Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wawili wafariki ajali ya gari lililokuwa likisafirisha maiti

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linamshikilia dereva wa gari hilo, Mohamed Kisukari (43), mkazi wa Kimara Dar es Salaam, kwa kosa la kuendesha gari kwa uzembe na kusababisha ajali hiyo iliyogharimu maisha ya watu.

Morogoro. Watu wawili wamefariki dunia na wengine saba kujeruhiwa katika ajali ya gari lililokuwa likisafirisha maiti, iliyotokea katika Kijiji cha Badilo kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linamshikilia dereva wa gari hilo, Mohamed Kisukari (43), mkazi wa Kimara, Dar es Salaam, kwa kosa la kuendesha gari kwa uzembe na kusababisha ajali hiyo iliyogharimu maisha ya watu.

Ajali hiyo ilitokea jana Julai 9, 2025 saa nne usiku katika Kijiji cha Badilo ambapo gari aina ya Toyota Rosa lililokuwa likisafirisha maiti, liliacha njia na kutumbukia kwenye korongo, umbali wa mita 180.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama, watu hao wawili waliofariki dunia katika ajali hiyo ni waombolezaji waliokuwa wakisindikiza maiti.

Kamanda Mkama amesema uchunguzi wa awali katika eneo la ajali umebaini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari hilo kuendesha kwa mwendo kasi bila kuzingatia jiografia ya eneo hilo ambayo ni milima, miteremko na kona kali.

Katika ajali hiyo, waombolezaji wengine walipata majeraha na wanaendelea na matibabu ambapo majeruhi saba wamepelekwa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro kwa matibabu zaidi.

Dk Ablah Issa, mratibu wa huduma za tiba katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, amethibitisha kupokea majeruhi hao saba ambapo kati yao, wanne wa kike na watatu wa kiume wanaendelea na matibabu huku mmoja kati yao akiruhusiwa.

 “Leo tumepokea majeruhi saba, wanne wa kike na watatu wa kiume, kwa hali zao mpaka sasa hivi wanaendelea vizuri na matibabu na mmoja wao ameruhusiwa. Kwa hiyo wanabaki majeruhi sita, hali zao zinaendelea vizuri, hakuna mgonjwa anayehitaji uangalizi maalumu wa daktari wala kupewa rufaa,” amesema Dk Ablah Issa.

Kisukari, dereva aliyekuwa akiendesha gari lililopata ajali amesema walikuwa wanatokea Dar es Salaam kuelekea Kinore, Morogoro kuzika, akiwa njiani eneo la Kijiji cha Badilo, Kata ya Tegetero, kwenye kona kali, tairi ya mbele ya gari lilikanyaga jiwe na kupinduka kuelekea kwenye korongo umbali wa mita 180.

Mmoja wa majeruhi, Amina Makusi amesema msafara wao ulikuwa na gari tatu iliyobeba maiti ndiyo ilipata ajali.

“Juzi, mtoto wa mjomba wangu aligongwa na lori akiwa na bodaboda akafariki dunia, kwenye harakati za kusafirisha mwili, tumekuja vizuri, karibu na kufika nyumbani ndiyo tumepata ajali,” amesema Amina akiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro akipatiwa matibabu.