Kasoro katika utambuzi zamtoa jela aliyehukumiwa miaka 30
Muktasari:
- Seleman Nyigo alishtakiwa kwa unyang’anyi wa kutumia nguvu na ubakaji.
Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Iringa imemuachia huru mshtakiwa aliyehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kumbaka msichana raia wa Ujerumani.
Seleman Nyigo, mwosha magari eneo la Ndiuka, Kata ya Gangilonga, Manispaa ya Iringa ameachiwa huru na mahakama.
Mahakama katika hukumu iliyotolewa na Jaji Ilvin Mugeta imemuachia huru Seleman Nyigo maarufu Mwanyigo, muosha magari eneo la Ndiuka, Kata ya Gangilonga, Manispaa ya Iringa, kutokana na mpelelezi wa kesi hiyo kushindwa kueleza namna walivyombaini mtuhumiwa (mrufani) waliyemtia mbaroni na hatimaye kumfikisha mahakamani kuwa ndiye aliyetemtendea uhalifu huo msichana huyo.
Alihukumiwa adhabu hiyo na Mahakama ya Wilaya ya Iringa katika kesi ya jinai namba 18/2020.
Katika kesi hiyo alishtakiwa kwa makosa mawili, unyang'anyi wa kutumia nguvu na kubaka.
Alidaiwa siku ya tukio, Februari 12, 2021, alimbaka binti huyo wa miaka 19, aliyekuwa akifanya kazi ya ualimu wa kujitolea.
Pia alidaiwa kumpora simu ya mkononi aina ya Samsung Galax C7, kadi ya ATM na fedha taslimu Sh100,000.
Ilivyokuwa
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka na ushahidi wa upande wa mashtaka, mchana wa siku ya tukio msichana huyo alikuwa akitembea kutoka kazini Ipogolo kurudi nyumbani kwake eneo la Gangilonga kupitia njia ya mkato ya waenda kwa miguu.
Njiani alikutana na Mwanyigo anayedaiwa alimfunga kamba mikononi, akambaka na kumpora mali zake. Tukio inadaiwa lilidumu kwa dakika 30.
Msichana huyo, aliyekuwa shahidi wa kwanza, alidai alitoa taarifa polisi kisha akaenda hospitalini alikofanyiwa uchunguzi na Dk Shaban Likondongom.
Daktari huyo ambaye ni shahidi wa tatu, na ripoti yake ya uchunguzi, iliyopokewa na kuwa kielelezo cha pili cha upande wa mashtaka, aliona mbegu za kiume sehemu za siri, huku bikira ya msichana huyo ikiwa imetobolewa na kuvuja damu.
Polisi katika upelelezi kupitia shahidi wa nne, mpelelezi Koplo Lubeya alikuta nguo eneo la tukio zikiwa korongoni, ambazo waosha magari wa eneo la Ndiuka walizitambua kuwa za mshtakiwa.
Mwanyigo alitiwa mbaroni na likaandaliwa gwaride la utambuzi lililoendeshwa na shahidi wa pili Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, William Kilangi na msichana huyo alimtambua Mwanyigo kuwa ndiye mtuhumiwa aliyemfanyia uhalifu.
Mahakama ya Wilaya Iringa iliridhika kuwa binti huyo aliporwa mali na kubakwa na mshtakiwa.
Alitiwa hatiani kwa makosa yote mawili na kuadhibiwa kifungo cha miaka 15 jela kwa kosa la unyang'anyi wa kutumia nguvu na miaka 30 kwa kosa la pili la ubakaji.
Mwanyigo hakuridhika na hukumu, alikata rufaa Mahakama Kuu kupinga hatia na adhabu aliyopewa, akiwasilisha sababu 13.
Pamoja na mambo mengine alidai mashtaka hayakuthibishwa bila kuacha mashaka.
Ilichokisema Mahakama
Mahakama Kuu katika hukumu iliyotolewa Mei 30, 2024 na Jaji Mugeta, ilichambua tena ushahidi uliowasilishwa na imekubali hoja hiyo.
Jaji Mugeta amesema anakubaliana na hakimu aliyesikiliza kesi ya msingi kuwa ushahidi wa mwathirika na wa daktari aliyemtibu siku ya tukio kwamba msichana huyo aliingiliwa kingono na aliporwa mali zake kwa nguvu.
Amesema hoja inayobishaniwa ni iwapo mrufani ndiye aliyetenda matukio yote mawili kama alivyoshitakiwa nayo.
