Ubakaji washika kasi ukatili kijinsia

Wanafunzi wa kike wakiwa na mabango yenye ujumbe unaotaka kukomesha unyanyasaji wa kijinsia. Picha kwa Hisani ya Umoja wa Mataifa

Muktasari:

  • Ukatili wa kijinsia, mila na desturi kandamizi vyaongoza kupigiwa kelele Tanzania ikiungana na mataifa mengine kuadhimisha siku ya mtoto wa kike.

Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikiungana na mataifa mengine kuadhimisha siku ya mtoto wa kike duniani, kundi hilo limeendelea kukabiliwa na changamoto ya ukatili wa kingono, hali inayotishia ustawi wa maisha yao.

Kwa mujibu wa Taarifa ya Makosa ya Ukatili wa Kijinsia na Unyanyasaji ya Jeshi la Polisi kwa kipindi cha Januari hadi Desemba, 2022 kulikuwa na matukio 12,163 kati ya hayo 9,962 yaliwahusu wasichana.

Matukio yaliyoongoza ni ubakaji 6,335 yaliyowahusisha wasichana na ulawiti 1,557 hali inayoonesha kundi hilo ndio waathirika wakubwa wa vitendo vya ukatili.

Akizungumza leo Oktoba 11, 2023 wakati wa jukwaa la ajenda ya msichana lililoandaliwa na mashirika yanayotetea haki za wasichana, Mkurugenzi wa Msichana Initiative, Rebeca Gyumi amesema hatua zaidi zinapaswa kuchukuliwa

Amesema hadi sasa tamaduni na mazoea yaliyopo kwenye jamii vinachangia wasichana washindwe kujiamini na kukosa stadi za kujitambua, hivyo wengi wao hujikuta wakipoteza mwelekeo.

“Wasichana wana changamoto nyingi ikiwemo ukatili, kukosa mahitaji muhimu kutoka kwa wazazi hali inayosababisha waangukie kwenye vishawishi ndiyo hapo tunasikia mimba na ndoa za utotoni.

“Katika hili tunaomba Serikali iwekeze kwenye stadi za maisha na kujitambua kwa wasichana. Mtoto wa kike tangu anapozaliwa, anatakiwa alelewe katika misingi itakayomuweka salama na kumfanya ajitambue na atambue ndoto zake,” amesema Rebecca.

Mwanafunzi wa kidato cha tatu kutoka Shule ya Sekondari Jangwani, Emma Pius amesema maadhimisho hayo yanapaswa kwenda sambamba na Serikali kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha mtoto wa kike analindwa na anakuwa salama wakati wote.

“Hadi leo bado kuna wanafunzi wanalazimika kujenga urafiki na makondakta na madereva boda boda ili waweze kuwa na uhakika wa usafiri. Hii ni changamoto kubwa kwa wanafunzi hasa wasichana kwa sababu ni rahisi kuingia kwenye vishawishi.

“Pia tunahitaji mara kwa mara kupata mafunzo ambayo yatatuweka vyema kisaikolojia, kuna mengi tunapitia katika maisha yetu ya kila siku ambayo kwa hakika yanatupa msongo na wapo wenzetu tunaowashuhidia wakikatisha ndoto zao,” amesema Emma.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima ametumia jukwaa hilo kuitaka jamii kutovumilia mwenendo wa vitendo vya ukatili na kushiriki kikamilifu katika kuwafichua wahusika ili hatua za kisheria zichukuliwe.

“Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kumlinda mtoto wa kike ili aweze kukua na kufikia ndoto zake. Pamoja na jitihada hizi bado watoto wa kike wengi wanakabiliwa na vikwazo mbalimbali zinavyorudisha nyuma maendeleo yao.


“Vitendo vya ukatili dhidi ya watoto, mimba na ndoa za utotoni pamoja na ukeketaji kwa baadhi ya jamii ni sehemu ya vikwazo hivyo. Sasa hivi tunaenda ukatili unafanyika hadi kwenye mitandao, watoto wa kike wanakutana na mambo ya ajabu huko,” amesema Dk Gwajima.

Kwa mujibu wa Taarifa ya Utafiti wa Hali ya Ukatili dhidi ya Watoto kwa Njia ya Mtandao ya mwaka 2021 asilimia 67 ya watoto wenye umri wa miaka 12 hadi 17 wanatumia mitandao ya kijamii na asilimia 4 katika yao wamefanyiwa aina moja ama nyingine ya vitendo vya ukatili mtandaoni.

Kwa kutambua hilo Dk Gwajima ameeleza kuwa Serikali kupitia wizara yake Wizara imeunda Kikosi Kazi cha Taifa cha Kisekta kinachohusisha wadau wote wanaohusika na mitandao kinaandaa mkakati wa Taifa wa kumlinda mtoto na kundi la vijana balehe wanapokuwa mtandaoni.