Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uganda yaanzisha kilimo cha bangi

Wafanyakazi wa kiwanda cha Hemp wilayani Kasese wakiandaa miche ya bangi kwa ajili ya kupelekwa shambani. Picha kwa hisani ya Gazeti la Daily Monitor la Uganda

Muktasari:

Uganda imehalalisha kilimo cha bangi kwa ajili ya matumizi ya kutengeneza dawa za binadamu.

Kampala. Zaidi ya kampuni 24 nchini Uganda zimeomba leseni kwa ajili ya kuingiza mbegu za bangi na udongo wenye rutuba kwa ajili ya kilimo cha zao hilo.

Waziri wa Afya, Jane Ruth Aceng amepokea maombi ya kampuni 24 yanayotaka kuanzisha kilimo cha bangi nchini humo.

Hata hivyo, alisema wanasubiri mwongozo wa baraza la mawaziri kuhusu idadi inayotakiwa kufanya uwekezaji huo.

Mwaka jana kampuni ambazo tayari zina kibali ziliingiza nchini humo jumla ya tani 150 za udongo na mbegu za bangi kilo 2,000.

Udongo uliokuwa kwenye makontena matano na mbegu hizo ziliingizwa nchini humo zikitokea kwenye benki za kuhifadhi mbegu hizo zilizoko nchi za Uholanzi, Sri Lanka na kisiwa kilichopo Asia kusini.

Gazeti la Daily Monitor lilifanikiwa kuona nyaraka za uingizaji wa mbegu za bangi zikiwa na muhuri wa Mamlaka ya Mapato ya Uganda (URA) uliokuwa na tarehe ya Agosti 30, 2018.

Uganda imehalalisha kilimo cha bangi kwa ajili ya matumizi ya kutengeneza dawa za binadamu.

Mmoja wa wakurugenzi wa kiwanda cha Hemp (U) Ltd iliyoruhusiwa kuingiza udongo na mbegu za bangi, Benjamin Cadet alisema, “Hii ni kwa madhumuni ya dawa, hatuwezi kuingia kwenye hatari, unahitaji kudhibiti kila kitu. Kilimo hiki kinatokana na itifaki ya Shirika la Afya Duniani inayotaka uandaaji wa mipango ya kuwa na malighafi zinazotumika kutengeneza dawa.”

Kiwanda hicho kilichoanzishwa mwaka 2012 hivi sasa kinalima na kutengeneza dawa zinazotokana na mmea wa bangi.

Kampuni hiyo ilipata leseni inayosimamiwa kwa ukaribu na wizara ya afya na mambo ya ndani ikishirikiana na Mamlaka ya Dawa ya Taifa.

Kiwanda cha Hemp Uganda Ltd chenye makao makuu yake Hima iliyopo Wilaya ya Kasese kikishirikiana na kiwanda cha dawa cha Globus Pharma Uganda Ltd ni waagizaji wa mbegu za bangi na udongo kutoka Israeli.

Pia, kiwanda cha Hemp kimeagiza udongo wenye rutuba ya kilimo cha bangi kutoka Sri Lanka kwa gharama ya dola 300,000 (sawa na Sh1.12 bilioni za Uganda). Udongo huo wenye rutuba ya kutosha unasaidia miche ya bangi kukua vizuri na yenye ubora.

Dawa zinazotokana na bangi zinatarajiwa kuuzwa katika nchi za Canada na Ujerumani kwa thamani ya Sh600 bilioni kwa mwaka.

Waziri wa Kilimo, Vincent Ssempijja alisema kwa siku zijazo wanatarajia kuagiza mbegu za bangi kutoka Ujerumani kwa kuwa nao ni wauzaji wakubwa kwenye soko la kimataifa.