Dira ya Taifa 2050 itakavyochochea uchumi

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo.
Muktasari:
- Baadhi ya malengo ya Dira ya mpya ya Taifa ya mwaka 2050 ni pamoja kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi jumuishi unaopunguza umasikini, unaozalisha ajira na kuchochea mauzo ya nje ya bidhaa.
Dar es Salaam. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo ameeleza malengo ya Dira mpya ya Taifa ya mwaka 2050, kuwa ni kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi jumuishi unaopunguza umasikini, unaozalisha ajira na kuchochea mauzo ya nje ya bidhaa.
Mengine ni kuongeza tija katika uzalishaji na uongezaji thamani katika mifugo, madini, misitu na kilimo.
Profesa Kitila ameyasema hayo leo Desemba 9, katika maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru wa Tanganyika na Mkutano wa Kwanza wa Kitaifa wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 leo tarehe 09 Desemba, 2023.
“Hii inaenda sambamba na kuweka msukumo wa uongezaji tija katika uzalishaji na uongezaji thamani sekta ya kilimo ufugaji uvuvi, misitu na madini,” amesema Profesa Kitila.
Amesema lengo lingine ni kuchochea na kuboresha ubora wa elimu na mafunzo katika ngazi zote, kuongeza na kuimarisha matumizi ya teknolojia zaidi ya hasa ya teknolojia ya habari na Mawasiliano (Tehama) hasa katika zama za mapinduzuzi ya nne ya viwanda.
“Pia kuongeza uzalishaji viwandani na kuimarisha huduma bora za jamii kwa wote,” amesema.
Kuhusu uratibu, amesema kutakuwa na timu itakayoratibu maandalizi ya dira itakayokuwa katika makundi matatu, ambapo itahusisha sekretarieti chini ya menejimenti ya Tume ya Mipango, timu kuu ya wataalamu ambayo nayo itaratibu ukusanyaji wa maoni, kuandika na kufanya uchambuzi.
Pia kutakuwa na Kamati ya kitaifa ya usimamizi ya uandishi wa dira ikiwa chini ya usimamizi wa Mwenyekiti Kassim Majaliwa ambaye ni Waziri Mkuu na Mwenyekiti mwenza Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman.
Wajumbe
Wajumbe 21 wa timu kuu ya kitaalamu watakaofanya kazi chini ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Lawrence Mafuru ni pamoja na Mkurugenzi wa Taasisi ya Twaweza, Aidan Eyakuze, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuendeleza Kilimo Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini (SAGCOT), Godrey Kirenga na Balozi Msatafu wa Tanzania nchini uingereza Asha-Rose Migiro.
Wengine ni Profesa Lusias Msambichaka kutoka Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Profesa Joseph Semboja (UDSM), Dk Florence Turuka (Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Dk Amina Msengwa (Chuo cha Takwimu), Dk Yahya Hamad Shehe (Chuo Kikuu Zanzibar), Dk Mariam Vuai (Taasisi ya utafiti wa sera Zanzibar), Abdula Anaudhuru.
Wengine ni Emmy Hudson ambaye ni mwanasheria mwandamizi ofisi ya Mwanasheria wa Serikali, Dk Ntuli Kapologwe (Mkurugenzi huduma za kinga Wizara ya Afya, Ally Samaje, Dk Richard Kimwaga (mhandisi msaidizi wa maji), Dk Richard Shukiya (mhadhiri mwandamizi wa elimu ya awali), Dk Gladness Salema (UDSM), Iman Nkui (Kamishana wa uhifadhi), Amne Kagasheki, Zahoro Muhaji (Mkurugenzi wa Tanzania startups Association), Dk Neema Mduma (Taasisi ya Teknlojia Nelson Mandela) na Dorice Mgeta.
“Lengo letu ni kujenga mwafaka wa kitaifa kuhusu malengo na kule tunakotaka kwenda miaka ijayo kwa pamoja. Kwa mfano, kama tunataka kwenda Mwanza tutofautiane njia tunazotaka kutumia kufika huko lakini wote tufike huko,” amesema Profesa Kitila.
Kuhusu hoja ya kuongezwa kwa muda wa utekelezaji wa dira ya maendeleo baada ya kuwapo kwa maoni kuwa miaka 25 ni michache na vyema iongezwe, Profesa Kitila amesema wataalamu watakapokuwa wakikusanya maoni watahoji pia suala hilo na kama utaonekana ulazima wa kufanya hivyo basi utaongezwa.
Mafanikio ya Dira 2025
Profesa Kitila amesema moja ya malengo yaliyokuwapo wakati wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2000 inayokaribia kufikia ukingoni, ilikuwa ni kuongeza idadi ya wanafunzi wanaoingia sekondari kutoka shule ya msingi.
“Wakati dira ya sasa inaanza kutekelezwa ni asilimia 20 ya wanafunzi waliomaliza darasa la saba ndiyo walienda kidato cha kwanza na kwa sasa ni asilimia 70 na malengo yetu hadi mwaka 2025 tuwe asilimia 90,” amesema Profesa Kitila.
Amesema anaamini hilo litafanikiwa hasa baada ya Serikali kuondoa ada ya kidato cha nne na kidato cha tano.
Upatikanaji wa maji vijijini ulikuwa kwa asilimia 32 na malengo yalikuwa kufikia asilimia 85 mwaka 2025 lakini hadi mwaka jana walikuwa asilimia 77.
Upatikanaji wa umeme mwaka 2000, asilimia 10 ya Watanzania ndiyo walikuwa wakipata umeme mjini na vijijini na malengo yalikuwa asilimia 90 mwaka 2025 lakini hadi mwaka jana wamefikia asilimia 78.
Mwa upande wa miundombinu, mwaka 2000, mtandao wa barabara za mikoani chini ya Wakala wa Barabara (Tanroads) za lami na zege zilikuwa km4179 na malengo yalikuwa hadi mwaka 2025 tuwe na km13,000 lakini mwaka jana tulikuwa tayari km11,969,” amesema Profesa Kitila.
Kwa upande wa miundombinu ya kidigitali, kaya asilimia 30 ndiyo zilikuwa zinamiliki simu za mkononi huku malengo yakiwa ni kaya zote kumiliki simu za mkononi ifikapo mwaka 2025 na hadi mwaka jana, takwimu zinaonyesha kuwa tumefanikiwa kwa asilimia 86.
“Inteneti hakukuwa na takwimu kabisa kwa kipindi hicho lakini mwaka 2010 Watanzania milioni 13.2 walikuwa na mtandao wa intaneti na sasa wamefikia milioni 34.5, watumiaji wa mitandao ya kijamii 16.7 milioni wanatumia mitandao hiyo,” amesema Profesa Kitila.
Awali, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Lawarence Mafuru alisema katika uandaaji wa dira hiyo, kutakuwa na makongamano na mijadala ili kupanua wigo wa watu wengi kushiriki katika maandalizi ya dira hiyo.