TPDC, Dangote wasaini mkataba upatikanaji wa gesi

Muktasari:
Wataanza kuitumia siku 30 kuanzia leo
Dar es salaam. Shirika la Taifa la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesaini mkataba na Kampuni ya Saruji ya Dangote-Tanzania, utakaosaidia kiwanda hicho kuachana na matumizi ya mafuta ya dizeli katika uzalishaji wa umeme.
Uwakilishi kutoka Kiwanda cha Dangote umesema kiwanda hicho rasmi kitaanza kutumia umeme wa gesi asilia siku 30 zijazo kuanzia leo.
Makubaliano hayo yatasaidia kiwanda hicho kuongeza kiwango cha uzalishaji wa umeme kutoka wastani wa megawatt 20 (18MW -22MW) hadi megawatt 35 za gesi asilia.
Akizungumza na wanahabari leo Agosti 20,2018 jijini Dar es salaam, wakati wa kusaini makubaliano hayo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mhandisi Kapuulya Musomba amesema mkataba huo utadumu kwa miaka 20.
Kwa mujibu wa TPDC, kiwanda hicho ni sehemu ya viwanda saba vilivyopo kwenye mpango wa shirika katika mwaka wa fedha 2018/19, hivyo bado kuna vingine sita vitaunganishwa hapo baadaye.
"Tunajua Serikali iko kwenye hatua za kujenga uchumi wa viwanda, kwa hiyo sisi (TPDC) kwa nafasi yetu tutahakikisha viwanda vinazalisha bidhaa kwa gharama nafuu kupitia matumizi ya gesi, wataanza kutumia futi za ujazo milioni nane na baada ya miaka miwili ijayo wataanza kutumia futi za ujazo milioni 20,” amesema Mhandisi Musomba.
Kiwanda hicho kinaongeza idadi ya viwanda vinavyotumia gesi asilia kwa ajili ya uzalishaji wa umeme kufikia 42 nchini, ambavyo vinatumia futi za ujazo milioni 15 tu kutoka akiba ya futi za ujazo trilioni 57, zinazoweza kutumika miaka 40 ijayo nchini.
TPDC ilianza kuunganisha viwanda katika kipindi cha 2006/07.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa kiwanda hicho cha Saruji, Jagat Rathee amesema kiwanda hicho kilikuwa kinatumia wastani wa lita 106,000 za Dizeli kwa siku katika uzalishaji wa tani 2000 tu.
Hata hivyo, Rathee amesema makubaliano hayo yatasaidia kiwanda hicho kuongeza kiwango cha uzalishaji wa saruji kutoka wastani wa tani 2000 hadi tani 6000 kwa siku kutokana na kushuka kwa gharama za uzalishaji.