Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kauli ya ‘mwanamme suruali’ ilivyosababisha mauaji

Tabora. Ni kweli ndoa inahitaji uvumilivu lakini kuna maneno ukimtamkia mumeo yanaweza yasikuache salama, hiki ndicho kilichotokea, baada ya mume kumuua mkewe bila kukusudia baada ya kuitwa mwanamume suruali.

Kauli hii ilikuja baada ya mume kubembeleza apewe tendo la ndoa alilokuwa amenyimwa kwa miaka miwili na mkewe, na siku hiyo alikuwa ameahidiwa kupewa lakini wakati akiomba haki yake akanyimwa na kutamkiwa maneno hayo.

Mauaji hayo yaliyochangiwa na mgogoro baina ya mume na mke kutokana na mke kumnyima mumewe haki ya tendo la ndoa, na baadaye mke kutamka maneno yaliyokuwa kiini cha mauaji, yanaweza kuwa fundisho tosha kwa wanandoa.

Omary Kabwedeke ambaye Aprili 24, 2020 alimuua mkewe Hawa Juma bila kukusudia huko kijiji cha Isikizya wilaya ya Uyui mkoani Tabora, alihukumiwa kifungo cha maisha jela, lakini akapambana kupinga adhabu hiyo kwa kile alichokieleza kuwa ni kubwa.

Mungu si Athuman, jana Jumanne, Julai 1,2025, majaji watatu, Rehema Mkuye, Dk Paul Kihwelo na Dk Ubena Agatho wamebaini dosari za kisheria na kurejesha jalada kwa jaji aliyesikiliza shauri hilo, ili ampe Kabwedeke adhabu kwa mujibu wa sheria.

Majaji hao walisema tangu Juni 3, 2022, mrufani anatumikia adhabu batili.


Tukio la mauaji lilivyokuwa

Ushahidi ulieleza siku ya tukio Aprili 24, 2020 saa 2:00 usiku, mshtakiwa ambaye katika shauri hili la rufaa ni mrufani, alirejea nyumbani kutoka katika shughuli zake za kila siku na kuwakuta watoto wake Amina Omary na Rahma Moshi.

Mshtakiwa akakaribishwa mezani kwa ajili ya chakula cha usiku lakini alikataa na kwenda nje na kukaa huko kwa muda mfupi na kurudi, baadaye usiku watoto walikwenda kulala chumba chao na mume na mke nao wakaenda chumbani kwao.

Usiku wa manane, shahidi wa pili, Rahma alimsikia mama yake akipiga kelele za kuomba msaada ambapo alitoka chumbani na kwenda katika chumba cha wazazi wake na kumkuta baba yake wa kambo akimpiga mama yake kwa mkuki.

Akiwa amechanganyikiwa na asijue afanyeje, alikimbia na kutoka nje ya nyumba akifuatiwa na mdogo wake (Amina) na kupiga mayowe ili kuomba msaada ambapo alijitokeza jirani yao, Hassan Kizota aliyekuwa shahidi watatu.

Baada ya kumweleza nini kinamkuta mama yao kwamba ameshambuliwa vibaya na baba yao, jirani huyo aliwachukua na kuwapeleka nyumba ya jirani na yeye kurudi eneo la tukio, wakati huo akiwa na mwenyekiti wa mtaa wanaoishi.

Waliporudi katika nyumba hiyo walimkuta mshtakiwa akiwa amekaa nje ya nyumba na walipomuuliza kulikoni aliwaeleza kumetokea kupishana maneno na mkewe na kusababisha kufikia hatua ya kupigana na kwa utiifu akawapeleka chumbani.

Ndani kulikuwa na mazingira ya kuogofya kwani walikuta marehemu alikuwa amelala kwenye dimbwi la damu akiwa na majeraha ya kuchomwa mara mbili, huku mkuki ukiwa pembeni ya kitanda.

Mshtakiwa alikiri mbele yao kuwa amemuua mkewe kutokana na kutoelewana muda mrefu ndani ya ndoa yao na kilele cha kutoelewana ni siku hiyo, ambapo taarifa ya tukio ilitolewa kwa uongozi wa kijiji na baadaye polisi.

