Tanzania yasaini mikataba mitatu uwekezaji Bandari na DP World

Muktasari:
- Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameshuhudia utiaji saini wa mikataba mitatu ya uwekezaji na uendelezaji wa Bandari ya Dar es Salaam kati ya Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Serikali ya Dubai kupitia Kampuni ya DP World.
Dar es Salaam. Hatimaye Serikali ya Tanzania imetia saini mikataba mitatu ya uwekezaji na uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam baina yake na Kampuni ya DP World kwa lengo la kuongeza ufanisi katika ndandari hiyo.
Kabla ya kutia saini mikataba hiyo, Serikali iliingia makubaliano na Serikali ya Dubai kuhusu uwekezaji huo (IGA) ambayo yalikosolewa na wadau mbalimbali. Hata hivyo, Serikali ilisisitiza mkataba huo utakuwa na manufaa makubwa.
Shughuli ya kutia saini mikataba hiyo imefanyika leo Jumapili, Oktoba 22, 2023 Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma na kushuhudiwa na Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na viongozi mbalimbali wa kisiasa na serikal;I wengine akiwemo Rais mstaafu, Jakaya Kikwete na Waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa amebainisha Serikali itatia saini mikataba mitatu na kampuni ya DP World.
Ameitaja mikataba hiyo ni mkataba wa nchi mwenyeji (HGA), mkataba wa ukodishaji na uendeshaji wa gati 4 – 7, na uendeshaji wa pamoja wa gati 0 – 3 kati ya TPA na DP World kwa shughuli za kibiashara na za kiserikali.
“Mikataba hii haihusishi shughuli zote za uendeshaji wa bandari ya Dar es Salaam wala bandari nyingine za Tanzania,” amesema Mbossa akiongeza tayari wameanza mchakato wa kumpata mwendeshaji wa gati 8 – 11 ambaye siyo DP World.
Mbossa amesema Serikali itakuwa inapata ada na tozo kutoka kampuni ya DP World ambazo zitaongeza mapato yake na kupunguza gharama za uendeshaji.
Pia, amesema Serikali imekuwa inatumia asilimia 90 ya mapato yote yanayokusanywa katika uendeshaji wa maeneo yaliyokodishwa. Hivyo, kwa mkataba huo, itapunguza matumizi hayo na kubaki na zaidi ya asilimia 60.
“Kutokana na mikataba hii, Serikali itaweza kubakia na zaidi asilimia 60 ya mapato yote kutokana na gharama zote za uendeshaji kwenda kwa kampuni ya DP World.
“TRA atakusanya mapato kutokana na idadi ya meli ambapo zimehudumiwa, kwa hiyo tukiongeza ufanisi, badala ya kuhudumia meli 90, tukahudumia meli 130 maana yake TRA atakusanya kodi katika meli 130 badala ya meli 90 ndani ya mwezi mmoja,” amesema Mbossa.
Mkurugenzi huyo wa TPA amesema wanategemea mapato yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika bandari hiyo yataongezeka kutoka Sh7.8 trilioni kwa mwaka 2021/22 hadi kufikia Sh26 trilioni ifikapo mwaka 2032.
Amesema mikataba hiyo mitatu imezingatia masuala mbalimbali kwa ajili ya manufaa ya nchi. Manufaa hayo ni kuhusisha baadhi ya magati ya bandari ya Dar es Salaa na siyo bandari yote. Pia amesema haihusishi bandari nyingine za mwambao wa maziwa makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa.
“Mkataba huu utakuwa na ukomo wa miaka 30 na utendaji wa DP World utakuwa ukipimwa kila baada ya miaka mitano na siyo miaka 100.
“Serikali kupitia TPA itakuwa na umiliki wa hisa katika kampuni itakayokuwa ikifanya kazi katika bandari ya Dar es Salaam,” amesema Mbossa.
Ameongeza kutakuwa na viwango vya utendaji kazi ambavyo mwekezaji atapaswa kuvifikia. Pia, watumishi wa sasa wa TPA watakuwa na nafasi ya kuchagua kubaki TPA au kuhamia kampuni ya DP World.
Mbossa amebainisha jukumu la ulinzi na usalama katika eneo la bandari na yake yaliyokodishwa yaliyokodishwa kwa DP World, litaendelea kubaki chini ya Serikali.
“Mwekezaji atalipa kodi zote za Serikali kwa kuzingatia sharia za Tanzania. Sharia za Tanzania ndiyo zitakazotumika katika utekelezaji wa mikataba hii. Watanzania pia watashiriki katika mkataba huu kupitia vifungu vinavyohusisha.
“Serikali itakuwa na haki ya kujiondoa katika mkataba huu pale itakapoona inabidi kufanya hivyo,” amesema Mbossa huku akishangiliwa na baadhi ya watu waliohudhuria hafla hiyo wakiwemo wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC).
Akizungumzia manufaa ya uwekezaji huo, Mbossa amebainisha ni pamoja na kuongeza ufanisi kwa huduma zitakazotolewa kwa meli na shehena, hali hiyo itavutia meli nyingi na shehena kupita katika bandari ya Dar es Salaam.
Pia, amesema utaboresha huduma katika bandari ya Dar e Salaam kwa kupunguza muda wa kuchakata nyaraka kwa kuwa kampuni ya DP World itatumia mifumo ya kisasa ya Tehama itakayofungamanishwa na wadau wote wa bandari.
“Kuongezeka kwa mapato ya serikali hususani ushuru wa forodha kufuatia ongezeko la shehena na meli. Kutaiongezea TPA uzoefu. Ajira kwa wafanyakazi wa TPA na ajira mpya kwa Watanzania kutokana na kupanuka kwa shughuli za uendeshaji wa bandari,” amesema.
Amesisitiza kwamba siku za kusafirisha mzigo kutoka Mashariki ya Kati zitapungua kutoka siku 30 hadi siku 15. Pia, itachochea sekta nyingine za uchukuzi kama vile reli na barabara kutokana na kuongezeka kwa shehena.
“Natoa rai kwa Watanzania wote wa sekta zote kujipanga na kutumia gfursa mbalimbali zitakazojitokeza kufuatia uwekezaji huu ikiwemo usafirishaji wa mizigo kutoka bandarini,” amesema mkurugenzi huyo.
Ameongeza uwekezaji huo utapunguza gharama za kusafirisha mizigo kupitia bandari ya Dar es Salaam.