Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wananchi wataka ofa ya mwendokasi Sabasaba iendelee

Abiria wakitumia usafiri wa basi la mwendokasi, jijini Dar es Salaam. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) ilitoa mabasi yaendayo haraka katika njia ya Mbagala – Gerezani ambayo bado ujenzi unaendelea. Ofa hiyo ilikuwa ni maalumu katika msimu wa maonyesho ya Sabasaba.

Dar es Salaam. Wananchi wanaotumia huduma ya mabasi yaendayo haraka kati ya Mbagala Rangitatu hadi Gerezani wametaka huduma hiyo kuendelea hata baada ya maonyesho ya Sabasaba kukoma ili kusaidia kupunguza adha ya usafiri wanayokutana nayo.

Wametoa kauli hiyo ikiwa imebaki siku moja kabla ya huduma hiyo kufikia tamani Julai 14, 2023 kwa mujibu wa kibali kilichotolewa na Mamlaka ya Usafiri wa Ardhini (Latra).

Huduma hiyo ya mabasi yaendayo haraka ilikuwa maalumu kwa ajili ya kurahisisha usafiri kwa wananchi wanaokwenda kwenye Maonyesho hayo ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF).

Wakizungumza na Mwananchi, wamesema uwepo wa mabasi yaendayo haraka ulisaidia kupunguza muda waliokuwa wakitumia kutoka Mbagala hadi Gerezani.

“Nusu saa (dakika 30) ni nyingi umeshafika mjini, kwa kawaida ilikuwa unatumia hadi saa zima na nusu hasa asubuhi. Huwezi kupita dirishaji au kupigania mlangoni, utasimama sana kituoni,” amesema Rebecca Mlay, mkazi wa Mbagala Charambe.

Kwa upande wake, Dausen Msangi amesema uwepo wa huduma hiyo ulikuwa si msaada tu kwa wafanyabishara bali hadi wanafunzi ambao kwa kawaida husubiri kituoni kwa muda mrefu kutokana na makondakta kukataa kuwabeba wengi.

“Kuna wakati konda anasema anataka wanafunzi wawili au watano pekee, sasa wakiwa wengi wanakaa sana kituoni, ila mwendokasi ilikuwa haichagui nani wa kuondoka naye, ilikuwa ahueni, kama ingewezekana huduma iendelee,” amesema Msangi.

Licha ya kuwa miundombinu haijakamili, Rosemary Wangabo amesema kuwe na namna ambayo ujenzi unaweza kuendelea huku huduma nayo ikiendelea kutolewa ili watu waendelee kufurahia usafiri huo.

“Hii ni kama kuonja chakula halafu hauli ukashiba, kama tuliweza kutumia sasa hivi, nafikiri tunaweza kuendelea kutumia maeneo ambayo tayari yamekamilika na yale ambayo hayajakamilika yaendelee na ujenzi,” amesema Wangabo na kuongeza

"Hii haitatisaidia sisi pekee itachochea pia ukuaji wa uchumi wetu kwani tunatumia muda mwingi barabarani ambao tungeweza kuutumia kufanya uzalishaji mali.

Akizungumzia suala hilo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma – Dart, William Gatambi alisema huduma ile ilikuwa maalumu kwa ajili ya maonyesho ya Sabasaba kuanzia Juni 27 mpaka Julai 14 na haiwezi kuendelea kwa sababu ujenzi wa miundombinu bado unaendelea.

“Tunatambua mahitaji ya huduma za mwendokasi ni makubwa lakini lazima ukamilishe miundombinu ili tuweze kutoa huduma bora zaidi, hivyo wananchi wa maeneo hayo waendelee kuwa watulivu,” amesema.

Amesisitiza kwamba kibali kilikuwa cha wiki mbili ambacho hakiwezi kuathiri ujenzi lakini ukiongeza muda maana yake itavuruga utaratibu wa ujenzi kwa mujibu wa mkataba.