Shahidi wa nne, G.7846 Konstebo Matiku ambaye ni ofisa wa Polisi ambaye alimkamata mshtakiwa usiku uleule wa mauaji, alieleza alivyomkamata na hata alipofikishwa mahakamani, hakukanusha kuhusika na mauaji ya mkewe.

Kwa upande wake, shahidi wa tano ambaye ni mtendaji wa kijiji, Ramadhan Yusuph hakuwa na ushahidi unaotofautiana sana lakini shahidi wa kwanza, Dk Andrea Sikaluanda ambaye aliuchunguza mwili wa marehemu kubaini kiini cha kifo.

Katika ushahidi wake, shahidi wa sita, Jackline Lukuba, mlinzi wa amani alieleza mshtakiwa alivyokiri mbele yake kutenda kosa hilo na shahidi wa saba, G.6650 Konstebo Sharif alieleza mshtakiwa alikiri kosa katika maelezo aliyoyaandika.


Kauli ya ‘mwanamume suruali’

Katika utetezi wake kizimbani chini ya kiapo, mshtakiwa hakukanusha maelezo kuwa alimshambulia mkewe hadi kumsababishia kifo, na alitumia dakika moja kuelezea uhusiano wao wa mke na mume ulivyopitia katika misukosuko mingi.

Kwa mujibu wa ushahidi uliochambuliwa na majaji hao, mshtakiwa alieleza uhusiano wao kama wanandoa ulikuwa na hasira, hisia mbaya, ukosefu wa nia njema kipindi kirefu cha ndoa yao na kuifanya ndoa isiyo na amani.

Alifafanua kuwa kwa ujumla ndoa yao ilikumbwa na mabishano ya kindoa kuhusu haki ya tendo la ndoa kwa zaidi ya miaka miwili, lakini kilele cha mahusiano kilifikia usiku wa siku ya tukio ambapo marehemu alikataa kumpa tendo la ndoa.

Mshtakiwa huyo aliieleza Mahakama kuwa anakumbuka siku ya tukio haikuwa ni mwanzo, kwani mwaka 2018 ndio alianza kumnyima tendo la ndoa na jitihada za kuwasuluhisha hazikuzaa matunda licha ya kuahidi kumpa mara kadhaa bila utekelezaji.

Siku ya tukio kwa mujibu wa mshtakiwa, mkewe alikuwa amemwahidi angempa tendo la ndoa na siku hiyo kwa mara ya kwanza mkewe alilala nusu utupu kuelekea eneo ambalo mumewe hulala, jambo ambalo kwake lilikuwa si la kawaida.

Lakini kwa mshangao, mkewe aliendeleza msimamo wa kumnyima licha ya kumuomba mara kadhaa usiku huo kiasi cha kutolala na hapo ndio alishindwa kuzuia hasira aliyokuwa nayo hasa baada kumtusi na kumdhalilisha.

Anaeleza mkewe alimwambia ni ‘mwanamme suruali’, na ndipo alipochukua mkuki na kumshambulia nao marehemu mara mbili na alikuwa anajutia kitendo hicho ambacho kilitokea bahati mbaya ndio maana hakutoroka.

Katika ushahidi huo kwa ujumla wake, iliona Jamhuri imethibitisha mshtakiwa alitenda kosa hilo lakini hata hivyo, mahakama iliona mshtakiwa alithibitisha kuwa alichokozwa (provoked) na marehemu mwenyewe.

Hivyo Mahakama ikamuona ana hatia ya kosa la kuua bila kukusudia badala ya kosa la kuua kwa kukusudia alilokuwa ameshtakiwa nalo, hivyo Juni 3,2022 ikamuhukumu kifungo cha maisha jela kwa mujibu wa kifungu cha 295 cha CPA.

Hakuridhika na hukumu hiyo na Oktoba 20, 2022 alikata rufaa Mahakama ya Rufani akieleza adhabu aliyopewa ilikuwa kubwa mno na jaji alikosea kwa kushindwa kuzingatia maombolezo aliyoyatoa kabla ya kutamka adhabu.


