Wawili wafariki kwa ajali Tabora

Hili ndilo basi lililogonga bajaji ya mizigo na mabaki ya vyuma hivyo ni ya bajaji ambayo imegongwa katika eneo la Malolo manispaa ya Tabora. Picha na Hawa Kimwaga
Muktasari:
- Ajali hiyo ilihusisha basi la abiria pamoja na bajaji ya kubebea mizigo, imegharimu uhai wa watu wawili na majeruhi mmoja ilitokea eneo la Miemba, Malolo Manispaa ya Tabora.
Tabora. Watu wawili wamefariki dunia akiwemo dereva wa bajaji ya mizigo na msaidizi wake kufuatia kugongwa na basi la abiria kampuni ya Yehova Yire, lililokua likitokea Dar es Salaam kwenda mkoani Kigoma baada ya kuacha njia na kuigonga bajaji hiyo.
Akizungumzia ajali hiyo Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Costantine Mbogambi amesema imetokea katika Barabara ya Mirambo eneo la Malolo Manispaa ya Tabora saa tano na nusu asubuhi na kusababisha vifo hivyo, baada ya ajali dereva wa basi hilo amekimbia kusikojulikana.
Aidha amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa basi hilo anayefahamika kwa jina la Abdala Ramadhani (43) ambaye aliondoka na basi hilo kituo kikuu cha mabasi Tabora akielekea mkoani Kigoma, ambapo muda mchache baadaye basi hilo liliacha njia na kugonga bajaji ya mizigo iliyokua imebeba magunia ya mpunga.
Amesema waliofariki dunia katika ajali hiyo ni pamoja na dereva wa bajaji aitwaye Kafumu Shabani (30) na Athumani Ramadhani (28) huku Thomas Joseph (50) akisalia mahututi kufuatia majeraha makubwa yaliyosababishwa na ajali hiyo.
“Ajali hii imetokea Malolo Tabora na chanzo ni uzembe wa dereva wa basi kuacha njia yake na kugonga bajaji hiyo kama ambavyo nimeeleza, amegharimu maisha ya watu wawili na mwingine hali yake ni mbaya yuko Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kitete,” amesema Kamanda.
Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora Kitete kwa ajili ya taratibu zingine za mazishi.
Mmoja wa abiria katika basi hilo, Masumbuko Musa amesema wakiwa ndani ya basi waliona likiyumba sana na kupoteza mwelekeo ndio baadaye ikatokea ajali hiyo.

Haya ni mabaki ya vyuma vya bajaji ya mizigo baada ya kugongwa na basi kampuni ya Yehova Yire katika eneo la Malolo manispaa ya Tabora. Picha na Hawa Kimwaga
“Yaani tumeshangaa tu basi linayumba sana halafu watu wakaanza kuruka kwenye madirisha badala ya kupitia kwenye mlango wa basi, kumbe ajali imeshatokea kubwa na watu wameumia damu tu zimesambaa chini,” amesema.
George Masele ni mwenyekiti wa Miemba amesema ajali hiyo imesababisha uharibifu mkubwa katika bajaji kwa maana imeharibika zaidi kutokana na kuburuzwa na basi hilo.