DPP atwishwa zigo hukumu kesi ya mjane wa Bilionea Msuya

Dar es Salaam.Wakati maswali kuhusu mhusika wa mauaji ya Aneth Msuya na mahali aliko yakiendelea kugonga vichwa vya jamii na wadau wa masuala ya sheria na haki za binadamu, Jeshi la Polisi limesema haliwezi kuzungumzia hukumu ya Mahakama.

Badala yake limeeleza kuwa sheria inaelekeza kama mtu hajaridhika na hukumu,  anaweza kukata rufaa.

Dada wa bilionea Erasto Msuya, Aneth Msuya wakati wa uhai wake

Aneth alikutwa amefariki dunia nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, wilayani Temeke (wakati huo), jijini Dar es Salaam, asubuhi ya Mei 26, 2016.

Alikuwa ni mdogo wa aliyekuwa mfanyabiashara maarufu wa madini mkoani Arusha, Erasto Msuya, maarufu kama Bilionea Msuya, aliyeuawa kwa kupigwa risasi eneo la Mijohoroni, wilayani Hai, Mkoa wa  Kilimanjaro, Agosti 7, 2013.

Kwa mujibu wa ripoti ya uchunguzi wa sababu za kifo cha Aneth iliyowasilishwa mahakamani na kupokelewa kuwa kielelezo cha upande wa mashtaka,  ni kuvuja damu nyingi kwenye jeraha lililotokana na kukatwa shingo na kutenganisha koromeo kwa kitu chenye ncha kali.

Jamhuri kupitia Jeshi la Polisi, chombo chenye dhamana ya ulinzi na usalama wa raia na mali zao, pia ofisi ya uchunguzi wa makosa ya jinai, iliwashtaki wifi wa marehemu Aneth, Miriam Mrita, ambaye ni mjane wa Bilionea Msuya na Revocatus Muyella maarufu Ray, kuhusu mauaji hayo.

Mjane wa Bilionea Msuya, Miriam Mrita akishangilia baada ya kushinda kesi ya mauaji iliyokuwa inamkabili yeye na mwenzake Revocatus Muyella katika chumba cha Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, jana jijini Dar es Salaam. Picha na Sunday George

Mahakama katika hukumu iliyosomwa Ijumaa, Februari 23, mwaka huu na Jaji Edwin Kakolaki aliyeisikiliza kesi hiyo ya jinai namba 103/2018, iliwaachia huru washtakiwa wote baada ya kuwaona hawana hatia kwa mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili.

Mahakama ilifikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha kuwa upande wa mashtaka,  ulishindwa kuwasilisha ushahidi kuthibitisha bila kuacha shaka kuwa washtakiwa hao ndio waliohusika na mauaji hayo.

Miongoni mwa ushahidi uliokuwa unategemewa na upande wa mashtaka ni wa uchunguzi wa kisayansi, hasa wa vinasaba.

Ushahidi huo ni kuoana kwa  vinasaba katika vielelezo viwili vilivyokutwa eneo la tukio la mauaji (ulikokuwa mwili wa marehemu) ambavyo ni kisu na filimbi, pamoja na vinasaba vilivyopatikana katika sampuli ya mpanguso wa mate ya mshtakiwa wa pili, Muyella.

Hata hivyo Jaji Kakolaki alisema kuwa licha ya ushahidi huo kuonyesha mshtakiwa wa pili alikuwapo eneo la tukio la mauaji au aliwezesha vielelezo hivyo kuwepo eneo la tukio,  upande wa mashtaka haukuweza kuwasilisha ushahidi unaothibitisha ndiye aliyetenda kosa hilo.

Alisema kutokuwepo ushahidi wa vinasaba kwenye makali ya kisu hicho, kunaonyesha vinasaba hivyo ni vya marehemu Aneth,  hivyo kunaifanya Mahakama ibaki na shaka kama kweli kisu hicho ndicho kilichotekeleza mauaji hayona  kumhusisha mshtakiwa wa pili.

Alihitimisha kuwa mtu kuwepo tu eneo la tukio hakuwezi kuthibitisha uhusika wake na tukio bila kuwepo ushahidi unaothibitisha kuhusika kwake bila kuacha shaka yoyote.

Kutokana na hitimisho hilo la Mahakama ndipo yanaibuka maswali, nani aliyehusika au waliohusika na mauaji hayo, wako wapi na namna gani watapatikana ili wachukuliwe hatua na hatimaye kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria?


Mzigo kwa DPP

Mwananchi linatambua kuwa katika aina hiyo ya kesi, anayeweza kukata rufaa ni  Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Wakili, Constantine Kakula alisema kwa kesi za jinai  Serikali kupitia ofisi ya DPP ndiyo yenye wajibu wa kukata rufaa kama inaona ina hoja za msingi kupinga uamuzi huo.
Naye wakili, Francis Stolla akizungumza na gazeti hili juzi alisema ambacho Serikali inaweza kufanya dhidi ya walioshinda kesi ni kukata rufaa na kama ina ushahidi mpya, inaweza kuomba iruhusiwe kuuwasilisha ili Mahakama iweze kuuzingatia.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Sylvester Mwakitalu hakupatikana kuzungumzia hukumu hiyo na kama ofisi yake ina mpango wa kukata rufaa.

Simu yake ya mkononi iliita bila kupokewa na hata alipoulizwa kupitia ujumbe mfupi (sms) na kupitia mtandao wa WhatsApp, hakujibu chochote.


