Mbowe atia mguu madai kina Lissu kukamatwa Mbeya

Muktasari:

  • Mbowe amesema viongozi hao wakuu wa chama na Bavicha waachiwe bila masharti.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe amelitaka Jeshi la Polisi kuwaachia viongozi wakuu wa chama hicho wanaodaiwa kukamatwa mkoani Mbeya jana Jumapili Agosti 11, 2024.

Mbowe amesema hayo jana usiku kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X (zamani Twitter), ikiwa ni saa chache tangu Polisi ikataze kongamano la vijana wa chama hilo lililopangwa kufanyika leo Jumatatu Agosti 12, 2024 mkoani Mbeya.

“Tunalaani vikali Jeshi la Polisi kukamata viongozi wetu wakuu wa chama, wakiwemo viongozi wa Baraza la Vijana wa Chadema, Bavicha,”ameandika.

Pia, ameongeza; “Tunadai kuachiwa haraka na bila masharti viongozi, wanachama na wapenzi wetu wote waliokamatwa maeneo mbalimbali ya nchi.”

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga alipoulizwa kuhusu taarifa za kukamatwa viongozi hao jana na Mwananchi, ameomba apewe muda awasiliane na Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO), kwani yupo katika shughuli nyingine za kikazi.

“Ndiyo maana nimekuambia kwa sasa hivi kuna kazi nyingine naifanya, mpaka nizungumze na RCO, nitajua kuhusu jambo hilo,”amesema Kuzaga.

Hata hivyo, jana asubuhi, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa jeshi hilo, Awadhi Juma Haji alitangaza marufuku ya kongamano hilo lililopangwa kufanyika leo jijini Mbeya, huku akisema watakaokaidi hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa.

 Mbali na Mbowe kuzungumzia kuakamatwa kwa viongozi wa chama hicho, pia amekinzana na kauli iliyotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusu kuzuia kongamano la Bavicha.

“Aidha, tunalaani mkakati wa Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kushirikiana na polisi kuzuia kongamano la Bavicha katika kuadhimisha siku ya vijana duniani hapo kesho Jumatatu Agosti 12 (leo),”ameandika Mbowe.

 Msingi wa kauli ya Mbowe kuhusu ofisi ya msajili inaijibu barua ya kuzuiwa kwa kongamano hilo (ambayo Mwananchi imeiona), imeandikwa Agosti 8, 2024 na Msajili wa Vyama vya Siasa iliyosainiwa na Naibu Msajili, Sisty Nyahoza kwenda kwa Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika.

Katika barua hiyo, ofisi hiyo imewaasa viongozi wa Chadema kusitisha shughuli yoyote waliyopanga kuifanya Agosti 12, 2024 Mbeya au mahali popote nchini, ambayo wanajua itasababisha uvunjifu wa sheria, amani na utulivu, kwa maelezo ya Katibu Mwenezi wa Baraza la Vijana wa Chadema katika video hiyo.

“…yanakiuka sheria ya vyama vya siasa na yanaashiria, mkusanyiko huo unaweza kutumika kuhamasisha vijana kufanya vitendo vya uvunjifu wa sheria kama ilivyotokea Kenya,” imeeleza barua hiyo.

Aidha, Mbowe amesisitiza Chadema inafuatilia kwa makini yanayoendelea na kitaendelea kuuhabarisha umma kila linalojiri hatua kwa hatua.


 Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari na taarifa zaidi.