Ukaguzi wa watu, mizigo katika kizuizi cha uvinza utaendelea

Muktasari:
Mbunge Mwilima amelalamikia ukaguzi huo
Kigoma. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema ukaguzi wa watu na mizigo unaofanywa katika kizuizi cha Uvinza mkoani Kigoma utaendelea kufanyika ili kudhibiti wimbi la uingizwaji wa silaha haramu nchini.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema hayo leo Jumapili, Julai 29, 2018 wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Uvinza akiwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi mkoani hapa.
“Lazima ukaguzi ufanyuke ili kujiridhisha kama watu wote wanaoingia nchini wamepita kihalali na kama hawapitishi silaha haramu na vitu vingine ambavyo haviruhusiwi kuingizwa nchini,” amesema Majaliwa
Majaliwa ametoa ufafanuzi huo baada ya Mbunge wa Kigoma Kusini (CCM), Hasna Mwilima kudai wananchi wengi wanapata usumbufu mkubwa kutokana na ukaguzi unaofanywa na maofisa wa Uhamiaji katika kizuizi cha Uvinza.
Waziri Mkuu amesema iwapo viongozi wa mkoa huo hawatakuwa makini katika kufanya ukaguzi kwenye vizuizi watasababisha watu wengi kuingia kiholela nchini hivyo kuathiri mipango ya Serikali ya kuwahudumia wananchi wake.
Pia, Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu Emanuel Maganga kufuatilia kwa umakini mwenendo wa utendaji kazi katika kizuizi cha Uvinza.
Waziri Mkuu amesema iwapo atabaini kuwapo kwa maofisa wa kizuizi hicho wanaojiashishughulisha na vitendo vya rushwa pamoja na kuwasumbua wananchi na abiria wanaopita kizuizini hapo awachukulie mara moja.