Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania yaimarisha tahadhari dhidi ya mlipuko wa Ebola

Muktasari:

  • Katika hatua ya udhibiti wa sampuli, Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe ameagiza kila maabara izingatie taratibu zote za udhibiti bila kuruka hatua yoyote. ili kuepuka madhara yoyote ya maambukizi yanayoweza kujitokeza.

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Afya, Dk Florence Samizi amesema Tanzania inaendelea na hatua za kuzuia na kuimarisha utayari dhidi ya mlipuko wa ugonjwa wa Ebola unaosababishwa na virusi vya Bundibugyo unaoendelea katika nchi jirani za Jamhuri ya Demokrasia Congo na Uganda.

Dk Samizi ameyasema hayo Jumanne, Mei 26, 2026 kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, huku akisisitiza mshikamano wa kikanda na umuhimu wa ushirikiano wa pamoja katika kulinda usalama wa afya wa wananchi.

Alikuwa kwenye mjadala kuhusu mlipuko wa Ebola katika nchi hizo, uliofanyika Brazzaville, Jamhuri ya Congo, akishiriki kwa njia ya mtandao kutokea katika ofisi za Wizara jijini Dodoma.

Kwa mujibu wa taarifa za mamlaka za afya, zaidi ya watu 906 wanashukiwa kuambukizwa Ebola katika maeneo mbalimbali ya mashariki mwa DRC, huku idadi ya waliokufa ikifikia 223.

Ugonjwa huo umeenea zaidi katika jimbo la Ituri, na wagonjwa kadhaa wamebainika pia katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini karibu na mpaka wa Rwanda.

Katika mjadala huo, Tanzania imeeleza mshikamano wake na Serikali pamoja na wananchi wa DRC na Uganda kufuatia mlipuko huo, huku ikitoa pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao pamoja na wahudumu wa afya waliopo mstari wa mbele wakitoa huduma.

Aidha, Dk Samizi amesema Tanzania inatambua uratibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Maambukizi cha Afrika (Africa CDC) na itaendelea kushirikiana na kutekeleza hatua za pamoja katika kushughulikia masuala ya dharura ili kuendelea kulinda afya za wananchi.


Maelekezo kwa maabara

Wakati huohuo wataalamu wa maabara nchini wametakiwa kuzingatia kikamilifu tahadhari zote za usalama katika uchukuaji, usafirishaji, uchakataji na upimaji wa sampuli za magonjwa ya milipuko ili kujikinga dhidi ya maambukizi na kulinda afya za wananchi.

Mganga Mkuu wa Serikali Dk Grace Magembe ametoa tahadhari hiyo wakati akiongea na wataalamu wa maabara nchini kwa njia ya mtandao kufuatia mlipuko wa Ebola katika nchi hizo.

"Mnapaswa kufuata taratibu zote za ukusanyaji wa sampuli kuanzia hatua ya uchukuaji, uhifadhi, usafirishaji hadi uchakataji wake bila kuruka hatua yoyote, kutofuata utaratibu kunaweza kuhatarisha maisha ya watumishi wa afya pamoja na jamii kwa ujumla," amesema Dk Magembe.

Aidha, Dk Magembe amesisitiza wataalamu wa maabara kufuata kila hatua ya upimaji, akionya dhidi ya kufanya kazi kwa mazoea.

Suala la utoaji wa taarifa, Dk Magembe amesema majibu ya vipimo yanapaswa kutolewa kwa kufuata utaratibu rasmi uliowekwa na Wizara ya Afya, ambapo majibu hayo yanapaswa kupitia ngazi zote zinazohusika kabla ya kutolewa rasmi.

"Si sahihi kwa watumishi wa afya kusambaza majibu ya vipimo kupitia njia zisizo rasmi kama WhatsApp au barua pepe bila kufuata utaratibu uliowekwa, taarifa zote za afya ya umma zinahitaji uthibitisho na mamlaka rasmi kabla ya kutolewa kwa jamii," amesema Dk Magembe.

Kwa upande wa usafi na udhibiti wa taka, Dk Magembe amesema wataalamu wanapaswa kuhakikisha maeneo yote ya kazi yanafanyiwa usafi mara baada ya matumizi pamoja na kuhakikisha udhibiti wa taka.

Pamoja na hayo Dk Magembe amewatoa hofu Watanzania kuwa hadi sasa hakuna mgonjwa yeyote mwenye maambukizi ya ugonjwa huo aliyegundulika nchini na kuwa Serikali inaendelea kujipanga vizuri kuhakikisha ugonjwa huo hauingii.


Wataalamu wajengewa uwezo

Katika upande mwingine Wizara kupitia Idara ya Dharura na Maafa imeendelea kuimarisha utayari wa wataalamu wa afya kupitia mafunzo kwa vitendo na usimamizi shirikishi wa huduma za dharura, maafa na wagonjwa mahututi mafunzo yaliyofanyika Wilaya ya Mvomero ili kuongeza uwezo wa kukabiliana na matukio ya mlipuko wa ugonjwa wa Ebola.

Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Dk Philipina Philipo, wakati mafunzo kwa vitendo ya huduma za dharura, maafa na wagonjwa mahututi yaliyofanyika wilayani hapa.

Amesema mafunzo hayo yamejikita katika kuimarisha uwezo wa wataalamu wa afya katika utambuzi wa mapema wa viashiria vya magonjwa ya mlipuko, uratibu wa huduma na utekelezaji wa hatua za mwitikio wa haraka ili kuongeza utayari dhidi ya Ebola.

 “Kupitia mafunzo haya tunajenga mfumo imara wa mwitikio dhidi ya Ebola na kuhakikisha wataalamu wetu wanakuwa tayari kulinda afya ya wananchi.”

Kwa upande wake, Mratibu wa Huduma za Dharura na Maafa kutoka Wizara ya Afya, Dk Michael Kiremeji amesema mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuendelea kuimarisha utayari wa Taifa katika kukabiliana na milipuko ya magonjwa kwa kujenga uwezo wa wataalamu waliopo katika ngazi za utoaji huduma.