Tehama kutumika kupunguza mdondoko shuleni

Muktasari:
- Kwa mfano, takwimu hizo zinaonyesha kuwa mwaka 2015 wanafunzi 61,488 waliripotiwa kuacha shule.
Takwimu za wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), zinaonyesha kuwa bado kuna changamoto tete ya wanafunzi wengi wa shule za msingi kuacha masomo.
Kwa mfano, takwimu hizo zinaonyesha kuwa mwaka 2015 wanafunzi 61,488 waliripotiwa kuacha shule.
Kuna sababu nyingi ambazo huwafanya wanafunzi kuacha shule, ikiwamo mazingira magumu ya kujifunzia katika baadhi ya shule.
Aidha, kutokuwapo kwa uwiano usio rafiki wa wanafunzi na madarasa katika baadhi ya shule, kumesababisha msongamano mkubwa wa wanafunzi, hali inayochangia ugumu katika kufundisha na kujifunza.
Wakati miongozo ya kielimu ikitaka uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi wasiozidi 45, uzoefu unaonyesha katika shule nyingi uwiano upande wa wanafunzi ni maradufu.
Kwa mfano, katika shule za msingi ya Chemchem na Charambe wilayani Temeke jijini Dar es Salaam, kila darasa lina wanafunzi zaidi ya 100.
Kimsingi, msongamano katika madarasa ni miongoni mwa sababu ambazo huwafanya baadhi ya wanafunzi kuacha shule.
Sababu nyingine ni uchache wa matundu ya vyoo usiolingana na idadi ya wanafunzi hasa wa kike. Hii huwafanya wawe katika mazingira magumu na kusababisha baadhi yao kuacha shule.
Taarifa njema
Changamoto hizo na nyingine zimeisukuma kampuni ya EagleAnalytics ya jijini Dar es Salaam kutengeneza mfumo wa kielekroniki unaoitwaDropwall.
Mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo, Rose Funja anasema mfumo huo una lengo la kupunguza idadi ya wanafunzi wanaoacha shule.
Katika mfumo huo, kutakuwa na takwimu za elimu ambazo zinachakatwa na kampuni hiyo na kuweka kwenye mtandao utakao kuwa wazi kwa kila mmoja kuutumia.
Funja ambaye ni mhandisi Tehama, anasema kila shule itakuwa na taarifa kwenye mtandao huo.
Baadhi ya takwimu hizo ni uwiano wa walimu na wanafunzi, uwiano wa wanafunzi na vyoo, uwiano wanafunzi na madarasa.
Takwimu nyingine ni uwiano wa wanafunzi na waangalizi wa afya, uwiano wa maendeleo ya mwanafunzi na marafiki zake.
“Takwimu hizi zinapopatikana kwa urahisi kupitia mtandao zitawawezesha wazazi na halmashauri kuchukua hatua kuboresha upungufu kabla ya wanafunzi hawajaacha shule,”anasema.
Akifafanua, Funja anasema baadhi ya wasichana wamekuwa wakiacha shule kwa sababu ya uchache wa matundu ya vyoo.
“Tunajua wasichana wakiwa kwenye hedhi wakati huduma za vyoo zina upungufu,wengi wanaona mazingira ya shule sio rafiki, hivyo wanaamua kuacha shule,” anasema.
Faida za mfumo wa dropwall
Anasema kwa kuweka takwimu hizo wazi, jamii itaweza kuchukua hatua kukabiliana na upungufu kabla wanafunzi hawajaacha shule.
“Kama kuna upungufu wa matundu ya vyoo katika shule husika, hatua zitachukuliwa ili kujenga na hivyo kuzuia wanafunzi wasiache shule,”anasema.
Aidha, mfumo huo utawasaidia watendaji wanaopanga bajeti kuangalia maeneo yenye matatizo na kuyapa upendeleo.
“Kama shule ina upungufu wa madarasa kuliko shule nyingine itawasaidia wanaopanga bajeti kuipa upendeleo wa fedha ili kukabiliana na tatizo hilo,” anaeleza na kuongeza:
“Changamoto zikiwa wazi ni rahisi kuchukua hatua;mfumo wa Dropwall una lengo la kupunguza mdondoko wa wanafunzi.”
Mradi huo unafadhiliwa na Shirika la Malengo ya Milenia (MCC) na umeanzia katika wilaya za Mbeya Mjini na Nzega.
“Ukifungua kwenye mtandao wetu (www.eagleanalytics.tz/dlli) utakuta taarifa za elimu zilizochakatwa zinazohusu shule zote za miji hiyo,”anasema na kuongeza kuwa matarajio ni kuzifikia wilaya zote ikiwa watapata rasilimali fedha.
“Tumepewa fedha kwa ajili ya wilaya hizo mbili ikiwa ni mradi wa majaribio tunasubiri fedha nyingine ili tuendelee kwenye wilaya nyingine.
Anasema juhudi zinafanyika ili taarifa hizo ziweze kupatikana kwa njia ya simu za mkononi.
“Lengo ni kuwa kila Mtanzania akitaka kupata taarifa azipate kwa haraka na kuchukua hatua,”anasema.
Anasema tofauti na sasa ambapo jitihada hufanyika baada ya mwanafunzi kuacha masomo, mfumo wa Dropwall utawezesha jitihada kufanyika kabla mwanafunzi hajaacha shule.
Tatizo la takwimu
Kwa upande wake, Geofrey Chambua kutoka Taasisi ya Data for Local Impact (DLI) inayoratibu mradi huo kwa kushirikianana Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), anasema kumekuwa na tatizo la upatikanaji wa takwimu nchini.
“Tunataka tuwe na takwimu huria ambazo zitakuwa wazi kwa yeyote,ili zisaidie kutatua changamoto zilizopo katika jamii,” anasema.
Anasema mfumo wa kielekroniki wa dropwall, unalenga kuongeza matumizi ya taarifa zilizokusanywa na wadau mbalimbali ikiwamo Serikali.
Anatoa wito kwa wasomi wengine kubuni mifumo itakayosaidia kuondoa matatizo kwenye jamii.