Ndugai ajigamba na 'cleen sheet' aliyopiga 2020, ajipanga tena

Muktasari:
- Hatua ya Mbunge wa Kongwa kufurahia ushindi wa "cleen sheet'' anayopata kila chaguzi zinafanyika ilivyoibua mvutano wa aina yake na Mbunge wa Kibakwe Simbachawene, huku Wasira akitoa neno kutuliza mjadala huo.
Kongwa. Mbunge wa Kongwa (CCM), Job Ndugai amesema uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 wanausubiri kwa shauku kubwa huku akijigamba kupata ushindi wa 'cleen sheet' kila chaguzi zinapofanyika ni sababu ya eneo hilo kuwa kitovu na ngome ya demokrasia kwa CCM mkoani humo.
Ndugai ambaye ni Spika mstaafu wa Bunge la Tanzania, amejenga hoja hiyo kwa kujinasibisha na ushindi wa kishindo walioupata katika uchaguzi mkuu wa 2020, huku akisema walifanya vizuri ikilinganisha na majimbo mengine ndani ya mkoa huo.
Amesema hayo leo Alhamisi, Aprili 24, 2025 katika mkutano uliofanyika Kongwa, mgeni rasmi akiwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira aliyekuwa anapita kukagua utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama hicho
"Kongwa ni nguzo na tegemeo kubwa la Mkoa wa Dodoma, sisi huwa hapa tunashinda kwa 'Cleen Sheet' wajumbe wote wa serikali za vijiji, vitongoji vyote, wenyeviti wote, madiwani wote mbunge ndiyo usipime," amesema Ndugai huku akishangiliwa na makada wa chama hicho waliokuwa wakisema mitano tena.
Amesema kutokana na morali waliyonayo kikubwa wanasubiri uchaguzi wa Oktoba 2025.

"Kikubwa tupeleke salamu kwa Rais Samia Suluhu Hassan, watu wa Kongwa wanachosubiri ni masanduku ya kura tu basi, maneno mengine hakuna tuko imara zaidi na kikubwa nisisitize apumzike atulie tutampa mitano tena," amesema na kuongeza.
"Na Mbunge wetu Ndugai mitano tena na tumejipanga mtoa rushwa hawezi kutokea."
Wakati Ndugai akijimwambafai hivyo, hoja hiyo iliibua ukinzani wa kiutani na Waziri wa Nchi Ofisi Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene aliyekuwa anazungumza kama mbunge Kibakwe alipinga hoja hiyo.
"Mimi naomba nipingane naye ili t baada ya uchaguzi tuone ngome hapa itahama au haihami kule Mpwapwa na Bahi wanasema ni ngome, Kondoa nako hivyohivyo hapa mwenyekiti dawa yake kutushindanisha tu atakayeshinda ni ngome," amesema
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM, mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa amesema pamoja na kwamba Kongwa iliongoza kwa kufanya vizuri kwenye uchaguzi wa 2020, lakini deni walilonalo mbele halifanani na lile la uchaguzi uliopita.
"Deni la safari hii ni kubwa mno, Rais Samia amefanya mengi makubwa katika maendeleo na dawa ya deni ni kulipa na tunatakiwa kumlipa kupitia kura," amesema Kimbisa.
Kwa upande wake, Wasira pamoja na tambo za wabunge hao bado msimamo wa chama hicho ni kuwasikiliza wananchi ili wapate mtu anayekubalika na wote.
"CCM safari hii hatutaki kujichosha, hatutaki kubeba mizigo kama umepakia kwenye mkokoteni halafu unasukuma hatutaki, mnasema Ndugai mitano tena, Simbachawene mitano tena je, wanakubalika lakini waamuzi wa mwisho ni wajumbe," amesema Wasira.