Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mangi Marealle akwaa tena kisiki

Muktasari:

  • Hii ni mara ya pili Frank anashindwa shauri hilo, kwani Mei 5,2023 baraza hilo kupitia kwa mwenyekiti, Reginald Mtei lilitamka ardhi hiyo ni mali ya Ackley Marealle aliyekuwa akitetewa na wakili Julius Semali wa mjini Moshi.

Moshi. Mfanyabiashara mashuhuri na Mangi wa wachaga wa Marangu, Mkoa wa Kilimanjaro, Frank Marealle, anayetaka mwili wa mama yake mdogo ufukuliwe na kuzikwa eneo lingine kwa madai eneo hilo ni mali yake, amekwaa kisiki kortini.

Hii ni mara ya pili Frank anashindwa shauri hilo, kwani Mei 5,2023 Baraza hilo kupitia kwa mwenyekiti, Reginald Mtei lilitamka ardhi hiyo ni mali ya Ackley Marealle aliyekuwa akitetewa na wakili Julius Semali wa mjini Moshi.

Ackley ni mtoto wa mwisho wa marehemu Veronica Mlang’a na muda wote wa shauri hilo yeye binafsi na kupitia kwa wake alikuwa akipinga madai ya Frank Marealle, na kusisitiza kuwa ardhi hiyo ni mali yake.

Mwili wa Veronica ambaye alikuwa ni mke wa sita wa Mangi David Mlang’a ulizikwa Jumamosi ya Machi 21, 2020 katika kitongoji cha Moori, kijiji cha Lyamrakana, katika maziko yaliyosimamiwa na Jeshi la Polisi Himo na Moshi.

Frank katika hati ya shauri hilo alikuwa anadai kuwa yeye ndio anamiliki kihalali ardhi hiyo tangu mwaka 1931 kupitia kwa mama yake aitwaye Asinath Marealle aliyekuwa miongoni mwa wake wa Mangi David Marealle.

Marealle aliwasilisha shauri katiba baraza hilo, akiliomba litoe amri kuwa ardhi yenye ukubwa wa hekari mbili iliyopo kijiji cha Lyamrakana Marangu wilaya ya Moshi ni mali yake na mwili wa Veronica uliozikwa hapo ufukuliwe na kuondolewa.

Frank kupitiwa kwa wakili wake, Modestus Njau hakuridhika na kukata rufaa Mahakama Kuu Moshi ambapo Jaji Mfawidhi Lilian Mongela, alibatilisha sehemu ya mwenendo wa shauri na kuagiza lisikilizwe na mwenyekiti mwingine.

Jaji Mongella alisema baada ya kupitia hoja za pande mbili katika mgogoro huo, Mahakama ilibaini dosari za uendeshaji wa shauri hilo ikiwamo mwenyekiti kuingiza taarifa mpya kwenye hukumu, ambazo haziko kwenye mwenendo.

Kutokana na dosari hizo, Jaji Mongella alisema Mahakama imebatilisha mwenendo wa shauri hilo katika baraza kuanzia Machi 6, 2023, sehemu ya mwenendo ambao mwenyekiti wa baraza alitoa amri ya kutembelea eneo lenye mgogoro.

“Nabatilisha hukumu yote na naamuru shauri hili lirudishwe kwenye Baraza la Ardhi na Nyumba Moshi kumalizia usikilizwaji wa shauri mbele ya mwenyekiti mwingine kwa vile dosari hazijasababishwa na upande mmojawapo,” alisema Jaji.

Hata hivyo baada ya kusikiliza upya shauri hilo kama Mahakama Kuu ilivyoagiza, hukumu iliyotolewa Ijumaa ya Mei 8,2025 na Mwenyekiti wa Baraza, Hussein Lukeha, maamuzi yamebaki kuwa kama yalivyokuwa awali kabla ya rufaa.

Kulingana na uamuzi huo, baraza baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili na kutembelea eneo hilo lenye mgogoro, limetamka kuwa mmiliki halali wa eneo hilo ni Ackley Mlang’a Marealle na Veronica alizikwa kihalali katika eneo hilo.

Katika uamuzi huo, mwenyekiti huyo ameamuru mwili wa Veronica usifukuliwe na kuzikwa eneo lingine na kwamba kila upande utawajibika kubeba gharama za kesi hiyo kutokana na mazingira ya kesi yenyewe.


Kauli za mawakili

Akizungumza na gazeti jana, wakili Semali aliyekuwa akimtetea Ackley alisema yeye pamoja na mteja wake wameridhishwa na hukumu hiyo, lakini wakili wa Mangi Marealle alisema hawajaridhishwa nayo na wanakata tena rufaa.

“Sisi tumeridhika. Mahakama imetenda haki na tunaamini wenzetu nao wataridhika kwa sababu haki si kushinda tu hata kushindwa ni haki japokuwa inakuwa ni ngumu kukubali. Ukweli unabaki kuwa Baraza limetenda haki,”alisema.

Hata hivyo, wakili Njau alisema mteja wake hakuridhika na hukumu hiyo na wanakata rufaa Mahakama Kuu, akisema mwenyekiti ametoa hukumu bila mdaiwa (Ackley) kutoa uthibitisho wa kutosha kuwa alipewa hilo eneo na nani.

“Upande wa Frank Marealle anakata rufaa kwa sababu hakuridhika na maamuzi. Sababu za rufaa ni kwamba Mahakama Kuu ilivyoamua kurudisha hii kesi tena Baraza la Ardhi ilifuta huo mwenendo wa awali,”alisema wakili Njau.

“Lakini sisi ilivyorudi tukaenda tu kuangalia eneo lenye mgogoro halafu huyu mwenyekiti mwingine ambaye siye aliyesikiliza kesi mwanzoni akaandika hukumu bila kuzingatia kwamba Ackley hakuwa na uthibitisho alipewa hilo eneo na nani,” alisema.