Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NEC CCM kuhitimisha DP World

Dodoma. Zikiwa zimetimia siku 106 tangu Hamashauri Kuu ya CCM (NEC) ilipotoa maelekezo kwa Serikali kutaka elimu itolewe kwa wananchi kuhusu mkataba wa bandari suala hilo linaelezwa ni moja kati ya ajenda kwenye NEC inayokutana leo.

Mkataba huo ni wa makubaliano (IGA) kati ya Serikali za Tanzania na ya Dubai kuhusu uendelezaji wa bandari za bahari na maziwa kupitia kampuni ya DP World ya Dubai.

Mbali na ajenda hiyo, pia inatajwa kikao hicho huenda kikaigusa sekretarieti ya NEC kwa kufanya mabadiliko madogo kwa baadhi ya wajumbe kwa madai kuwa wanapwaya.

Taarifa za ndani za CCM zililitaarifu gazeti hili kuwa licha ya kuwapo mabadiliko, suala kubwa linalotarajiwa kuzungumzwa na NEC ni kuhitimisha hoja ya mkataba huo.

Mkataba wa IGA uliibua mjadala ukiwagawa wananchi katika makundi ya wanaounga mkono, wanaopinga vifungu na wanaotaka ufutwe wote.

Baada ya Juni 10, 2023 Bunge kupitisha Azimio kuridhia mkataba huo, NEC ya CCM iliyokutana jijini Dodoma Jumapili ya Julai 9, 2023, ilitaka Serikali kutoa elimu kwa wananchi kuhusu suala hilo.

CCM kupitia kwa Katibu wa Itikadi na Uenezi, Sophia Mjema alisema mkutano wa NEC wa Julai 9, 2023 ulipokea na kujadili taarifa ya makubaliano ya uwekezaji na uendeshaji wa bandari na kuazimia kuwa uwekezaji na uendeshaji ni kwa manufaa ya uchumi wa nchi hivyo uendelee.

“Uwekezaji huo ni utekelezaji wa vitendo wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020–2025, ibara ya 59, ukurasa wa 92, hivyo Halmashauri imetaka Serikali kuongeza kasi ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya uhalisia uliomo katika makubaliano ya uwekezaji na uendeshaji huo wa bandari,” alisema Mjema.

Kabla ya mjadala bungeni, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alitoa maelezo kuhusu manufaa kwa Taifa ikiwamo ufafanuzi wa muda wa mkataba ambacho kilikuwa miongoni mwa vipengere vyenye shaka.

Profesa Mbarawa alitoa ufafanuzi huo kutokana na kasoro zilizokuwa zikielezwa ikiwamo mkataba hauonyeshi muda halisi wa ukomo, hakuna vipengele vya moja kwa moja vinavyombana mwekezaji kuendeleza bandari, Serikali ya Tanzania haitaweza kumwajibisha mwekezaji huyo ikiwemo kuvunja mkataba huo endapo tu ikionekana kwamba baadhi ya vipengele muhimu vya kimkataba vimekiukwa.

Bunge katika Azimio lake lilisema mkataba huo utasaidia kuongeza fursa za ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kutokana na uwekezaji mkubwa na ongezeko la shehena ya mizigo itakayopitia Bandari ya Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Azimio hilo, mkataba utasaidia kuongezeka kwa ufanisi katika uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi na kuleta tija stahiki katika mnyororo wa thamani wa huduma za bandari nchini;

Pia, Azimio la Bunge lilisema mkataba huo utasaidia kuongezeka kwa Pato la Taifa kutokana na uboreshaji wa shughuli za kibandari na kuongeza tija na kuwezesha mwendelezo wa miradi mikubwa ya kimkakati.


Ajenda ya kisiasa

Suala la mkataba huo liligeuka ajenda ya kisiasa, huku viongozi wa upinzani na chama tawala wakishindana kutumia mikutano ya hadhara kuuzungumzia.

CCM ilifanya mikutano kadhaa ya hadhara nchini, ikitumia baadhi ya wabunge na mawaziri, wakati Chadema kupitia viongozi wake walifanya mikutano kueleza ni kwa nini unaupinga mkataba huo.


Waraka wa Maaskofu

Mjadala wa mkataba wa bandari pia uliligusa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), ambao Agosti 18, 2023 walitoa waraka uliopewa jina la Sauti ya Watu, Sauti ya Mungu ukiitaka Serikali kuwasikiliza wananchi kwa kusitisha utekelezaji wa mkataba huo.

