UDBS kuja na kliniki ya biashara
Muktasari:
- Kliniki hiyo inalenga kutoa ushauri wa bure kwa wafanyabiashara na wale wanaotamani kuanzisha biashara na kuwasaidia kufahamu namna sahihi ya kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Dar es Salaam. Ili kuwasaidia wafanyabiashara wadogo na kati kupata elimu ya fedha na namna sahihi ya uendeshaji wa biashara Shule Kuu ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS) imekuja na kliniki maalum ya biashara.
Kliniki hiyo inalenga kutoa ushauri wa bure kwa wafanyabiashara na wale wanaotamani kuanzisha biashara na kuwasaidia kufahamu namna sahihi ya kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Akizungumza na waandishi wa habari Amidi wa UDBS, Profesa Omari Mbura amesema uanzishwaji wa kliniki hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya ubunifu na utafiti ambayo kwa upande wa UDSM inayotarajiwa kufanyika kuanzia Mei 5-7,2025.
Mbura amesema wazo la kuja na kliniki ya biashara imetokana na changamoto mbalimbali wanazopitia wafanyabishara katika kufanya shughuli zao.
Miongoni mwa changamoto alizozibainisha ni pamoja na upatikanaji wa mitaji, ukosefu wa elimu ya fedha na namna sahihi ya uendeshaji wa biashara.
Sababu hizo amezitaja kuwa miongoni mwa vikwazo vinavyowafanya baadhi ya wafanyabishara kushindwa kunufaika na shughuli wanazozifanya,
“Kupitia kliniki hii, wataalamu wa Shule Kuu ya biashara watatoa ushauri katika maeneo mbalimbali ikiwemo masuala ya kodi, mitaji, usimamizi na utunzaji wa fedha, masoko, utunzaji wa taarifa za biashara, na kukuza biashara” amesema.
Ameongeza kuwa katika maadhimisho hayo pia kutakuwa na mafunzo maalum ya utafiti kwa wanafunzi wa shahada ya uzamivu na uzamili, na watafiti wanaochipukia.
“Mafunzo haya yanalenga kuongeza ubora wa tafiti na machapisho ili kusaidia kuongeza idadi ya machapisho kwenye majarida shindani ya ndani na kimataifa”amesema.