THRDC yalaani madai kukamatwa kina Lissu, waandishi wa habari

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa

Muktasari:

  • Hatua ya Jeshi la Polisi kuwakamata viongozi na wafuasi kadhaa wa Chadema, imeendelea kulaaniwa na kupingwa na wadau mbalimbali, ukitajwa ni uamuzi unaokwenda kinyume na ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Dar es Salaam. Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), umeungana na wadau wengine kulaani kukamatwa kwa viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na wanahabari wakielekea katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani jijini Mbeya.

THRDC imetoa tamko hilo  leo Jumatatu, Agosti 12, 2024, ikidai takribani watu 300 wamekamatwa na Jeshi la Polisi, akiwemo Makamu Mwenyekiti wa Chadema-Bara, Tundu Lissu, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika na Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu.

Wengine wanaodaiwa kukamatwa ni Wakili Deogratias Mahinyila na waandishi wa habari wa Jambo Tv ambao ni Ramadhan Khamis na Fadhil Kirundwa. Pia wamo viongozi wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Twaha Mwaipaya, Moza Ally, Deusdedith Soka na wengine.

Kabla ya THRDC kutoa tamko hilo, jana Jumapili Agosti 11, 2024, Chadema ililaani na kupinga kitendo hicho ikilitaka jeshi hilo liwaachie mara moja na kusitisha kuwahoji, kwa kuwa walichotarajia kukifanya ni haki yao ya kidemokrasia na kikatiba.

Mzizi wa yote hayo ni uamuzi wa Bavicha kupanga maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani katika viwanja vya Ruanda Nzovwe jijini Mbeya na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ndiye alitarajiwa kuwa mgeni rasmi. Maadhimisho hayo yalipangwa kufanyika leo Jumatatu, Agosti 12, 2024.

Kilichosababisha shughuli hiyo iingiliwe kati na Jeshi la Polisi ni kauli ya Bavicha iliyohusisha mfano wa kilichofanywa na vijana wa nchini Kenya, ikiwasifu wamejitambua, jambo lililotajwa kama dalili ya vurugu.

Kabla ya Jeshi la Polisi kuwakamata viongozi hao, lilipiga marufuku kufanyika kwa shughuli hiyo, ikisisitiza kuna viashiria vya uvunjifu wa amani na vurugu ndani yake.

Polisi ilitangaza uamuzi huo, ukitanguliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kumwandikia barua Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika Agosti 8, 2024 kumtaka kusitisha shughuli yoyote iliyopangwa ufanyia leo (Agosti 12) kwa kile alichodai lugha za viongozi wa Bavicha zinaashiria uvunjifu wa amani.

Barua hiyo ambayo nakala ilitumwa kwa Inspekta Jenerali wa Polisi nchini (IGP), iliwataka viongozi wa Chadema, akiwemo Mbowe, Mnyika na Mwenyekiti wa Bavicha, John Pambalu kufika ofisi ya Msajili jijini Dar es Salaam, kesho Jumanne, Agosti 13, 2024 saa 5:00 asubuhi.

Hata hivyo, jana jioni, Mnyika baada ya kuwasili jijini Mbeya akiwa na Lissu na viongozi wengine, alizungumza na waandishi wa habari akisema wamepokea barua: “Na hatutakwenda.” Huku akimtaka msajili kufanyia kazi kauli nyingine alizodai zimekuwa zikitolewa na viongozi wa vyama vingine.

Asubuhi ya leo Jumatatu, Mwananchi limemtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga kuhusu taarifa za kukamatwa viongozi hao na simu ilipokelewa na msaidizi wake aliyesema yupo kikaoni, ataturudia baadaye.

Hata hivyo, jana usiku alipotafutwa aliomba apewe muda awasiliane na Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO), kwani yupo katika shughuli nyingine za kikazi.

“Ndiyo maana nimekuambia kwa sasa hivi kuna kazi nyingine naifanya, mpaka nizungumze na RCO, nitajua kuhusu jambo hilo,” amesema Kuzaga.


Tamko la THRDC

Katika tamko lake, THRDC imenukuu Ibara ya 18 na 20(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotoa haki na uhuru wa watu kujumuika, kufanya mikutano, maadhimisho na kueleza mawazo yao.

“Haki hizi hazipo kwenye Katiba peke yake, bali zipo kwenye mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda ambayo Tanzania imeridhia,” imeeleza sehemu ya tamko hilo.

Imeeleza ukamatwaji huo unafifisha uhalisia wa maridhiano, ustahimilivu na mabadiliko ambayo Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akihubiri tangu alipoingia madarakani.

“Tunatoa wito kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini kuwaachilia huru watu wote waliokamatwa bila masharti, ili kuadhimisha Siku ya Vijana Duniani kama ambavyo vyama vingine vimeshaadhimisha na hatukuona wakikamatwa,” imeeleza taarifa hiyo.

Tamko hilo, limehusisha wito kwa viongozi wengine wa nchi kuanzia Rais Samia walione suala hilo kuwa linatia doa nchi, hivyo wachukue hatua za haraka ikiwemo kuwaachia watu wote.

“Pia tunawashauri viongozi wa vijana na vijana wote watakaoshiriki katika maadhimisho hayo wazingatie masuala ya utulivu, amani na sheria za nchi yetu,” imeeleza.