraza,  Hussein Lukeha, anakusudia kukata rufaa Mahakama Kuu kanda ya Moshi,”inasema barua hiyo ya wakili Njau.

“Hakubaliani na uamuzi wote pamoja na amri zake. Kwa lengo hilo (la kukata rufaa), muombaji Frank Marealle anaomba apatiwa nakala ya mwenendo wa shauri, hukumu na amri za Baraza lako ndani ya muda muafaka,”ameeleza.

Wakili huyo alipotafutwa na Mwananchi leo amejibu kwa kifupi kuwa; “Ni kweli nina maelekezo kamili ya kwenda High Court (Mahakama Kuu) na tuna sababu za msingi za kupinga ile hukumu. Tutakutana nao mahakamani.”

Katika uamuzi huo, mwenyekiti wa baraza hilo aliamuru kuwa eneo hilo ni mali ya Ackley Marealle na mwili wa Veronica usifukuliwe na kuzikwa eneo lingine na kila upande utawajibika kubeba gharama za kesi.

Hii ni mara ya pili Frank anashindwa shauri hilo, kwani Mei 5,2023 baraza hilo kupitia kwa mwenyekiti, Reginald Mtei lilitamka ardhi hiyo ni mali ya Ackley Marealle aliyekuwa akitetewa na wakili Julius Semali wa mjini Moshi.

Ackley ni mtoto wa mwisho wa marehemu Veronica Mlang’a na muda wote wa shauri hilo yeye binafsi na kupitia kwa wake,  alikuwa akipinga madai ya Frank Marealle na kusisitiza kuwa ardhi hiyo ni mali yake.

Mwili wa Veronica ambaye alikuwa ni mke wa sita wa Mangi David Mlang’a ulizikwa Jumamosi ya Machi 21, 2020 katika kitongoji cha Moori, kijiji cha Lyamrakana, katika maziko yaliyosimamiwa na Jeshi la Polisi Himo na Moshi.


Kiini cha mgogoro

Kulingana na nyaraka za mahakama, Frank Marealle alikuwa anadai kuwa marehemu Mangi David Marealle, ambaye ni baba yake, alikuwa mmiliki halali wa eneo hilo lililopo kijiji cha Lyamrakana kilichopo Marangu wilaya ya Moshi.

Frank alidai mama yake aitwaye Asnath David Marealle alikuwa mke wa nane  wa marehemu mangi David, alimiliki eneo hilo na kuliendeleza kuanzia mwaka 1931.

Alidai mwaka 1961, Mangi David Marealle aliwagawia watoto wake Wilfred Marealle na Frank Marealle eneo la Magharibi na Mashariki na baada ya muda kupita, mama mzazi wa Ackley, alipewa eneo la Kusini la shamba hilo la Mangi.

Alidai kuwa Machi 18, 2020 baada ya kifo cha Veronica ambaye ni mama mzazi wa Ackley, mchakato wa mazishi ulianza ambapo mtoto wa marehemu alipanga kumzika mama yake katika eneo la Frank Marealle na alifanikiwa kumzika.

Hata hivyo, katika majibu yake, Ackley alikanusha madai ya mdai na kusisitiza kuwa ardhi hiyo inamilikiwa na mama yake ambapo aliishi hapo tangu alipoolewa na baba yake hadi alipofariki dunia mwaka 2020.

Baada ya Baraza kusikiliza ushahidi wa pande hizo mbili, uliamua kuwa Ackley ndio mmiliki halali wa ardhi hiyo kama mtoto wa mwisho wa marehemu na baraza likatoa zuio la kudumu kwa Frank au mawakala kuingia katika eneo hilo.