Ujenzi barabara ya mwendokasi Mbagala-Vikindu mbioni kuanza

Rais Samia Suluhu Hassan akiwasikiliza wananchi mkoani Pwani ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake mikoa ya Kusini.
Ikwiriri. Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza upembuzi yakinifu wa ujenzi wa Barabara ya Mabasi yaendayo haraka kutoka Mbagala - Vikindu ufanyike haraka ili utaratibu wa kuanza ujenzi uanze mara moja.
Hayo yamesemwa na Waziri Innocent Bashungwa leo Septemba 20, 2023 mbele ya wananchi wa Ikwiriri mkoani Pwani ikiwa ni mwendelezo wa ziara ya Rais Samia kwa mikoa ya Kusini.
"Rais BRT kutoka Mbagala Rangi Tatu hadi Vikindu umetuelekeza usanifu ufanyike haraka ili barabara hiyo na njia nne ije mpaka Vikindu ili wananchi wa mkoa wa hapa Pwani na Rufiji waweze kuingia Dar es Salaam kwa wepesi na kutoka kwa wepesi," amesema Bashungwa.
Waziri Bashungwa amesema ujenzi wa miundombinu ya barabara nchini unafanyika kwa umakini na viwango vya ubora chini ya Rais Samia.
"Sisi kazi yetu ni kutekeleza yale ambayo Rais ametuagiza, kwenye maelekezo uliyotupatia ya utiaji saini mikataba mbalimbali ambayo inakaribia Sh2 trilioni hata Tarura watakuwepo kuonesha namna Serikali yako ilivyojipanga katika ujenzi wa barabara," amesema Bashungwa.
Naye Mbunge wa Rufiji ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Mohammed Mchengerwa amesema Rais Samia ameridhia kutoa kiasi cha Sh75 bilioni kuanza ujenzi wa Barabara ya Nyamwage - Utete yenye urefu wa kilometa 37 na tayari wakandarasi wanaendelea na ujenzi wa barabara hiyo.
"Naomba nitumie nafasi hii kukushukuru Rais kwa kuridhia kujenga barabara ya Ikwiriri- Mkongo kwa kiwango cha lami na tayari mkandarasi yupo site amekwishaanza kujenga daraja la mbambe na barabara itakayotoka mbambe kuja hapa Ikwiriri mjini," ameongeza Mchengerwa,