Prime
Kapteni JWTZ aachiwa huru mauaji ya kigogo Polisi
Muktasari:
- Wakati kesi hiyo ikianza, Kepteni Sudi Mabena alishtakiwa kwa mauaji ya kukusudia ya ASP Laurent Minja yaliyotokea siku moja kabla ya Sikukuu ya Krismasi mwaka 2017 katika klabu ya River Road baa iliyopo Kibaha mkoani Pwani, kabla ya kubadilishwa shtaka na kuwa la mauaji ya bila kukusudia.
Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Tanzania, imemwachia huru Kapteni wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Sudi Mabena, aliyeshtakiwa kwa kosa la kumuua afande wa Polisi, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Laurent Minja.
Awali, Kapteni Mabena alishtakiwa kwa mauaji ya kukusudia ya ASP Minja yaliyotokea siku moja kabla ya sikukuu ya Krismasi mwaka 2017 katika klabu ya River Road Baa iliyopo Kibaha mkoani Pwani, kabla ya kubadilishwa na kuwa mauaji ya bila kukusudia.
Hata hivyo, muda wote tangu kukamatwa kwake, kusikilizwa kwa kesi yake na kuonekana ana kesi ya kujibu na kujitetea, alikuwa akikana kuhusika hadi Ijumaa Machi 8, 2024 alipoachiliwa huru na Mahakama Kuu, kanda ya Dar es Salaam.
Upande wa mashtaka uliwakilishwa na mawakili wa Serikali, Emmanuel Maleko, Sofa Gimbija, Clemence Kato na Joseph Isaka wakati kwa mshtakiwa alitetewa na mawakili Dominiscus Nkwera, Yohana Kibinda na Francis Munuo.
Tukio la mauaji lilikuwaje
Maelezo ya kosa hilo yalieleza kuwa usiku wa Desemba 24, 2017, ASP Minja alikuwa miongoni mwa wateja waliokuwapo baa ya River Road ambayo ilikuwa na ‘Live’ Band, nightclub na kuuza vinywa mbalimbali kwa lengo la kuvutia wateja.
Wakati akiendelea kuburudika, starehe yake ilikatizwa ghafla baada ya kuingia katika mzozo na kupigana ambako matokeo yake, yalisababishwa apigwe kabla ya kupelekwa Hospitali teule ya Tumbi iliyopo Kibaha kwa matibabu.
Ingawa ASP Minja aliruhusiwa siku iliyofuata, afya yake haikuimarika, hivyo akapelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili -Mloganzila kwa matibabu zaidi.
Alipewa rufaa kwenda Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi) na baadaye akarudishwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ambako alilazwa.
Akiwa MNH alilazwa kwa siku kadhaa, lakini kwa bahati mbaya hali yake haikuimarika na ilizidi kuwa mbaya hadi alipofariki dunia Januari 12, 2018 na uchunguzi (post-mortem) ulionyesha viungo vilishindwa kufanya kazi na alikuwa na majeraha.
Kepteni Mabena alidaiwa ndiye aliyemshambulia ASP Minja usiku wa Desemba 24, 2017, alikamatwa na kushtakiwa kwa mauaji ya kukusudia ambayo hata hivyo baadaye yalibadilishwa na upande wa Jamhuri na kuwa kuua bila kukusudia.
Hati ya mashtaka ilieleza kuwa Desemba 25, 2017 katika baa ya River Road, iliyopo Kibaha mkoani Pwani, mshtakiwa alisababisha kifo cha ASP Minja, mashtaka aliyokana na hata katika utetezi wake aliyakana.
Walichokisema mashahidi
Shahidi wa kwanza, Rose Shayo aliyekuwa mhudumu wa kaunta, alieleza kuwa siku ya tukio, ASP Minja alifika saa 1:00 jioni na yeye ndiye aliyemhudumia na baadae alifika mshitakiwa akiwa na dada mmoja akiulizia huduma ya M-Pesa.
Shayo aliieleza mahakama kuwa ASP Minja alimuonya asiwasikilize, akisema watu hao ni matapeli na kwamba kutokana na kauli hiyo, mshtakiwa na mwanamke huyo walimfuata marehemu hadi chooni alikokuwa amekwenda kujisaidia.
Wakati akijibu maswali ya dodoso kutoka kwa mawakili wa mshtakiwa, shahidi huyo alisema hakushuhudia tukio lililotokea mbali na kaunta na kwamba watu wengi walikuwa wakienda mara kwa mara msalani ndani ya baa hiyo.
Shahidi wa pili, Aziza Mhigi ambaye ni matroni wa wahudumu, alieleza siku ya tukio alikuwa akiwakatia wateja tiketi za kuingia nightclub, aliona watu wawili karibu na ngazi wakimshambulia marehemu ambaye ni afande Minja.
Baada ya kupewa nafasi ya kujikumbusha, alisema alimuona marehemu akizungumza na simu ya kiganjani na kushambuliwa kichwani na mtu aliyemtambua kama mrefu na mweusi na pia alimtambua kwenye gwaride la utambuzi Polisi.
