Mdondoko wa wanafunzi shule za msingi tishio, wadau washauri

Muktasari:
- Wazazi watakiwa kutoa kipaumbele katika elimu na kuongeza ufuatiliaji wa masomo kwa watoto wao
Dar es Salaam. Jitihada zaidi zinahitajika ikiwemo kuelimisha wazazi juu ya umuhimu wa elimu jambo litakalosaidia kudhibiti mdondoko wa wanafunzi shule ya msingi, na hivyo kuhakikisha wanaoanza shule, wanamaliza kama ilivyokusudiwa.
Hiyo ni kutokana na kile kilichobainika kuwa, wanafunzi waliokuwa darasa la saba, sita na tano mwaka 2023 ni pungufu ya kati asilimia 21 na 25.
Idadi hiyo ni wastani wa wanafunzi 308,945 kwa kila darasa ikilinganishwa na idadi yao walipokuwa madarasa ya chini mwaka 2020.
Takwimu hizo ni kwa mujibu wa ripoti za Best za mwaka 2023 na 2020 zilizotolewa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa (Tamisemi).
Ripoti hizo zinaonyesha kuwa, wanafunzi milioni 1,408,227 waliokuwa darasa la saba mwaka jana hadi ripoti hiyo ilipotolewa ni pungufu ya wanafunzi 415,096 ikilinganishwa na walipokuwa darasa la nne mwaka 2020.
Wakati wapo darasa la nne mwaka huo, wanafunzi hao waliokuwa milioni 1,706,134.
Wanafunzi waliokuwa darasa la sita mwaka jana pia walikuwa pungufu kwa 459,382 ikilinganishwa na wanafunzi milioni 1,847,933 walipokuwa darasa la tatu mwaka 2020.
Kwa wanafunzi wa darasa la tano mwaka 2023, ilikuwa pungufu ya wanafunzi 361,303 ikilinganishwa na idadi yao ya milioni 1,738,108 walipokuwa darasa la pili mwaka 2020.
Wadau wanasema huenda wanafunzi hao wamerudia darasa, kuacha shule kwa sababu mbalimbali hivyo kuchauri wadau hasa wazazi na walezi kuwa makini na makundi hayo.
Akizungumzia suala hilo, Mtafiti wa Elimu, Muhanyi Nkoronko amesema wakati wanafunzi wa vijijini wakiongoza zaidi kuacha shule kuliko wa mjini amesema ni vyema wazazi wa maeneo hayo wakalimishwa juu ya umuhimu wa watoto kwenda shule.
Hiyo ni kutokana na kile alichokieleza kuwa, kutoonekana kwa matokeo ya tofauti kati ya watoto waliosoma na ambao hawajasoma inawafanya wazazi wengi kuona shuleni kama sehemu ya kukua tu.
“Akisoma darasa la awali hadi la tatu akiwa mkubwa anaacha shule anapotea, juhudi za haraka zinahitajika hasa katika kuwaelimisha wazazi wakajua thamani ya elimu zinahitajika, hili litawezekana kwa ushirikiano wa Serikali na wadau,” amesema Nkoronko.
Amesema hilo lunaweza kuwa na matokeo zaidi ikiwa wazazi wataonyesha baadhi ya watoto waliosoma na matokeo waliyoyapata ikilinganishwa na ambao hawajasoma.
“Yakipatikana majibu kuwa mtu akimaliza shule anaenda wapi itaongeza ari ya wazazi kupeleka watoto wao shule pia thamani ya elimu ikiongezeka utaongeza chachu ya wazazi kupeleka watoto shule.
Lakini ili kuvutia wanafunzi kubaki shuleni ni vyema pia kutatua changamoto zinazopatikana katika upatikanaji wa elimu ikiwemo kuongeza madarasa, walimu, vifaa vya ufundishaji na kujifunza ambavyo vinaweza kufanya mwanafunzi apate ari ya kujifunza.
“Pia iongeze bajeti ya elimu, kuongeza vitendea kazi ili mwanafunzi anapoingia shuleni apate maarifa sahihi anapokuwa shuleni,” amesema.