Kauli ya Polisi

Msemaji wa Jeshi la Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi, David Misime, amesema ni vigumu kuzungumzia maamuzi yaliyotolewa na Mahakama kwa sababu sheria inasema kama mtu hakuridhika na hukumu anakata rufaa.

"Na hamna chombo ambacho kina uwezo wa kuanza kuchambua kuwa aah! unajua sijui nini. Ziko taratibu za kisheria, kwa hiyo mimi siwezi kulizungumzia hilo.... amesema na kuongeza:

"Huko unakotaka kunipeleka siko, sheria haituelekezi hivyo na wala haimuelekezi mtu yeyote hivyo. Polisi hatuwezi kuizungumzia maana tuna taratibu zetu za kisheria. Lazima tufuate taratibu za kisheria."


Kachero mstaafu na udhaifu mifumo ya  upelelezi

Akizungumzia taratibu za upelelezi katika kesi za makosa ya jinai yakiwemo mauaji, kachero na Kamanda wa Polisi  wa mkoa mstaafu,  Jamal Rwambow amesema uchunguzi kwa kesi hizo unapaswa kutoacha shaka yoyote.

Amesema kama wapelelezi hawatatekeleza vema wajibu wao na kuacha shaka, basi Mahakama inakuwa haina namna zaidi ya kumnufaisha mshtakiwa kwa mashaka hayo.

Rwambow ambaye amewahi kushika nyadhifa mbalimbali katika Jeshi la Polisi, hasa Idara ya Upelelezi ngazi ya wilaya, mkoa mpaka wadhifa wa Kamanda wa Polisi Mkoa,  amesema katika kesi za mauaji inapokuwa imetumika silaha kama vile kisu kinapaswa kufanyiwa uchunguzi usioacha shaka.

Amesema katika hali ya kawaida kisu hicho kama kina damu, uchunguzi unapaswa ufanyike kwanza kujua kama damu hiyo ni ya mnyama au ni ya binadamu na kama ni binadamu, basi ni ya nani.

"Lakini mimi (mpelelezi) ninachotafuta ni damu inayofanana na ya marehemu. Ukishabaini kuwa ni damu ya marehemu lazima sasa uhusianishe na mtuhumiwa katika vitu vingi," amesema Rwambow na kufafanua:

"Kwa hiyo unaweza kuchunguza vinasaba vinavyopatikana kwenye kisu hicho kwamba ni vya mtuhumiwa, ni vya marehemu (mwenyewe) au vya nani. Vyote hivi lazima uvipate kuondoa mashaka yoyote."

Amesema ukichunguza ukakuta vinasaba vilivyoko kwenye kisu chenye damu ya marehemu ni vya marehemu, inaashiria kisu kilitumika na marehemu mwenyewe.

"Lakini sasa kimetumikaje na marehemu, alikuwa anakitumia katika kukatia vitunguu au alikitumia kujiua? Kwa hiyo ili Mahakama iweze kuona kwamba huyu (mshtakiwa) ana hatia lazima maswali yote yanayoacha shaka yawe yamejibiwa kwa ushahidi," alisema.

Rwambow amesema, "Sasa kama mtu anaulizwa, bwana ulichukua vinasaba vya marehemu, kama haukufanya hivyo, kunaweza kuleta shaka ambayo Mahakama inampa faida mshitakiwa. Ikifikia hayo mashaka kwenye kesi ya mauaji,  mtu anaweza kuachiwa tu."

Rwambow amesisitiza katika kuchunguza kesi za mauaji unapoacha kuunganisha mambo hayo yote ama kwa uzembe au kwa makusudi,  ni rahisi kupoteza kesi hata kama inaonekana iko wazi.

Amesema hata kama kisu kilichokuwa eneo la tukio kikikutwa na vinasaba vya marehemu, ni lazima ushahidi uonyeshe kilifikaje pale na kama ni yeye aliyekitumia.

"Yaani ni lazima kuwepo na ushahidi wa kuunganisha mpaka ifikie mahali Mahakama iseme kwa ushahidi huu, washtakiwa wanahusika na mauaji haya," amesema

Amehoji kama damu ya marehemu haikuchukuliwa kuchunguzwa kulinganisha na damu iliyoko kwenye kisu inawezekanaje kusema hicho kisu ndicho kilitumika kwenye mauaji hayo?

"Yaani katika vielelezo vyote unashindwa kuchukua sampuli ya damu ya marehemu? Hii ni poor and weak investigation (uchunguzi dhaifu). Kama wapelelezi hawakupeleka kwa Mkemia sampuli ya damu ya marehemu ichunguzwe ilinganishwe na iliyokuwa kwenye kisu hawakutimiza wajibu wao,” amesema.

"Sasa hawakutimiza kwa kutojua au kwa kukataa kupata ukweli. Kama kisu kina damu lazima kuchunguza na kuoanisha. Damu ya kisu ni kundi gani ya marehemu ni kundi gani na ya washtakiwa ni kundi gani. Kwa hiyo wapelelezi hawakupaswa kuharakisha," amesema Rwambow.

Hata hivyo, amesema jalada la uchunguzi wa kesi mpaka liende mahakamani linapitia Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS),  na akahoji ilikuwaje nao hawakuweza kuona pengo hilo na kulirejesha Polisi ili kulishughulikia?

"Kwa hiyo, wakati fulani watu wanaweza kuonekana hawakutenda haki kumbe tu matakwa ya kisheria katika kuthibitisha hayakukamilishwa. Na kama wanadhani kwamba hayo yalithibitishwa, bado upande ule ambao unaona kwamba haukutendewa haki, una haki ya kukata rufaa na jopo la majaji litaangalia,” amesema.