Matapeli wa simu wamjaribu waziri

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Isaac Kamwelwe.
Muktasari:
Safari hii matapeli hao wamemtumia ujumbe wa kitapeli, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Isaac Kamwelwe.
Dar es Salaam. Kama ulidhani ni wananchi wa kawaida peke yao wanakutana na matapeli kwa njia ya simu, basi umekosea.
Safari hii matapeli hao wamemtumia ujumbe wa kitapeli, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Isaac Kamwelwe.
Akizindua programu ya uvumbuvi wa vipaji na maendeleo ya kampuni ya huduma za mawasiliano nchini Huawei juzi, Kamwelwe alisema hata yeye ni mwathirika wa utapeli huo.
“Licha ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kutoa onyo kwa matapeli hao na watu zaidi ya kumi kukamatwa kwa kujaribu kutapeli fedha kwa kutumia simu za mkononi, hata mimi juzi nimepokea ujumbe ukinitaka nitume fedha kwa namba hiyo,” alisema Kamwelwe.
Akinukuu ujumbe aliotumiwa Kamwelwe alisema: “Tafadhali tuma fedha kwenye namba hii kwa sababu simu yangu imeharibika.”
Aliwataka wataalamu wa masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano nchini kutoa elimu kuisaidia kufikia malengo ya kuwa na Tanzania ya viwanda ifikapo 2025 badala ya wananchi kutapeli fedha.
“Tehama ni muhimu hasa linapokuja suala la uchumi wa viwanda, lakini inapotumika kinyume chake inarudisha nyuma juhudi zetu,” alisema Kamwelwe.
Naye Balozi wa China nchini, Wan Ke alihimiza kampuni za China ambazo zimewekeza kwa kiasi kikubwa nchini kufuata sheria ikiwamo kulipa kodi.
“Huawei ni kampuni binafsi lakini tunaipa ushirikiano kwa sababu inafanya kazi kwa kufuata sheria,” alisema Wan Ke.
Wiki iliyopita watu 13 walipandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa makosa ya kutumia simu kufanya utapeli.