Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ubunifu, teknolojia kubeba dira ya maendeleo 2050

Baadhi ya washiriki wa mkutano ulioandaliwa na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF),  kwa lengo la kukusanya maoni kutoka kwa wadau wa sekta binafsi  ili kufanikisha uandaaji wa dira ya maendeleo ya Tanzania 2050.

Muktasari:

Wadau wa Sekta binafsi nchini wameishauri Tume ya Taifa ya Mipango kukumbatia ubunifu na teknolojia ili kufanikisha utekelezaji wa dira ya maendeleo ya 2050, ambayo mchakato wa kuiandaa umekwishaanza.

Dar es Salaam. Wadau wa Sekta binafsi nchini wameishauri Tume ya Taifa ya Mipango kukumbatia ubunifu na teknolojia ili kufanikisha utekelezaji wa dira ya maendeleo ya 2050, ambayo mchakato wa kuiandaa umekwishaanza.

Hayo yamesemwa leo katika mkutano ulioandaliwa na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) kwa lengo la kukusanya maoni kutoka kwa wadau wa sekta binafsi  ili kufanikisha uandaaji wa dira ya maendeleo ya Tanzania 2050.

"Lazima tujenge Tanzania ambayo itategemea kwa kiasi kikubwa ubunifu na teknolojia,  tunatazamia Tanzania ambayo biashara za ndani na nje zinawekeza katika utafiti wa hali ya juu na teknolojia, na kutuwezesha kufikia viwango vipya vya ufanisi na ushindani wa kimataifa," amesema Mkurugenzi Mkuu wa TPSF, Raphael Maganga wakati wa mkutano huo leo jijini hapa.

Maganga amesema matarajio ya sekta binafsi ni kukuza uchumi thabiti wa kidijitali ili kuwawezesha wafanyabiashara na wavumbuzi kuongoza barani Afrika na kwingineko.

"Tunapotafakari dira ya 2025, lazima tuelewe dira hii ilituongoza kutoka uchumi wa kijamaa ambapo Serikali ndio ilikuwa mfanyabishara mkubwa na kuweka misingi imara na kukua kwa sekta binafsi nchini. Misingi hii ndio ilituwezesha kama Taifa kupiga hatua mpaka kuwa miongoni mwa nchini zenye

kipato cha kati 2023.

"Dunia ya sasa sio sawa na miaka 25 iliyopita, njozi tulizokuwa nazo kama Taifa miaka 25 iliyopita, haziwezi kutuvusha miaka 25 ijayo, lazima tufanye mageuzi makubwa sana. Pale tulipokuwa tunatambaa, ni lazima tutembee, pale tulipokuwa tunatembea lazima tukimbie na pale tulipokuwa tunakimbia lazima tupae ili kuhakikisha dira 2050 tunaitimiza," amesema.

Pia sekta hiyo imeshauri ukuaji wa maendeleo endelevu na jumuishi, ikisema ukuaji wa maendeleo katika uchumi usipimwe kw viwango vya kifedha tu bali ujumuishe uboreshaji wa ubora wa maisha ya kila Mtanzania.

"Dira hii iwezeshe kutengeneza mazingira ambayo ukuaji wake unanufaisha wananchi wote, kwa kuwa na usawa wa elimu bora, huduma za afya na fursa bila kujali asili ya mtu," ameongeza Maganga.

Amesema kuwa dira ya 2050 idhamirie kuimarisha utawala bora na utawala wa sheria ili kuweka mazingira ya uwazi, uwajibikaji na rafiki kwa uwekezaji,  yakisimamiwa na mfumo thabiti wa kisheria unaowezesha sekta binafsi kustawi na kuchangia kwa kiasi kikubwa utajiri na ustawi wa Taifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mipango ya Kitaifa wa Tume ya Mipango, Mulsali Milanzi ambaye alikuwa akimwakilisha Katibu Mtendaji wa tume hiyo, Lawrence Mafuru, amesema mkutano huo ni hatua ya mchakato wa kuandaa dira ya 2050 na tume hiyo imeanza kuwashawishi wananchi na wadau wengine kushiriki kwa namna mbalimbali.

"Sisi kama tume tumeamua kushirikiana na sekta binafsi katika kikao chao cha leo ili kujadiliana kuona ni namna gani dira ya 2050 itaandaliwa vizuri kwa manufaa ya nchi yetu," amesema Milanzi.

Amesema wanatambua mchango ilionao sekta binafsi ikiwa ni pamoja na kuajiri idadi kubwa ya Watanzania, lakini pia matumizi makubwa ya teknolojia katika uzalishaji na utoaji wa huduma zake.

"Ni muhimu sana wao kushiriki ili kutupatia maoni yatakayotusaidia kutekeleza dira ya utekelezaji wa miaka 25 ijayo baada ya hii tuliyonayo kumalizika 2025.

"Tumetekeleza dira ya 2025 kwa kiwango kikubwa na tumefanya vizuri katika maeneo mbalimbali na ndiyo maana sasa hivi tumevuka kutoka hadhi ya uchumi wa chini hadi kufika uchumi wa kati wa chini," ameongeza.

Amesema hiyo ni ishara ya kuongezeka kwa pato la mtu mmoja mmoja na ishara ya kupungua kwa umaskini.

"Tumeona kwamba Tanzania imekuwa ikikuza uchumi wake kwa asilimia 6 kwa mwaka, si jambo dogo lakini tungependa kuona katika miaka 25 ijayo tunafika katika kiwango cha juu zaidi cha ukuaji wa uchumi," amesema Milanzi.


Changamoto

Milanzi amezitaja baadhi ya changamoto ambazo Serikali imekumbana nazo katika kipindi cha utekelezaji wa dira ya maendeleo ya 2025 ikiwemo ujuzi mdogo ambapo amesema wangetamani kuongeza wajuzi zaidi ili kufanikisha utelekezaji wa dira ya 2050.

"Changamoto nyingine ni zile za nje kwa mfano janga la Uviko-19 ambalo lilitikisa nchi nyingi kiuchumi. Tumeona mgogoro wa Russia na Ukraine ulivyoathiri mnyororo wa usambazaji wa bidhaa na huduma. Kwa hiyo tunataka tuijenge nchi yetu kwa namna ambayo itaweza kuhimili changamoto kama hizi," amesema.