Jaji Mugeta amesema ushahidi wa moja kwa moja wa tukio lilivyotendeka aliutoa mwathirika hakuweza kumtambua mrufani (Mwanyigo).
Badala yake amesema ushahidi unaomuunganisha na tukio ni wa mpelelezi kwamba karibu na eneo la tukio kwenye korongo alipata nguo za mtuhumiwa ambazo waosha magari wenzake eneo la Ndiuka waliozitanbua kuwa ni za Mwanyigo.
"Hata hivyo, waosha magari hao hawakuletwa mahakamani kuthibitisha jambo hili, kinyume chake, mrufani aliwaleta mahakamani mashahidi watatu, ambao walisema muda na siku inayodaiwa tukio kutendeka walikuwa naye kwenye kijiwe chao cha kuosha magari katika eneo la Ndiuka," amesema.
Jaji Mugeta amesema ushahidi wa upande wa mashtaka una matatizo makuu mawili ya msingi.
Amebainisha la kwanza ni mwathirika katika ushahidi hakusema aliwaeleza polisi wajihi wa mtuhumiwa ambao uliwasaidia katika upelelezi na kumkamata mrufani na utambuzi wake kwenye gwaride la utambuzi lililoendeshwa na shahidi wa pili.
"Kueleza wajihi na hata mavazi ya mtuhumiwa ni sharti la msingi la kisheria la kufanya mahakama imwamini shahidi mtambuzi aliyeona kwa macho na kuleta thamani ya kiushahidi linapofanyika gwaride la utambuzi," amesema Jaji Mugeta akirejea uamuzi uliowahi kutolewa na Mahakama ya Rufani.
Amesema kwa msingi huo utambuzi wa mwathirika kwa mrufani kwenye gwaride la utambulisho na mahakamani bila ushahidi wake wa jinsi alivyomwelezea mtuhumiwa baada ya tukio kwa watu wengine na gwaride lenyewe la utambuzi, havina thamani kiushahidi na ni batili.
"Ninatambua katika ushahidi wake, shahidi wa nne (mpelelezi wa kesi) alisema mwathirika alimweleza kuwa mnyanganyi na mbakaji alikuwa mweusi, mwenye pua kubwa na mrefu wastani," amesema Jaji Mugeta na kuongeza:
"Hata hivyo, shahidi wa nne hakueleza kuwa mrufani ndiye mtu pekee ambaye ni mweusi, mwenye pua kubwa na mrefu wastani na ni kwa namna gani wajihi huo ulimsaidia yeye kubaini mhalifu na shahidi wa kwanza (mwathirika) kumtambua kwenye gwaride la utambuzi."
Jaji Mugeta amesema tatizo la pili katika ushahidi huo ni namna polisi walivyombaini mtuhumiwa, kutumia utambuzi wa nguo zake zilizokutwa korongoni jirani na eneo la tukio bila kuwaleta mahakamani mashahidi waliotambua nguo hizo.
Amesema kutofika kwa mashahidi hao kunafanya ushahidi wa mpelelezi kuwa nguo zilizokutwa karibu na eneo la tukio ni za mrufani kuwa ushahidi wa kuambiwa, ambao hauna nguvu kisheria chini ya kifungu cha 62 cha Sheria ya Ushahidi.
Amesema kwa mambo hayo mawili, ameridhika utambuzi wa mrufani kama mkosaji unatia shaka.
"Katika shauri hili mrufani hakutambuliwa ipasavyo, hivyo asingetiwa hatiani hata bila ya kujitetea. Kwa msingi huo, licha ya kuhuzunishwa na tukio lililompata mwathirika, siyo halali wala haki kisheria mrufani abebe msalaba kwa tuhuma ambazo hazina ushahidi wa kuzithibitisha."
"Ninahitimisha kwamba licha ya tukio kufanyika mchana, hakuna ushahidi toshelevu kuthibitisha kuwa lilitendwa na mrufani," amesema.
Amesema ni makosa kuamini kuwa kila tukio linalofanyika mchana mtambuzi hawezi kukosea katika utambuzi wake hasa kwenye mazingira ambayo muathirika na mtuhumiwa hawafahamiani.
"Hivyo, hatia ninaifuta na adhabu yake nimeibatilisha. Rufaa imeshinda. Mrufani aachiwe huru kutoka gerezani anakoshikiliwa mara moja isipokuwa kama kuna sababu nyingine nje ya shauri hili inayohalalisha kuendeleza kushikiliwa kwake," ameamuru Jaji Mugeta.