Mabishano ya kisheria

Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo iliyosikilizwa Juni 23,2025, mrufani aliwakilishwa na wakili Kelvin Kayaga wakati mawakili wa Serikali Joseph Makene na Aziza Mfinanga wao walisimama kuiwakilisha Jamhuri.

Akiunga mkono rufaa, wakili Kayaga alieleza jaji alikosea kisheria kwa kutompa adhabu kulingana na kosa la kuua bila kukusudia, jambo ambalo ni kinyume cha kifungu cha 312(2) cha sheria ya CPA kinachotaka adhabu itajwe kwenye hukumu.

Akirejea ukurasa wa 113 kumbukumbu za rufaa ambapo Jaji alimtia hatiani mrufani na ukurasa wa 114, wakili huyo alieleza uwepo wa dosari za kisheria zinazofanya mrufani awe anatumikia kifungo batili tangu Juni 3,2022.

Wakili huyo alisema kifungo cha maisha jela ni cha juu mno na wala Jaji hakuzingatia kuwa kosa lilitendeka katikati ya joto la shauku (heat of passion) na kulingana na kanuni za Jaji mkuu 2023, mrufani alistahili kupewa adhabu ndogo.

Wakili Mfinanga aliunga mkono rufaa hiyo kwa kigezo kuwa hapakuwa na adhabu iliyotolewa kwa mrufani na Mahakama Kuu kwa kuwa inaonekana alitiwa hatiani kwa kuua bila kukusudia, lakini adhabu haikuwa imetamkwa kisheria.

Kwa mujibu wa wakili huyo, mshtakiwa alipelekwa gerezani kutumikia kifungo cha maisha pasipokuwepo adhabu rasmi kinyume cha kifungu 298(3) na 312(2) vya CPA na kwamba hilo lilikuwa ni kosa na kushauri hukumu yote ifutwe.

Badala yake, alipendekeza hukumu sahihi iandikwe kuhusiana na kosa hilo akisisitiza kuwa kutokana na silaha iliyotumika ambayo ni mkuki na majeraha mawili aliyoyasababisha, basi adhabu ya kifungo cha maisha jela ni sahihi.

Hata hivyo, alipoulizwa maswali na jopo la majaji kuhusu uhalali wa adhabu hiyo, wakili huyo alibadili msimamo na kusema kifungo cha maisha ilikuwa ni adhabu kubwa na anastahili kifungo cha miaka isiyozidi 10 gerezani.


Hukumu ya majaji

Katika hukumu yao, jopo la majaji hao walisema baada ya kusikiliza mawasilisho ya mawakili hao, hoja iliyopo mbele yao ni kwamba jaji hakuwa amemtakia adhabu mrufani baada ya kusikiliza kesi hiyo na hatimaye kumtia hatiani.

Walisema ushahidi uliopo katika kumbukumbu za mahakama ni kwamba Jaji aliyesikiliza shauri hilo katika ukurasa wa 113,  alibadili hukumu na kuwa ya kuua bila kukusudia katika eneo la kosa la kuua kwa kukusudia.

Majaji hao walisema baada ya kumtia hatiani mshtakiwa, sheria inamtaka jaji au hakimu kutamka adhabu kulingana na sheria na hukumu lazima ionyeshe waziwazi kuwa jaji au hakimu alipitia mchakato wa kumpa adhabu mshtakiwa.

“Ni wazi jaji hakutoa adhabu kwa mrufani kama inavyotakiwa na kifungu 298(3) na 312(2) cha CPA na hili liko wazi kwenye kumbukumbu za mahakama, walisema majaji hao na kufafanua kuwa ni dosari na kufanya adhabu anayotumikia kuwa batili.

Majaji hao walisema kwa sababu hizo, wanaona rufaa hiyo ina mashiko na kwa mlolongo wa kimantiki, unataka kurudisha jalada kwa jaji aliyeisikiliza ili aziite pande mbili zitoe hoja ya adhabu sahihi inayopaswa kutolewa kisheria.