Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Umri wamnusuru kifungo cha miaka 30 jela

Muktasari:

  • Umri wa mwathirika katika kesi za ubakaji ni kigezo muhimu katika kuthibitisha kosa la ubakaji na zaidi sana katika utoaji wa adhabu,  kwa kuwa adhabu kwa mshtakiwa aliyetiwa hatiani kwa kosa hilo hutofautiana kulingana na umri wa mwathirika.

Dar es Salaam. Mahakama ya Rufani imetengua hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza iliyothibitisha hukumu ya Mahakama ya Wilaya Bukombe (Geita) kwa kumpa Cosmas Herman kifungo cha miaka 30 jela, kutokana na umri wa mwathirika kutothibitishwa.

Herman ambaye ni mkazi wa kijiji cha Msasa wilayani Bukombe, mkoani Geita alipewa adhabu hiyo katika hukumu yake ya Aprili 15, 2020, baada ya kumtia hatiani kwa kosa la ubakaji katika kesi ya jinai namba 72 ya mwaka 2019.

Katika kesi Herman alishtakiwa kwa kosa la kumbaka binti mwenye umri wa miaka 13, kinyume cha vifungu 130(1) (2) (e) na 131(1) vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code – PC), akidaiwa kutenda kosa hilo Aprili 19, 2019, 2017, nyumbani kwake kijijini hapo.

Awali Herman alikata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza kupinga hukumu hiyo ya Mahakama ya Wilaya, yaani hatia na adhabu lakini Mahakama Kuu ilitupilia mbali rufaa yake hiyo na badala yake ilithibitsha hukumu ya Mahakama ya Wilaya kuwa ilikuwa sahihi.

Alikata rufaa ya pili Mahakama ya Rufani ambayo katika hukumu yake iliyotolewa na jopo la majaji watatu lilioongozwa na Jaji Stella Mugasha, na wenzake Issa Maige na Amour Khamis, imetengua hukumu ya Mahakama Kuu.

Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo baada ya kubaini kuwa katika kumbukumbu za rufaa hiyo zilizoko mahakamani hakuna ushahidi wa upande wa mashtaka kuthibitisha umri wa mwathirika.

Kabla ya uamuzi huo wa mahakama, wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo Serikali nayo iliunga mkono rufaa hiyo kutokana na kasoro hiyo na ikaiomba mahakama hiyo imwondolee hatia na adhabu Cosmas.

“Mwishowe na kutokana na sababu zilizoelezwa, tunakubali rufaa, kwa hiyo tunatengua hatia na kufuta adhabu iliyotolewa dhidi ya mrufani (Cosmas)”, imesema mahakama katika hukumu yake baadaya kurejea kumbukumbu na hoja za rufaa hiyo, na kuhitimisha:

“Tunaamuru aachiliwe huru kutoka gerezani mara moja isipokuwa kama ataendelea kushikiliwa kwa sababu nyingine halali.”

Jinsi ilivyokuwa

Wakati wa usikilizwaji kesi ya msingi, ilidaiwa na upande wa mashtaka kuwa siku ya tukio na muda uliotajwa, mshtakiwa (Cosmas) alimchukua mwathirika akaenda naye chumbani kwake ambako alimuingilia kingono isivyo halali.

Binti huyo aliporejea nyumbani, aliulizwa na baba yake, Jafari John (shahidi wa pili katika kesi hiyo), mahali alikokuwa naye akamjibu kuwa alikuwa na Cosmas.

Baada ya kuhojiwa zaidi alibainisha kuwa alikuwa amebakwa na Cosmas kufuatia maelezo hayo, Cosmas alitiwa mbaroni na kupelekwa katika ofisi ya ofisa mtendaji wa kijiji, ambako alihojwa na mtendaji wa kijiji, Salome Ncharangi (shahidi wa tatu), na Cosmas alikiri kutenda kosa hilo.

Kisha mwathirika alifanyiwa uchunguzi na daktari Mariam Hemed (shahidi wa tano) na kupitia taarifa yake ya uchunguzi (ambacho ni kilikuwa kielelezo cha kwanza cha upande wa mashtaka) alibainisha kuwa mwathirika alikuwa amebakwa.

