Ufaulu hisabati wapanda, bado lashika mkia

Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Said Mohammed.
Muktasari:
- Necta yatangaza matokeo ya kidato cha nne, ufaulu ukiongezeka kwa asilimia 0.87, huku kiwango cha ufaulu wa hisabati kikipanda kuliko masomo yote japo somo hilo likiwa bado la mwisho katika ufaulu wa jumla.
Dar es Salaam. Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limetangaza matokeo ya mtihani wa Taifa wa kidato cha nne uliofanyika Novemba 2023, yakionyesha kuongezeka kwa ufaulu wa watahiniwa kwa asilimia 0.87 na ufaulu wa hisabati ukipanda kuliko masomo yote.
Mbali na kuongeza kwa kiwango cha ufaulu, ubora wa ufaulu kwa daraja la kwanza hadi la tatu nacho kimeongezeka kwa asilimia 0.47 ikilinganishwa na ilivyokuwa mwaka 2022.
Akitangaza matokeo hayo leo jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Necta Dk Said Mohamed amesema asilimia 37.42 ya watahiniwa wamepata daraja la kwanza hadi la tatu ikilinganishwa na asilimia 36.95 waliopata madaraja hayo mwaka 2022.
“Jumla ya watahiniwa wa shule 471,427 kati ya 527,576 wenye matokeo ambao ni sawa na asilimia 89.36 wamefaulu kwa kupata daraja la kwanza hadi la nne. Waliopata daraja la kwanza hadi la tatu ni asilimia 37.42,” amesema Dk Mohamed.
Ufaulu kimasomo
Kwenye upande wa masomo, licha ya hisabati kuendelea kuwa chini ya wastani, kiwango cha ufaulu kwa somo hilo kimepanda kuliko masomo yote ambapo takwimu zinaonesha ufaulu umeongezeka kwa asilimia 5.34. Mwaka 2022 ufaulu wa somo hilo ulikuwa asilimia 20.08.
Somo la Kiswahili ufaulu wake umeendelea kupanda ambapo asilimia 96.80 ya watahiniwa waliofanya mtihani huo wamefaulu.
“Wanafunzi waliopata daraja A hadi C kwenye Kiswahili ni asilimia 74.39, ufaulu wa watahiniwa waliopata A na B umeongezeka kwa asilimia 1.54,” amesema Dk Mohamed. Mwaka 2022 ufaulu wa jumla wa somo hilo ulikuwa 95.58.
Ufaulu kwa masomo mengine kulinganisha na mwaka 2022 ni kama ifuatavyo: uraia 70.04 kutoka 2022 67.83, historia 62.01 kutoka asilimia 63.20, jiografia 66.10 kutoka asilimia 64.32, Kiingereza 68.72 kutoka asilimia 69.09.
Masomo mengine ni fizikia kutoka 71.85 kutoka asilimia 68.34, kemia 96.14 kutoka asilimia 93.68 na biolojia 70.09 kutoka asilimia 67.84
Watahiniwa wa kujitegemea
Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea ufaulu wao umepungua kwa asilimia 15.90 ikilinganishwa na mwaka 2022.
Matokeo hayo yameonesha watahiniwa wa kujitegemea waliofaulu ni 13,396 sawa na asilimia 52.44 wakati mwaka 2022 watahiniwa wa kujitegemea waliofaulu walikuwa 19,475 sawa na asilimia 68.34.