Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ticts yaongezewa kodi kwa asilimia 100

Muktasari:

  • 2000- mkataba wa kwanza kati ya Ticts na TPA
  • 2015-Mkataba wa pili kati ya Ticts na TPA

Dar es Salaam. Kampuni ya kimataifa inayoshughulikia upakuaji wa makontena ya mizigo bandarini ya TICTS, imeongezewa kodi kwa asilimia 100 katika mkataba mpya uliosainiwa baina yake na Mamlaka ya Bandari (TPA).

Kodi hiyo imepanda kutoka Sh15.7 Bilioni hadi Sh 31.4 Bilioni.

Mkataba huo umesainiwa leo (Alhamisi, Julai 6) na Mwenyekiti wa bodi ya TPA, Profesa Ignas Rubaratuka (kwa upande wa TPA) na  Mkurugenzi  Mkuu wa TICTS Jared Zerbe.

Utiaji saini wa mkataba huo ulishuhudiwa na Waziri wa  Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi, Wajumbe wa bodi ya TPA, Wajumbe wa Kampuni ya TICTS, Mkurugenzi wa TPA, Mhandisi Deusdedith Kakonko na Kamati iliyofanya majadiliano ya mkataba huo.

Akizungumza baada ya utiaji saini huo, Waziri Mbarawa ameishukuru kamati hiyo kwa kufanya kazi kubwa.

Amesema mkataba huo mpya ni matunda ya agizo la Rais John Magufuli alilolitoa Septemba 26 mwaka jana wakati alipotembelea bandari hiyo kwani baada ya maagizo hayo aliunda kamati ya wataalamu, wengi wao wakiwa vijana ambao wamefanya kazi hiyo.

"Siyo jambo rahisi mpangaji wako ambaye alikuwa analipa kodi ya Sh100,000 leo uzungumze naye aanze kukulipa Sh200,000. Wao walikuwa wakilipa dola milioni saba kila mwaka, lakini sasa watalipa dola milioni 14 milioni na kila baada ya mwaka itakuwa ikiongezeka kwa asilimia tatu," amesema.

Mbali na hivyo, Profesa Mbarawa amesema kupitia mkataba huo kampuni hiyo itatakiwa kulipa ada ya kontena Sh44, 700 (dola 20) kwa kila kontena na ada hiyo itakuwa ikiongezeka kwa asilimia 4.

Pia, Ticts itarejesha bandari kavu ya Ubungo Serikalini na inatakiwa kuhakikisha makontena katika bandari yanaongezeka kwa asilimia 6.5 kila mwaka.

Profesa Kabudi almeusifu mkataba huo mpya kwa kusema ni mkataba uliosaniwa kabla ya sheria mpya za usimamizi wa rasilimali zilizopitishwa juzi bungeni, lakini una hadhi sawa kwa sababu mapitio yake yalifanyika kwa umakini.

Pia, ametoa rai kwa watumishi wanaopewa dhamana ya kuingia mikataba kwa niaba ya wananchi, kutanguliza maslahi ya taifa mbele kwani hizi siyo nyakati za kuingia katika mikataba ambayo baadaye inawanyima haki  Watanzania.

“Huu siyo wakati wa kuingia katika mikataba tukiwa katika hali ya unyonge, tujifunze kubadilika kulingana na wakati, Si vyema tukaingia katika mikataba ambayo baadaye watu wanaanza kuhoji elimu zetu au kuuliza makubaliano hayo tuliyaingia tukiwa tunaangalia wapi,”amesema Profesa Kabudi.

Amesema baadhi ya mambo yaliyokuwa ndani ya mkataba wa zamani baina ya Serikali hayakuwa na manufaa kwa uchumi wa Watanzania lakini huu mpya utakuwa na manufaa kwa pande mbili kwani wawekezaji hawa siyo wahisani na wao wanahitaji faida.

Mkurugenzi Mkuu wa Ticts, Zerbe amesema mkataba huo umesainiwa baada ya kuwepo kwa mazungumzo  ya muda mrefu  na sasa umemalizika salama.

“Mvutano na kamati ulikuwa mkali lakini tulifikia makubaliano. Tumekuwa hapa kwa muda mrefu sasa nasi tunaona ni sehemu salama ya kuendelea kukaa, bandari hii ina wateja wengi wa ndani na nje hivyo tunatarajia kuendelea kufanya biashara vizuri hata ndani ya mkataba huu mpya,”amesema Zerbe.

Mwenyekiti wa kamati iliyofanya mapitio ya mktaba huo, Hamza Johari ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) Tanzania, amesema;

 “Haikuwa kazi rahisi kufanikisha jambo hilo lakini tulitanguliza mbele weledi na uzalendo ndiyo maana tumefanikiwa.”