Prime
Mbunge akosoa elimu vyuoni, ahoji taaluma zisizo na soko

Mbunge wa Kuteuliwa, Shamsi Vuai Nahodha akichangia katika bajeti ya katika Mkutano wa 19 wa Bunge la Bajeti, kujadili taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kwa mwaka kwa mwaka wa fedha 2025/26. Video na Hamis Mniha
Muktasari:
- Ni mbunge wa kuteuliwa, Shamsi Vuai Nahodha aliyehoji kuna maana gani kwa sasa wanafunzi kusoma historia ya dunia na masuala ya fasihi , wakati hayawasaidii kwenye soko la ajira au kujiajiri.
Dodoma. Mbunge wa kuteuliwa, Shamsi Vuai Nahodha amesema mfumo wa elimu ya vyuo vikuu nchini, una kasoro na bila kuzitafutia ufumbuzi hajui Taifa linaelekea wapi.
Amesema kuendelea kuamini kuwa elimu ya chuo kikuu ndiyo kila kitu, ni kuchelewa kwani kuna wengine wanaosoma shahada za kama Kiswahili, lakini wakikutana kwenye midahalo na wenzao ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, wanakwama kimaarifa.
Nahodha ametoa kauli hiyo bungeni jijini Dodoma leo Alhamisi April 24, 2025 wakati akichangia Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Wizara ya Mipango na Uwekezaji ya mwaka 2025/2026 iliyowasilishwa na Waziri Profesa Kitila Mkumbo.
Profesa Kitila Mkumbo ameliomba Bunge kuidhisha mapato na matumizi ya Sh148.639 bilioni kwa ajili ya wizara hiyo na taasisi zake.
Akiwa mchangiaji wa kwanza kwa bajeti hiyo, Nahodha aliyewahi kuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), amesema elimu bora inaweza kulisaidia Taifa, lakini elimu ya vyuo vikuu isipowekewa mkakati inaweza kupotosha.
Kauli ya mbunge huyo imekuja ikiwa imepita miezi minne tangu mtaalaa mpya wenye maboresho kwa elimu ulipoanza kutumika kwa wanafunzi wa madarasa ya awali hadi kidato cha nne.
Hata hivyo amesema kufanya maboresho katika mitalaa ya elimu ya chini, lakini vyuo vikuu vikasahaulika ni sawa na kujaza wasomi wenye shahada wasiokuwa na mchango kwa Taifa .
Nahodha ametaja sababu mojawapo kwenye mfumo wa elimu ni kuendelea kutumia mbinu za kufundishia, ambazo zimepitwa na wakati na akapendekeza mambo manne ya kufanyia maboresho vyuo vikuu.
“Napendekeza mambo manne, kwanza tuwape wanafunzi wajibu mitihani kwa kutazamia vitabuni, siyo majibu ya kawaida. Pili tuwape kazi maalumu wanafunzi (project) na tatu wanafunzi wajifunze masuala ya uchambuzi,” amesema Nahodha.
Pendekezo la nne ni kutaka wanafunzi wawe na mawasilisho ambayo yataonyesha vipaji vyao, akisisitiza elimu ya ujuzi ipewe kipaumbele zaidi katika karne hii.
Amehoji kwa nini wanafunzi katika karne ya sasa wanaendelea kujifunza historia ya dunia ambayo huenda isiwe na maana kwao, badala ya kujifunza vitu vinavyoweza kuwasaidia katika maisha yao.
“Tunaandaa Taifa la namna gani, unamfundisha mtu ununuzi badala ya ujasiriamali; unamfundisha sosholojia badala ya saikolojia ya vitendo; unamfundisha mtu sarufi ya Kiswahili na Kiingereza badala ya lugha maalumu na mwingine unamfundisha fasihi badala ya uandishi wa ubunifu, tubadilike,” amesema Nahodha.
Aidha, amekosoa mfumo wa udahili kwa wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu Tanzania,akisema hauko rafiki na mazingira yaliyopo hivi sasa ukilinganisha na vyuo vingine duniani.
Akitolewa mfano wa udahili ameshangazwa kwamba mwanafunzi aliyemaliza stashahada akienda kujiunga chuo kikuu kwa baadhi ya taaluma ikiwemo uganga na sheria, lazima wamuulize cheti cha kidato cha sita ambacho anasema watu huwa wamefaulu masomo matatu tena wengi kwa kukaririshwa.
Mbunge huyo ametoa mfano wa baadhi ya nchi zilizoanza kuachana na wingi wa shahada kuwa ni China ambayo ilibadili vyuo vikuu karibu 600 na kuwa vya kati vinavyofundisha ujuzi, huku Rais wa Marekani Donald Trump akianzisha chuo kikuu cha ujuzi nchini mwake.
Mbunge wa Kiteto, Edward Olelekaita amesema mchango wa Nahodha unapaswa kupewa mkazo na kuzingatiwa akitolewa mfano wa jinsi ya kujibu mitihani kwa wanasheria kwamba huwa lazima watumie rejea ya vitabu.