Ukosefu wa ajira kwa vijana unavyozalisha ‘uchawa’

Mmoja wa washirkiki azingumza kwenye mdahalo wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, uliojadili tatizo la ajira kwa vijana leo Mei 30, 2024. Picha na Marian Mbwana

Muktasari:

  • Ukosefu wa nguvu za kiuchumi unaelezwa kusababishwa na mambo kadhaa, ikiwemo ukosefu wa ajira, ambao ni changamotoo kubwa inayowasumbua vijana na kuwafanya wajipendekeze ili kupata fadhila.

Dar es Salaam. Vijana kukosa mamlaka ya kisiasa na nguvu za kiuchumi, kumetajwa kuwa chimbuko la baadhi yao kujitafutia fursa kwa kugeuka ‘chawa.’

Chawa ni mdudu anayeishi mwilini kwa kunyonya damu, ambaye anafananishwa na vijana ambao wamekuwa wakijipendekeza na wakiwaganda watu wenye nacho au viongozi ili kujitafutia masilahi binafsi.

Ukosefu wa nguvu za kiuchumi unaelezwa kusababishwa na mambo kadhaa, ikiwemo ukosefu wa ajira, ambao ni changamoto kubwa inayowasumbua vijana.

Matokeo yake inaelezwa wahitimu wengi wa vyuo vikuu wamerejea kufanya kazi walizofanya wazazi wao kama vile umachinga, mama na baba lishe na sasa kuendesha bodaboda, ambazo awali zilionekana ni kazi za watu wenye kiwango kidogo cha elimu na wengine wameona ‘uchawa’ ni fursa mpya.

Hayo yalielezwa jana na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Sabatho Nyamsenda katika mdahalo wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, uliofanyika katika ukumbi wa Maktaba, chuoni hapo.

Mdahalo huo uliongozwa na kaulimbiu isemayo ‘Vijana na safari ya umoja na ukombozi wa pili wa Afrika.’

Mbali na hilo, Nyamsenda amesema vyombo vya habari navyo vimetumika kueneza uchawa kama tunu mpya ya Taifa.

"Wanaojiita machawa huonekana mara kadhaa wakidhihaki elimu kwa kusambaza video wakiwakejeli vijana wenye elimu wasio na ajira au wenye mshahara mdogo, huku wakisema kusoma ni kupoteza muda," amesema.

“Sijawahi kuona Waziri wa Elimu akikemea tabia hii, cha kushangaza machawa hawa hualikwa kusherehesha dhifa za kitaifa, jambo linalosababisha wengi kudhani ujumbe unaoenezwa na machawa hawa una baraka za viongozi. Si ajabu kuwa hata vijana wa vyuo vikuu wameanza kuiga mtindo huu,” amesema.

Kauli ya Nyamsenda iliungwa mkono na Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya Chama cha ACT-Wazalendo, Abdul Nondo aliyesema kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla bado ushiriki wa vijana katika nyanja za kiuchumi na kisiasa ni mdogo.

Amesema kwa mujibu wa utafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Maendeleo ya Jamii na Uchumi (Repoa) wa mwaka 2019, kati ya vijana milioni moja wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka, ni vijana 50,000 hadi 60,000 ndio hupata ajira katika sekta rasmi, huku waliobaki hugeukia kujiajiri na kuingia sekta isiyo rasmi.

Amesema hata katika sekta ya kilimo ambayo huzalisha ajira kwa asilimia 65, bado ushiriki wa vijana si wa kuridhisha kutokana na ugumu wa upatikanaji wa ardhi, mfumo wa elimu, mitaji na masoko.

Amesema vijana wengi walioajiriwa kwenye viwanda, ujira wao kwa siku si zaidi ya Sh10, 000 na wa mashambani badala ya kulima mazao kujipatia kipato, wamegeuzwa manamba, wakilima kwa ajili ya wenye mitaji, kwa siku kijana akipokea ujira wa Sh7, 000.

Amesema vijana hao wengi hawana mikataba, mfumo wa hifadhi ya jamii wala bima ya afya, jambo linalowaweka kwenye hatari kubwa ya kuendelea kuishi chini ya mstari wa umasikini.

Nondo amesema vijana wanaomaliza vyuo sasa wanaambiwa wakajitolee nguvu kazi zao bure kwanza, ndipo waajiriwe, ingawa kujitolea hakujaratibiwa na kuwa na mwongozo mzuri.

Amesema hata kupata nafasi ya kujitolea katika sekta mbalimbali sasa ni sawa na kuomba ajira.

Mbali na msisitizo uliowekwa kupitia sera ya Maendeleo ya vijana ya mwaka 2007, na mikataba ya kimataifa kama African Youth Charter ibara ya 11 kusisitiza ushiriki wa vijana katika masuala ya uongozi na siasa, amesema bado ushiriki wao ni mdogo.

“Nchini Tanzania mbali ya vijana kuwa nguvu kazi ya Taifa kwa asilimia 55, bado tunakumbana na changamoto kubwa ya kiuchumi, kuendelea kuwa katika tabaka la chini la wasio nacho, ukosefu wa ajira na umasikini wa kipato limekuwa ni tatizo na kilio kikubwa kwetu,” amesema.


Alitoa mfano wa ushiriki wa vijana katika kupiga na kupigiwa kura, akidai unazidi kupungua.

Alibainisha miongoni mwa sababu ni ugumu wa maisha na ukosefu wa ajira, jambo linalowafanya kujikita zaidi katika shughuli za kiuchumi na kuacha kutenga muda kwa ajili ya mambo ya kisiasa.

Kijana huyo amesema baadhi ya vijana hawaamini kura kama ni njia ya kutatua changamoto walizonazo kama vile ajira na ugumu wa maisha.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Dk John Kallage amesema sasa ni wakati wa kutafakari na kuchambua kwa kina maudhui ya mifumo iliyopo na utekelezaji wake katika kumuandaa mtoto na kijana kuishi katika Taifa hili na dunia ya vijana.

Amesema uzoefu unaonyesha Tanzania imefanikiwa kuwa na mifumo, sera na miongozo mizuri katika maeneo mbalimbali. Hata hivyo, haitekelezeki kwa ufanisi.

"Ukweli huu pia unahusu sekta ya elimu ambayo ni kitovu cha kuwaandaa vijana kujenga umahiri unaohitajika katika karne ya 21. Ni vema kuwa na sera nzuri, miongozo na mipango mizuri, lakini vema zaidi kuona utekelezaji unaoakisi dhamira ya dhati iliyoko katika sera na mipango hiyo," amesema.