Kuhusu walimu, tangu mwaka 2021, serikali ilianza kuajiri ili kukabiliana na ongezeko la wanafunzi na mwaka huo, walimu 6,949 waliajiriwa ambapo kati yao 3,949 walikuwa wa shule za msingi.
Baadaye Juni mwaka uliofuatia walimu 9,800 waliajiriwa ambapo kati yao 5,000 walikuwa wa shule za msingi. Mwaka 2023 pia ajira 13,130 zilitangazwa kwa ajili ya walimu wa msingi na sekondari.
Hilo limeendelea tena ambapo Januari 6 mwaka huu, Waziri wa Tamisemi, Mohammed Mchengerwa ametangaza ajira mpya za walimu na maofisa afya 23,000 katika kipindi cha Januari na Februari.
Mbali na ajira hizo kuwa hatua za kwenda kukabiliana na ongezeko la wanafunzi pia ni maandalizi ya miradi mbalimbali ambayo imekuwa ikifanywa na Serikali ikiwemo ya kuongeza shule na madarasa kupitia mradi wa kuimarisha na kuboresha elimu ya awali na msingi hapa nchini BOOST.
“Serikali imepanga kutumia Sh1.15 trilioni kupitia mradi wa Boost ni kwa ajili ya uboreshwaji wa miundombinu ya elimu ya awali na msingi, ikimepagwa kutumika katika kipindi cha miaka mitano na tunakusudia kujenga madarasa 12,000 na vyoo 6000 ifikapo mwaka 2025 kupitia mradi huo alioubuni Rais Samia Suluhu Hassan,” alisema Mchengerwa
Akitoa mbinu nyingine ya kukabiliana na mdondoko wanafunzi, Mdau mwingine wa elimu, Catherine Sekwao amesema ni vyema ukafanyika utafiti ili kujua sababu za wanafunzi hao kuacha shule ili kiini ndiyo kishughulikiwe.
“Watafiti wa elimu wanaweza kusaidia katika hili, hii inaweza kutupa suluhisho la kudumu, usipozijua sababu ni ngumu kushughulika nazo.
Yeye pia aligusia suala la uhaba wa walimu kuwa chanzo cha wanafunzi kuacha shule kwa kile alichoeleza kuwa maeneo mengi ya vijijini shule moja huweza kuwa na walimu watatu.
“Walimu hao pia hawakai shuleni wanatumia zaidi ya Km20 kufika shule, afike saa ngapi shuleni, anafika amechoka, hii inafanya hata umakini kwa mwalimu kupungua, anakuwa akifundisha wanaoelewa anaenda nao wasioelewa wanabaki,” amesema Sekwao.
Ikiwa mtu anavuka darasa na hajui kusoma anaona hakuna umuhimu way eye kuendelea na shule jambo ambalo hufanya hata wazazi wasiokuwa na mwamko wa elimu kuamua kuwazuia watoto kwenda shule ili wawasaidie kazi za nyumbani.
Kuhusu utafiti ili kujua sababu za mdondoko wanafunzi, Novemba 30 mwaka jana akizungumza katika ufunguzi maadhimisho ya Miaka 50 ya Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Profesa Adolf Mkenda ambaye ni Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia alisema Serikali itakwenda kufanya tafiti ili kujua sababu za mdondoko wa wanafunzi.
Amesema kufanya hivyo kunalenga kutafuta suluhisho la kudumu ili kuhakikisha kila mtoto ananufaika na fursa za elimu zinazotolewa.
Alitoa kauli hiyo wakati takwimu zikionyesha kuwa asilimia 26.8 ya wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza mwaka 2017 walishindwa kufikia mtihani wa darasa la saba mwaka 2023.
“Tumeangalia takwimu ya waliojisajili darasa la kwanza halafu wakafanya mtihani darasa la saba mwaka huu, tumepoteza wanafunzi katikati, ile idadi hairidhishi, tumeanza kuwatafuta na kuangalia nini kimetokea na kufanya tafiti, mikoa gani yenye tatizo na kwanini,” amesema Mkenda.
Amesema Serikali haiwezi kuvumilia kuona walioandikishwa wanashindwa kumaliza elimu yao ya msingi na wanalo jukumu kama Wizara ya kumueleza Rais Samia Suluhu Hassan nini wanafanya kukabiliana na suala hilo.
Mwisho.