Alipohojiwa na mawakili wa utetezi, shahidi huyo alikiri kwamba hakumtambua mshtakiwa siku ya tukio na pia alishindwa kufafanua kuhusiana na shambulizi wala nguo alizokuwa amevaa mshtakiwa na kushindwa kueleza aliona nini hasa.
Kwa upande wake, shahidi wa tatu, Inspekta Msaidizi Kilian, alieleza siku hiyo alikuwa ndani ya baa akihudhuria tafrija ya rafiki yake ya kumbukumbu ya kuzaliwa na alishuhudia mtu mmoja akimshambulia mwingine.
Alisema tukio hilo lilitokea karibu na steji ya ‘Live Band’, na alikwenda eneo hilo na kuona mtu amelala chini na alimtambua kuwa ni afande Minja na hapo alimkamata mshtakiwa na kumpeleka kituo cha Polisi kilichopo Kibaha.
Shahidi wa nne, Inspekta Geofrey Kaluse alielezea namna alivyoendesha gwaride la utambuzi wakati shahidi wa tano, Esther Minja ambaye ni mke wa marehemu, alieleza namna alivyopokea simu ikimjulisha mumewe amejeruhiwa.
Kwa upande wake, shahidi wa sita, Dk Benjamin Kiteleke ambaye alimhudumia ASP Minja katika Hospitali ya Tumbi, alieleza alimpokea ASP Minja akiwa hajitambui na alikuwa amekunywa pombe na alikuwa na majeraha kwenye pua.
Shahidi wa saba ni Koplo Danstan, aliyekuwa mpelelezi wa kesi, alichora ramani ya eneo la tukio na kwenda MNH ambapo alikutana na Dk Leah ambaye alichunguza mwili wa marehemu na kubaini jeraha kichwani na damu ilivuja kwa ndani.
Uchambuzi wa ushahidi
Hukumu ya kumwachia huru ilitolewa na Jaji Sedekia Kisanya ambaye mbali na kukubaliana na maoni ya wazee washauri wa mahakama kuwa kepteni huyo wa Jeshi hakuwa na hatia ya kosa la mauaji ya bila kukusudia aliloshtakiwa nalo.
Lakini Jaji akaenda mbali zaidi na kusema upande wa mashtaka ulishindwa kutimiza wajibu wake wa kubeba mzigo wa kuthibitisha shtaka pasipo kuacha mashaka yoyote, hivyo kwa msingi huo anaamuru kuachiliwa huru kwa Mabena.
Jaji alisema kwa ujumla wake, ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa mashitaka, ulishindwa kujenga msingi katika kipengele cha kama marehemu aliuawa bila uhalali na mshitakiwa, hivyo mshitakiwa hana hatia na kosa hilo.
Akichambua ushahidi wa mashahidi saba wa Jamhuri, Jaji alisema kulikuwa na mkanganyiko ni eneo gani hasa la tukio kati ya ngazi za kuelekea kwenye klabu ya usiku katika baa hiyo, ama lilitokea katika steji ya ‘live’ band katika baa hiyo.
Lakini hata hivyo Jaji alisema mkanganyiko huo haukuathiri hoja ya msingi kuwa kosa lilitendeka katika baa ya River Road iliyopo eneo la Picha ya Ndege Kibaha.
Mbali na hoja hiyo, Jaji Kisanya alisema kama mshtakiwa alikamatwa na polisi na baadaye kupewa dhamana ya polisi, ilitegemewa mtuhumiwa alipewa masharti ya dhamana ikiwamo tarehe ya kuripoti kituo cha polisi na wadhamini wake.
“Hakuna kitu chochote kinachoonyesha kwamba kukamatwa kwa mara ya pili kwa mshtakiwa kulitokana na kuruka masharti ya dhamana. Pia Ofisa wa Polisi aliyempa dhamana wala aliyemkamata Mgulani JKT hawakutoa ushahidi,” alisema.
Jaji alisema shahidi wa pili wa Jamhuri alionyesha kuwa marehemu alipigwa na watu wawili bila kueleza kama mshtakiwa alikuwa miongoni mwao na ni baada ya kujikumbusha ndipo akasema aliona watu asiowafahamu wakimshambulia Minja.
“Shahidi aliendelea kueleza huyo aliyekuwa akimshambulia marehemu alikuwa mrefu na mweusi na kwamba alimtambua katika gwaride la utambuzi, lakini alipododoswa alikana kumtambua ila alimtambua hapa mahakamani,”alisema.
Jaji alisema ni ushahidi ulio dhahiri kuwa shahidi huyo wa pili hakumtambua mshtakiwa katika tarehe ya tukio. Kukiri huko kunaibua maswali kuhusu namna baadaye alivyomtambua katika gwaride la utambuzi polisi,”alieleza.
Kutokana na sababu hizo, Jaji alisema anamuona mshtakiwa Kepteni Sud Hussein Mabena kuwa hana hatia katika kosa la kuua bila kukusudia, kinyume cha kifungu 195 na 198 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 kama kilivyorekebishwa 2022.