Tanzania yasaka Sh33.6 trilioni kwa ajili ya upatikanaji nishati kwa wote

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba 9kwa kwanza kushoto) akizungumza katika Mkutano wa Jukwaa la Nishati Afrika jijini Cape Town nchini Afrika Kusini.Picha na Wizara ya Nishati.
Muktasari:
- Fedha hizo zitasaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa nishati kwa wananchi wote na kuifanya nchi kuwa kitovu cha nishati barani Afrika.
Cape Town. Tanzania inasaka Dola 12.9 bilioni za Marekani (Sh33.6 trilioni) kwa ajili ya kuharakisha upatikanaji wa nishati nafuu na endelevu kwa watu milioni 42 ifikapo mwaka 2030, huku ikitekeleza mikakati mbalimbali chini ya mpango wa Bara la Afrika unaojulikana kama Mission 300.
Serikali ilieleza hatua hiyo katika Mkutano wa 27 wa Jukwaa la Nishati (Africa Energy Forum) uliofanyika jijini Cape Town Jumatano, huku Tanzania ikiwasilisha Mpango wa Utekelezaji wa Mkataba wa Taifa wa Nishati (National Energy Compact Implementation Plan).
Fedha hizo zitasaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati kwa miaka mitano ijayo, kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa nishati kwa wananchi wote na kuifanya nchi kuwa kitovu cha nishati barani Afrika.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba, aliyewasilisha mpango wa Tanzania katika eneo hilo, mahitaji hayo ya fedha yanajumuisha Dola 8.85 bilioni za Marekani kwa ajili ya uwekezaji wa umma na Dola 4.04 bilioni zitakazotokana na uwekezaji binafsi.
Amesema fedha hizo zitatumika katika uzalishaji, usafirishaji, usambazaji, ukarabati, miundombinu ya mwisho kwa wateja, usambazaji nje ya gridi kuu, upishi safi na ujenzi wa uwezo wa kitaasisi.
“Mathalani Tanzania, tunatarajia ongezeko kubwa la mahitaji ya umeme kwa asilimia 10 hadi 18 kwa mwaka katika kipindi kifupi kijacho,” amesema Mramba mbele ya washiriki wa mkutano huo.
Amesema Tanzania katika kipindi cha mwaka mmoja, uwezo wa uzalishaji wa umeme uliounganishwa kwenye gridi ya Taifa umeongezeka hadi megawati 4,031.71 kufikia Aprili 2025, sawa na ongezeko la asilimia 86.6 kutoka megawati 2,138 zilizokuwepo Machi 2024.
Kwa mujibu wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati, kati ya kiwango kinachozalishwa megawati 2,716.27 (sawa na asilimia 67.4) zinatokana na umeme wa maji, megawati 1,198.82 (asilimia 29.7) kutoka gesi asilia, megawati 101.12 (asilimia 2.5) kutoka mafuta, megawati 5 (asilimia 0.1) kutoka jua, na megawati 10.5 (asilimia 0.3) kutoka vyanzo vya biomasi.
Mramba pia amesisitiza faida ya kijiografia ya Tanzania ambayo ni mwanachama wa East African Power Pool (EAPP) na Southern African Power Pool (SAPP), akisema ina fursa kubwa ya biashara ya umeme miongoni wanachama wenzake.
“Tutakuwa tayari ifikapo mwakani kusafirisha umeme kutoka kaskazini kwenda kusini kwa kadri tunavyotekeleza miradi ya kikanda,” amesema Mramba na kuongeza kwa Tanzania inalenga kuendeleza rasilimali zake kubwa za gesi asilia na vyanzo mbadala vya nishati, zikiwemo umeme wa maji, jua, upepo, biomasi, na jotoardhi.
Amesema hatua hiyo itafanikishwa kupitia ‘Mission 300’ mpango wa pamoja unaoongozwa na Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), ukiwa na lengo la kuwapatia huduma ya umeme Waafrika milioni 300 ifikapo mwaka 2030.
Mradi huo unalenga kupanua upatikanaji wa nishati, kuboresha ufanisi wa mashirika ya nishati, kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi, na kuboresha uhusiano wa kikanda wa nishati Afrika.
Miongoni mwa maeneo makuu ya utekelezaji wa Mission 300 uunganishaji wa mwisho kwa wateja (last-mile connectivity) unakadiriwa kugharimu zaidi ya Dola 3.5 bilioni za Marekani, ukifuatiwa na uzalishaji wa nishati kwa Dola 4.1, bilioni za Marekani, miradi ya ukarabati kwa karibu Dola bilioni 1.4 za Marekani, na miradi ya upishi safi ikihitaji Dola milioni 800 za Marekani.
Mramba pia ameeleza baadhi ya hatua kuu ambazo Tanzania inapanga kuchukua ndani ya miezi 18 ijayo kutekeleza mkataba wa Mission 300.
Ili kuweka msingi wa upatikanaji wa nishati kwa wote, Tanzania inapanga kutekeleza hatua kadhaa za kipaumbele, zikiwamo kuanzisha mpango wa ununuzi wa uzalishaji wa Nishati Mbadala kwa Wazalishaji huru wa Umeme (Renewable Energy Independent Power Producer Procurement Programme - REI4P).
Hatua nyingine ni kuanzisha kitengo cha biashara ndani ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa ajili ya kurahisisha biashara ya umeme wa kuvuka mipaka; kununua na kufunga vifaa vya msingi vya kuoanisha mifumo na kutekeleza miradi ya kuunganisha nchi za kikanda kama vile njia ya msongo wa kilovoti 400 kati ya Uganda na Tanzania, na ile kati ya Tanzania na Zambia.
Tanzania pia, inapanga kuzindua mfuko kwa ajili ya kusaidia ufikishaji wa huduma za umeme, kuanzisha Mfuko wa Taifa wa Upishi Safi na kupunguza kodi na ushuru kwa majiko yenye ufanisi na vifaa vya kupikia visivyochafua mazingira pamoja na kuanzisha rasmi Kituo cha Uwekezaji wa Nishati Mbadala na kuhuisha viwango vya bei kulingana na gharama kwa wazalishaji wadogo wa umeme (SPPs).
Mipango mingine ni kuanzisha miradi ya majaribio ya usafirishaji huru wa umeme katika maeneo ya Shinyanga, Sumbawanga, Songea na Kibiti; kupitia upya muundo wa viwango vya bei ya umeme chini ya mfumo wa miaka mingi unaozingatia motisha; kuboresha mipango ya utendaji wa mashirika ya huduma chini ya usimamizi wa udhibiti na kujenga mustakabali endelevu wa nishati.
Mpango huu umejikita katika nguzo tano za kimkakati: ukarabati na upanuzi wa miundombinu; kutumia faida za ujumuishaji wa kikanda; kuunganisha wateja wa mwisho na matumizi ya nishati safi ya kupikia, kutoa motisha kwa sekta binafsi na kuboresha ufanisi wa kifedha wa mashirika ya nishati.
Wakati wa mkutano huo, Serikali ilisisitiza dhamira yake ya kutekeleza mageuzi, ikibainisha hatua zilizopigwa katika mapitio ya sera, uboreshaji wa kifedha wa mashirika ya nishati na uhamasishaji wa rasilimali.