Profesa Kitila ataja vipaumbele vitano Ofisi ya Msajili wa Hazina

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo
Muktasari:
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amewasilisha bajeti ya wizara hiyo huku akiainisha vipaumbele vitano ambavyo vitakwenda kutekelezwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amewasilisha bajeti ya wizara hiyo huku akiainisha vipaumbele vitano ambavyo vitakwenda kutekelezwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Vipaumbele hivyo vinalenga kuongeza ufanisi wa kiutendaji katika taasisi za umma, usimamizi wa rasilimali za umma na kukuza mapato yasiyo ya kodi.
Profesa Kitila amewasilisha bajeti hiyo leo Alhamisi, Aprili 24, 2025 bungeni mjini Dodoma ambapo, ameomba Bunge kuidhinisha Sh148.63 bilioni kwaajili ya kutekeleza shughuli na vipaumbele mbalimbali.
Miongoni mwa maeneo ya vipaumbele kwa upande wa Ofisi ya Msajili wa Hazina ni utekelezaji wa Mpango wa muda mrefu wa miaka 25, unaotarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2025/26 hadi mwaka 2049/50.
Mpango huu utatoa mwongozo wa muda mrefu kuhusu maeneo ya uwekezaji, usimamizi wa mali za serikali na mwelekeo wa kiuchumi unaoendana na dira ya taifa.
Profesa Kitila amesema Serikali itaendelea kufanya tathmini na ufuatiliaji wa mali za Serikali zilizopo chini ya usimamizi wa Ofisi ya Msajili pamoja na zile zilizobinafsishwa, ikiwemo mashamba, viwanda, nyumba na viwanja.
“Lengo la Serikali ni kuhakikisha matumizi bora ya rasilimali hizo kwa manufaa ya umma,” amesema.
Katika kuongeza ufanisi, Serikali imepanga kuimarisha matumizi ya TEHAMA ili kuuongeza ufanisi wa Ofisi ya Msajili katika ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kikodi.
Maboresho hayo yatawezesha upatikanaji wa takwimu kwa wakati, kuongeza uwazi na kurahisisha usimamizi wa mapato yasiyo ya kodi.
Kutokana na umuhimu wake, mashirika ya umma yamehimizwa kutenga bajeti kwa ajili ya kuwekeza kwenye mifumo ya TEHAMA inayosomana.
Pia ofisi hiyo kwa mwaka ujao wa fedha, itajikita kwenye kuboresha usimamizi wa taasisi na mashirika ya umma, kampuni tanzu na zile ambazo Serikali ni mbia.
Hili linajumuisha matumizi ya miongozo maalum kuhusu majukumu ya wajumbe wa bodi, tathmini ya utendaji kazi na nafasi ya wawakilishi wa Serikali katika taasisi zenye umiliki wa hisa chache.
Miongozo hiyo ni pamoja na Waraka wa Msajili wa Hazina Na. 1 wa mwaka 2023, Mwongozo wa Majukumu na Matarajio ya Serikali kwa Wajumbe wa Bodi, Mwongozo wa tathmini ya utendaji kazi wa Bodi za Wakurugenzi na Mwongozo wa Wawakilishi wa Serikali kwa Taasisi ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache.
Kwenye kuimarisha uwezo wa kiutendaji kwa watumishi wake, kwa kuwajengea uwezo ili kuongeza tija na ufanisi wa kazi zao.
Kwa upande wa mapato, Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imepanga kukusanya Sh1.56 trilioni katika mwaka wa fedha 2025/26.
Mapato hayo yatatokana na vyanzo visivyo vya kodi kama gawio kutoka mashirika ya umma, michango ya asilimia 15 ya mapato ghafi, mapato kupitia mfumo wa TTMS, pamoja na rejesho la mikopo, riba na mapato mengineyo.
Kiasi hiki ni ongezeko kutoka Sh1.113 trilioni zilizoidhinishwa katika mwaka wa fedha unaoishia, yaani 2024/25.
Hadi kufikia Machi 2025, jumla ya Sh664.53 bilioni zilikuwa zimekusanywa, sawa na asilimia 60 ya lengo la mwaka mzima na asilimia 86 ya lengo la kipindi hicho.
"Tuna imani kuwa lengo la mwaka wa fedha 2024/25 la kukusanya Sh1.113 trilioni litatimia kwani sehemu kubwa ya makusanyo itapatikana katika kipindi cha robo ya nne ya mwaka," amesema Profesa Kitila.