“Tukisukumwa na dhamiri iliyo na lengo la kulinda rasilimali, mshikamano, amani, uhuru, na umoja wa kitaifa; tunathubutu kusema kuwa baada ya miaka 63 ya uhuru wa nchi hii, wananchi hawajapenda kuiachia Bandari ya Dar es Salaam apewe mwekezaji mmoja aiendeshe kwa vile Watanzania wenyewe wana uzoefu wa kuiendesha,” inasema sehemu ya tamko hilo lilosainiwa na Maaskofu 37 na kuongeza:

“Hivyo tukiwajibika kimaadili, tunaona ni jukumu la Serikali kusikiliza wananchi wanaotaka mkataba huu ufutwe.”

Katika hotuba aliyoitoa mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan, Agosti 21, mwaka huu katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Makumira (Tuma), jijini Arusha wakati wa maadhimisho ya miaka 60 ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Mkuu wa kanisa hilo, Askofu Fredrick Shoo (aliyemaliza muda wake) alisema:

“Mheshimiwa Rais, Kanisa lipo pamoja na wewe. Tutaendelea kukuombea na kukuunga mkono katika kulisukuma gurudumu la maendeleo ya nchi kwa masilahi mapana ya nchi yetu.”

Akijibu maswali ya waandishi wa habari katika mkutano hivi karibuni, aliyekuwa Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alieleza hatua zilizofuatwa baada ya Mahakama Kuu kuitupa kesi iliyokuwa imefunguliwa kupinga mkataba wa IGA.

“Hakuna ukimya, Serikali ilishasema kwamba inapokea maoni ya Watanzania, baada ya kukamilisha michakato yote, Bunge limeridhia, hatua inayofuata sasa ni kuandaa nyaraka. Zikikamilika sasa ndiyo tunakwenda kuandaa miradi ya utekelezaji.

“Kinachofanyika ni hivi, baada ya makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai ni mikataba ya utekelezaji. Hii mikataba ndiyo itakayosema sasa mradi wetu utakuwa namna gani, tunashirikiana kwenye eneo gani na mikataba hii itakuwa mingi hautakuwa mmoja,” alisema Msigwa.

Alisema, “Kama ni mkataba wa mifumo bandarini, ushushaji na upakuaji wa mizigo; kama ni mikataba ya kujenga maeneo ya kuhifadhi, kwa kadiri tutakavyokubaliana tutakuja kuwajulisha.”


Mabadiliko CCM

NEC ya leo pia inaelezwa itakuwa mwendelezo wa mabadiliko ya uongozi ndani ya chama hicho ambacho Oktoba mosi, kilifanya mabadiliko kwa kuwateua Jokate Mwegelo, kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake (UWT) na Fakii Lulandala kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).

Hata hivyo, gazeti hili wiki iliyopita lilizungumza na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Annamringi Macha kuhusu mkutano huo lakini alisema ndani ya chama hicho hakuna kikao kilichoitishwa mwishoni mwa wiki.

“Hakuna kikao chochote ndani ya chama kilichoitishwa na mtu yeyote hapa Dodoma, nakuhakikishia kuwa hakuna kikao na mtaona hivyo, niamini mimi nakuambia.

“Siyo NEC wala Kamati Kuu, nakuambia kuwa hatuna mkutano wa CCM hapa Dodoma katika siku za hivi karibuni maana vinginevyo tungewapa taarifa sahihi,” alisema Macha.


Mkutano wenyewe

Pamoja na kauli ya Macha kwamba hakuna mkutano ulioitishwa, vyanzo vyetu vya habari ndani ya CCM, vimelithibitishia gazeti hili kuwa kikao hicho kimeitishwa na mwenyekiti mwenyewe, Rais Samia, huku wengine wakidai yalikuwa mawasiliano ya moja kwa moja bila kupitia sekretarieti.

“Huenda mkutano huu tukaufanyia Ikulu kule Chamwino, lakini lolote linaweza kutokea, hata hapa White House tunaweza kuwa hapa kwani wajumbe tuko wachache, ingawa nahisi tutakuwa Chamwino,” alisema mmoja wa wajumbe ambaye ni Mbunge kutoka Tanzania Zanzibar.

Katika maeneo mengi hadi jana kulionekana kuwa kimya licha ya baadhi ya watumishi wa ofisi za makao makuu kukiri kuwa mkutano huo umepangwa kufanyika leo.