Mahakamani

Cosmas alipandishwa kizimbani katika kesi ya msingi na kusomewa shtaka la ubakaji lakini alikana kuhusika na katika utetezi wake alidai kuwa kesi hiyo ilikuwa ni ya kutungwa kutokana na mgogoro baina yake na baba wa mwathirika.

Hata hivyo, mahakama hiyo baada ya kukamilisha usikilizwaji huo, ililiridhika na ushahidi wa upande wa mashtaka na ikamtia hatiani na kumhukumu adhabu hiyo ya kifungo cha miaka 30 jela.

Cosmas alikata rufaa Mahakama Kuu Mwanza kupinga hukumu hiyo, bila mafanikio kwa kuwa mahakama hiyo ilitupiliwa mbali ndipo akakata rufaa ya pili Mahakama ya Rufani.

Katika rufaa hiyo aliwasilisha sababu nane za rufaa, ambazo zote zilijielekeza kwenye hoja moja kuwa mashtaka dhidi yake hayakuwa yamethibitishwa bila kuacha shaka.

Siku ya usikilizwaji wa rufaa hiyo, Cosmas hakuwa na uwakilishi (wakili) na Serikali iliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu Revina Tibalengwa, akisaidiwa na mawakili wa Serikali Daniel Masambu na George Ngemela.

Cosmas aliiomba mahakama hiyo izingatie sababu zake za rufaa kama zilivyo katika hati ya sababu za rufaa kisha imwachilie.

Hata hivyo,  Wakili Masambu aliieleza mahakama kuwa mjibu rufaa (Serikali) anaunga mkono rufaa, akieleza kuwa kwa kifungu cha 130(2) (e) cha PC alichoshtakiwa nacho mrufani, umri wa mwathirika wa ubakaji ni kiini muhimu.

Hata hivyo, alifafanua kuwa hakuna shahidi yeyote wa upande wa mashtaka aliyebainisha umri wa mwathirika. Hivyo naye aliiomba mahakama kukubali rufaa hiyo na kumuachilia huru mrufani.

Uamuzi wa Mahakama

Mahakama katika hukumu yake imesema kuwa baada ya kuzingatia hoja wakili wa Serikali na kupitia kumbukumbu za rufaa (nyaraka zilizoambatanishwa kwenye rufaa hiyo), inakubaliana na wakili wa Serikali kuwa shtaka dhidi ya mrufani halikuthibitishwa bila kuacha shaka ya msingi.

Mahakama hiyo imesema kuwa kosa chini ya kifungu hicho hutendeka pale ambapo mwanaume hufanya ngono msichana kwa ridhaa au bila ridhaa, pale ambapo msichana huyo yuko chini ya umri wa miaka 18, isipokuwa kama ni mke wake ambaye ana umri wa miaka 15 au zaidi na hawajatengana.

“Kwa hiyo ni wazi kwamba ili kuwe na kosa la ubakaji chini ya kifungu cha 130 (2) (e) Sheria ya Kanuni ya Adhabu (alichoshtakiwa nacho Cosmas), mwathirika lazima awe msichana ambaye umri wake ni chini ya miaka 18”, imesema mahakama na kusisitiza:

“Hivyo, umri wa mwathirika ni kiini muhimu cha kosa ambacho bila kuwepo kosa kosa hilo haliwezi kuthibitika”.

Ikirejea uamuzi wa kesi mbambali ilizokwisha kuziamua, Mahakama ya Rufani imesema kuwa katika kesi ambapo umri wa mwathirika ni kigezo katika kuthibitisha kosa, ushahidi lazima utolewe kubainisha umri wa mwathirika.

“Tumechunguza kumbukumbu za rufaa na hatukupata shaka kwamba ushahidi wa upande wa mashtaka uko kimya kabisa kuhusu umri wa mwathirika”, imesema mahakama na kuhitimisha:

“Umri wake ulitajwa tu katika kielelezo cha upande wa mashtaka PI. Hata hivyo kielelezo hicho kiliondolewa na Mahakama Kuu kwenye kumbukumbu katika rufaa ya kwanza kwa kuwa hakuwahi kusomwa baada ya kupokewa. Katika mazingira haya shtaka dhidi ya halikuthibitishwa bila kuacha shaka yoyote.”