Malecela: Ajira si bomu la Tanzania pekee

Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela . Picha na Maktaba

Muktasari:

Akizungumza katika mahojiano maalumu nyumbani kwake Dodoma hivi karibuni, Malecela

Dodoma. Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela amesema mtu anayesema kwamba tatizo la ukosefu wa ajira ni bomu hajasema jambo jipya kwa kuwa limekuwapo kwa muda mrefu na pia ni la dunia nzima.

Akizungumza katika mahojiano maalumu nyumbani kwake Dodoma hivi karibuni, Malecela

alisema: “Nawaomba Watanzania wala tusilionee aibu. Mtu anaposema ni bomu hajasema jipya, ukosefu wa ajira ni jambo linalojulikana dunia nzima. Ni tatizo la kizazi hadi kizazi.”

Alisema hata nyaraka zinazoelezea Vita Kuu ya Pili ya Dunia zinabainisha kuwa wakati huo walikuwapo vijana wengi ambao hawakuwa na ajira.

Ingawa Malecela hakutaja jina la mtu, lakini kwa nyakati tofauti, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amenukuliwa akisema kuwa tatizo la ajira nchini ni bomu linalosubiri kulipuka, kauli ambayo imekuwa ikiungwa mkono na viongozi wa kada mbalimbali, wengi kutoka vyama vya upinzani.

Malecela ambaye hadi mwaka 2010 alikuwa Mbunge wa Mtera mkoani Dodoma, alieleza kuwashangaa baadhi ya Watanzania ambao wanadhani kuwa Serikali yao haifanyi lolote kuondokana na ukosefu wa ajira nchini bila kujua kuwa hilo ni tatizo la ulimwengu mzima.

“Uingereza kuna ukosefu wa ajira kwa vijana lakini tatizo lao kubwa ni kuchagua kazi. Sisi bado tunadhani tunaweza kupata kazi ya kufagia ofisini badala ya kwenda kukata mkonge,” alisema.

Suluhisho la ajira

Alisema ili Tanzania iweze kupunguza tatizo hilo, ni lazima iboreshe maisha ya watu katika maeneo ya vijijini ili kuwashawishi kubaki huko badala ya kwenda mjini kusaka ajira kama ilivyofanyika katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Tanga.

“Hata mkichunguza hamuwezi kuwakuta Wasambaa kutoka Lushoto jijini Dar es Salaam wakifanya umachinga. Nimekwenda Lushoto nikakuta kijana ana eka yake ya nyanya anailima na kupata tani kadhaa,” alisema.

Alisema miundombinu ya umwagiliaji ikiwekwa vizuri vijijini, yakiwamo mabwawa ya kutosha, ni wazi kuwa watu wengi watafanya shughuli za kilimo vijijini na hivyo kuwa rahisi kwa Serikali kuwasaidia.

Katika kuonyesha kuwa vijana wengi wamekuwa na tabia ya kuchagua kazi, Malecela alisema wakati akiwa serikalini aliyekuwa Waziri wa Mipango, Nsilo Swai alichukua vijana 3,000 kwenda kufanya kazi katika mashamba ya sukari Kilombero, lakini walirejea Dar es Salaam baada ya miezi mitatu tu licha ya kuwa walilipwa mishahara ya miezi miwili kabla na kupewa vitendea kazi.

Akitoa mfano wa pili alisema: “Mama Kunambi (DC wa Dar es Salaam wakati huo), aliwahi kuwachukua vijana 3,000 kwa ajili ya kufanya kazi katika mashamba makubwa na kuwalipa mshahara wa miezi miwili lakini baada ya miezi minne wote wakawa wamerudi Dar es Salaam.”

Wagombea urais

Akizungumzia hatua ya CCM kuwachukulia hatua makada wake sita kwa kitendo chao cha kuanza kampeni za urais mapema alisema: “Tufuate kanuni na utaratibu ulioko kwenye chama, tuangalie sana suala la fedha likianza kuingia kwenye uchaguzi hatutapata viongozi wa kweli ila tutapata viongozi wenye pesa.

Nchi ikianza kuwa na viongozi wenye pesa uwe na uhakika hapo mnajitafutia uhasama wa makundi. Kundi lilichonacho na kundi lisilonacho.”