Lissu, Mnyika, Sugu wadaiwa kukamatwa na Polisi Mbeya

Mbeya. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linadaiwa kuwakamata viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akiwemo Tundu Lissu ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara.

Mbali na Lissu, wengine ni Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika na Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu.

Viongozi hao wamedaiwa kukamatwa usiku wa leo Jumapili, Agosti 11, 2024 wakiwa ofisi za Chadema Kanda ya Nyasa ikiwa ni saa chache tangu wawasili jijini Mbeya, kushiriki maadhimisho ya siku ya vijana duniani kesho Jumatatu yaliyoandaliwa na vijana wa Chadema (Bavicha).

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema akizungumza na Mwananchi usiku huu, amesema wanaendelea kufuatilia kujua Lissu na wenzake waliokamatwa wamepelekwa wapi.

Mrema amedai waliokamatwa wamepelekwa vituo mbalimbali vya Polisi

"Hatujajua kama makamu na katibu mkuu watabaki hapo au itakuwaje.  Ndio tunafuatilia."

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga alipoulizwa kuhusu taarifa za kukamatwa viongozi hao, aliomba apewe muda awasiliane na Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) kwani yupo katika shughuli nyingine za kikazi.

“Ndiyo maana nimekuambia kwa sasa hivi kuna kazi nyingine naifanya, mpaka nizungumze na RCO, nitajua kuhusu jambo hilo,”amesema Kuzaga.

Hata hivyo, mapema leo asubuhi, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa jeshi hilo, Awadhi Juma Haji alitangaza marufuku ya kongamano hilo lililopangwa kufanyika kesho jijini Mbeya huku akisema watakaokaidi hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi