Ujio wa Chongolo waleta neema ya daktari, barabara kituo cha Afya Ifingo

Muktasari:

  • Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo ametoa saa 24 kwa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) kuanza ujenzi wa kilometa moja ya barabara inayoenda kituo cha Afya Ifingo, Mjini Mafinga na Mkuu wa Mkoa kuhakikisha daktari analetwa kituoni hapo.

Iringa. ‘Mgeni njoo, mwenyeji apone’ msemo huu unaweza kutumika na wananchi wa Kata ya Kinyanambo mkoani hapa baada ya ziara iliyofanywa na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo kusababisha kupatikana kwa daktari katika Kituo cha Afya cha Ifingo kilichopo eneo hilo.

Ziara ya Chongolo haijasaidia upatikanaji wa daktari tu bali pia kuanza kwa ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilomita moja kuelekea kituoni hapo.

Maagizo ya ukamilishaji ya masuala hayo yametolewa na Chgongolo leo Jumamosi Mei 27, 2023 alipotembelea kituo hicho na kusikia changamoto mbalimbali ambazo nyingi alijionea.

Akisomewa taarifa iliyoonyesha uhaba wa wataalamu wa afya akiwemo daktari na barabara ya kufika kituoni hapo, Chongolo ameagiza Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) kuanza ujenzi wa barabara hiyo ndani ya saa 24.

Kuhusu uhaba wa wataalamu wa afya kituoni hapo hususan daktari Chongoro amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego kumleta daktari katika kituo hicho.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego amesema kesho Jumapili Mei 28, 2023 daktari atakuwa ameshawasili katika Kituo hicho.

Akizungumza Baada ya kufanya ukaguzi kwenye kituo hicho, Chongolo amesema Rais Samia suluhu Hassan ametoa kibali cha kuajiri watumishi wa afya pamoja na walimu nchi nzima hivyo baadhi yao wataletwa kwenye maeneo yenye uhaba ndani ya mji huo.

"Kwa hiyo hadi Julai watumishi wa afya watakuja, tumekuja kutatua changamoto za wananchi sio kupiga porojo," amesema Chongolo na kuongeza;

"Pia Tarura kesho waanze mchakato wa kuchonga barabara inayokuja kwenye kituo hiki,”.

Awali, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga, Chitopela Maganga alisema zipo changamoto zinakikabili kituo hicho cha afya ikiwamo uhaba wa watumishi 33 kati ya 39 wataotakiwa, pia hakina daktari.