Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jela miaka saba kwa kumtapeli Ridhiwani Kikwete

Mshtakiwa Innocent Chengula (mwenye shati jeupe katikati) akiwa na washtakiwa wengine katika gari, baada ya kuhukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kifungo cha miaka saba. Picha Hadija Jumanne

Muktasari:

  • Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemuamuru Chengula kumlipa Ridhiwani kiasi cha Sh4 milioni, anachodaiwa kumtapeli.

Dar es Salaam. Innocent Chengula, amehukumiwa kifungo cha miaka saba jela, kwa kujipatia Sh4 milioni kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete.

Chengula (23) alijipatia fedha hizo baada ya kujitambulisha kwa Ridhiwani kuwa yeye ni Dk Hassan Abbas, ambaye kwa sasa ni Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii akiomba kupatiwa Sh5 milioni.

Hukumu hiyo imetolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu  leo Jumatano Juni 5 2024  na pia imemuamuru Chengula kumlipa Ridhiwani Sh4 milioni anazodaiwa kumtapeli.

Mbali na adhabu hiyo, Mahakama imetaifisha simu moja ya mkononi na laini tatu za simu alizotumia mshtakiwa kutenda kosa hilo.

Chengula, mkazi wa Kigogo Luhanga, alikuwa akikabiliwa na mashtaka sita, yakiwamo ya kujipatia fedha kwa udanganyifu na kutuma ujumbe wa maandishi kwenda mtandao wa kijamii wa WhatsApp akijitambulisha kwa Ridhiwani Kikwete na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia kuwa yeye ni Dk Abbas, akijua kuwa ni uongo.

Hukumu imetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Yusto Ruboroga katika kesi ya jinai namba 139/2022.

Hakimu Ruboroga amesema upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi 14 ambao wamethibitisha mashtaka pasipo kuacha shaka.

Baada ya kumtia hatiani kwa makosa yote sita aliyoshtakiwa nayo hakimu alimuhukumu kulipa faini ya Sh12 milioni au kwenda jela miaka saba kwa kujitambulisha uongo kwa Ridhiwani. Adhabu kama hiyo imetolewa pia katika shtaka la kujitambulisha kwa uongo kwa Karia.

"Shtaka la tatu la kujipatia Sh4 milioni kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa Ridhiwani, Mahakama inakuhukumu Chengula kifungo cha miaka saba jela, bila faini," amesema Hakimu Ruboroga.

Katika shtaka la nne, tano na sita ya kutumia laini ya simu inayotumiwa na mtu mwingine, mahakama  imehukumu kulipa faini ya Sh5 milioni kwa kila kosa au kutumikia kifungo cha miezi sita kwa kila moja.

Hata hivyo, Hakimu Ruboroga amesema adhabu zitatumikiwa kwa pamoja, hivyo atatumimia kifungo cha miaka saba jela.

Kabla ya adhabu kutolewa, Wakili wa Serikali, Glory Kilawa aliiomba mahakama kutoa iliyo kali kwa mshitakiwa ili iwe fundisho kwake na wengine wenye tabia za kuwaibia watu mtandaoni.

Mshtakiwa ameiomba mahakama impunguzie adhabu kwani amekaa gerezani mwaka mmoja na miezi minane.

Hakimu Ruboroga ametupilia mbali ombi la mshtakiwa alikisema Mahakama inampa adhabu kali iwe fundisho kwa wengine wanaoiba fedha za watu mtandaoni wakiwasumbua raia.


Ushahidi uliotolewa

Mshtakiwa anadaiwa kuwatumia ujumbe watu mbalimbali na baadhi ya hao ni Dk Hassan Abbas, Ridhiwani Kikwete, Wallace Karia na hayati Gardner Habash.

Hakimu Ruboroga akipitia ushahidi wa Ridhiwani, amesema Julai 26, 2022, Chengula kupitia mtandao wa WhatsApp alimtumia ujumbe kwamba yeye ni Dk Abbas anaomba apatiwe Sh5 milioni kwa maelezo kuwa ana shida.

Kwa wakati huo Dk Abbas alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Habari na Michezo.

Ridhiwani alidai baada ya kupata ujumbe huo hakuwa na wasiwasi kwa sababu Dk Abbas naye ni majirani na wanasaidiana kwa kiasi kikubwa.

Ujumbe ulipotumwa anadai Dk Abbas alikuwa nchini Marekani na Rais Samia Suluhu Hassan kwenye ziara ya The Royal Tour.

"Sikuwa na wasiwasi kwamba siyo Dk Abbas kwa sababu tuko majirani Dodoma na tunasaidiana kiasi kikubwa, hivyo uhusiano wetu ni wa karibu sana," amesema hakimu akisoma ushahidi wa Ridhiwani.

Amesema alimtaka kutuma fedha kwa namba nyingine.

"Nilienda Benki ya Exim iliyoko Dodoma, nilitoa Sh4 milioni iliyokuwapo katika akiba yangu nikampa mfanyakazi wa benki  aitwaye Gemma na namba ya simu, baada ya kutuma alinijulisha," amesema akikariri ushahidi wa Ridhiwani.

Anadai baada ya siku chache kupita, alipigiwa simu na Dk Abbas akamuuliza kama kuna mtu alimpigia simu na kujitambulisha kwa jina lake, akamjibu ndiyo.

"Nilivyomjibu aliniambia umetapeliwa, alinijulisha tapeli wamemkamata na kisha akaniunganisha na Inspekta Tunu wa Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam kwa ajili ya hatua nyingine," amesema katika ushahidi.

Amedai katika ushahidi alipowasiliana na Tunu, alimwezesha kuzungumza na mtuhumiwa aliyekiri kuchukua fedha na akaomba radhi.

"Nilimjibu sihitaji kuombwa radhi, nahitaji pesa yangu naye akadai hana bali anaomba radhi tu," amedai Ridhiwani katika ushahidi.

Pia alidaiwa kati ya Juni na Agosti, 2022 alitumia laini zilizosajiliwa kwa jina la Nuru Maulid, Deogratias Kimario na Asha Mkai bila kutoa taarifa kwa mtoa huduma.