Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ummy: Wananchi fichueni watumishi wazembe kwa namba 199

Muktasari:

  • Serikali imesema itaendelea kuwachukulia hatua watumishi wa afya wasiofuata maadili ya kazi zao, pamoja na usimamizi usioridhisha.

Dar es Salaam. Kufuatia malalamiko ya changamoto za ubora wa huduma za matibabu katika vituo vya afya, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ameitaka jamii iwaifichue watumishi wanaokwenda kinyume kwa kupiga simu namba 199.

 Hatua hiyo imekuja siku kadhaa tangu kuibuka kwa matukio ya wanawake kukosa huduma bora wakati wa kujifungua na malalamiko yaliyotolewa mitandaoni kuhusu kukosekana kwa huduma zenye staha kwa kundi hilo.

Waziri Ummy amesema hayo leo Ijumaa, Januari 5, 2024 akiwa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) wakati akipokea vifaa vya kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto vyenye thamani ya Sh14.9 bilioni.

Amesema wizara imebaini kuna upungufu kwenye weledi na ujuzi kwa baadhi ya wahudumu wa afya, hiyo ni pamoja na usimamizi usioridhisha na utoaji huduma bora.

Hata hivyo, ameitaka jamii kutoa ushirikiano kwa Serikali kwa kutoa taarifa ikiwa kuna uzembe unafanyika, ili hatua zichukuliwe.

“Jamii iwaibue wale ambao si wazuri, wanaofanya kazi kinyume. Aliyekosea tuleteeni jina lake, tarehe fulani alinifanyia hivi na vile na ushahidi na sisi tutachukua hatua.

“Piga simu namba 199 bila malipo utuambie ni kituo gani, halmashauri gani, sisi itatusaidia kufanya ufuatiliaji wa karibu kuanzia ngazi ya mkoa na halmashauri, Serikali itachukua hatua za haraka pale zinapojitokeza changamoto za sekta ya afya,” amesema waziri huyo.

Amesema changamoto za sekta ya afya zinaongezeka kila siku, akitaja sababu ya ongezeko hilo kuwa ni kukua kwa idadi ya watu na mtindo wa maisha.

Hata hivyo, amesema watumishi wengi wanaotoa huduma za afya wamekuwa wakifanya kazi kubwa kwa muda mrefu na wana weledi isipokuwa ni wachache.

 “Watumishi wengi wa afya wanafanya vizuri wanajitahidi na kujitoa, mpaka sasa wauguzi wengi wanaumwa migongo. Ikama tunayo isiyotosheleza ijapokuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameshaajiri watumishi 28,000 kwa kipindi cha miaka mitatu wameongezeka kidogo.

 “Tusiwahukumu watumishi wote wa afya, wengi ni wazuri, hakuna daktari anafurahia kupata kifo cha mjamzito wengi wanajitahidi kuokoa maisha ya kinamama wengi,” amesema.

Amesema kwa sasa mwelekeo wa wizara ni kwenda kuimarisha usimamizi wa utoaji wa huduma za afya, timu ya uendeshaji afya ya wilaya na halmashauri na kwamba wanapitia muundo wa timu za uendeshaji.

Akizungumza leo  na waandishi wa habari, Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi amesema wananchi wanapaswa kutoa taarifa pindi wanapoona kuna ukiukwaji wa utoaji huduma za afya.

“Haipaswi mtumishi wa afya kwenda kinyume na maelekezo ya Serikali, wito umetolewa wananchi kutoa taarifa ya kituo au mtumishi husika na namba imetolewa wasiogope kutoa taarifa, ili kuleta mabadiliko tunayoyahitaji,” amesema Matinyi.


Vifaatiba

Awali, akizungumzia vifaatiba, Waziri Ummy amesema Serikali imeweka fedha hizo kununua vifaa tiba, ili kufanikisha juhudi za kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kutoka 104 vya sasa kufikia chini ya 70 ifikapo mwaka 2030.

Amesema hizo ni jitihada zinazofanywa na Rais Samia pamoja na wadau wa afya katika kuhakikisha nchi inafikia malengo ya kitaifa na kimataifa.

“Malengo endelevu ya Milenia 2030 yanayotutaka kupunguza athari za vifo vitokanavyo na uzazi hadi kufikia chini ya 70 katika kila vizazi 100,000 vifo vya watoto chini ya 38 katika kila vizazi hai 1, 000,” amesema.

Amesema katika kuhakikisha hilo linafanikiwa, Serikali imejenga wodi za uangalizi maalumu wa watoto wachanga walio mahututi kwa mara mbili zaidi kutoka 99 mwaka 2021 mpaka kufikia wodi 189 mwaka 2023.

Amesema hiyo imesaidia watoto wengi waliozaliwa na uzito wa gramu 500 mpaka 600 na wale wanaozaliwa miezi mitano ya ujauzito au sita wanaishi.

Amesema juhudi hizo wamezipeleka pia katika upatikanaji wa vifaa vya afya ya uzazi kutoka asilimia 82.5 mwaka 2021 hadi 88.2 mwaka 2023.

 “Kwa upande wa vitanda vya kutolea huduma za uzazi, Serikali kwa kushirikiana na wadau imeendelea kuboresha upatikanaji wa vifaatiba hivyo kwa ajili ya huduma za afya ya uzazi ambapo hali ya vitanda vya kutokea huduma kwenye vituo vya afya imeongezeka kutoka 84,162 mwaka 2021 mpaka vitanda 104,687 mwaka 2023,” amesema.

Vifaa hivyo alivyopokea leo ni pamoja na vitanda vya wagonjwa 3080, vya kujifungulia 1000, magodoro 5,500, mashuka 36,808, meza za vitanda 306 vifaa mbavyo vitasambazwa katika majimbo 214 kwenye vituo 428 katika mikoa yote 26.

“Kila jimbo litapata vitanda 30, magodoro 30 na mashuka 120 na vitanda vya kujifungulia 20 na meza 15,” amesema.

Pia amesema wanatarajia kupokea vifaa tiba vingine ikiwemo vitanda vya kujifungulia 4280, vitanda vya kufanyiwa uchunguzi 4280, mkoba wa vifaa vya kujifungulia 4280, kabati za vitanda 6420 na stendi ya dripu 6420.

Taarifa za utafiti wa Demographia ya Afya ya Uzazi na Viashiria vya Malaria (TDHS/MIS) ya mwaka 2022 zinaonyesha nchi imepiga hatua katika viashiria vingi vya afya ya mama na mtoto.

“Vifo vitokanavyo na uzazi vimeshuka kutoka 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2015/16 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000 na vifo vya watoto chini ya miaka mitano vimeshuka kutoka 67 kati ya vizazi hai 1,000 mwaka 2015/16 hadi 43 kwa kila vizazi hai 1,000.

“Hii ni sawa na kupunguza vifo vya wajawazito kutoka 11,000 hadi vifo 2,500 kwa mwaka,” amesema Waziri Ummy.