Matumaini chanjo ya Ebola ikitarajiwa miezi miwili ijayo
Muktasari:
- Kwa mujibu wa taarifa ya watafiti, majaribio ya kitabibu kwa binadamu yanaweza kuanza ndani ya miezi miwili hadi mitatu ijayo, hatua inayotoa matumaini mapya katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo hatari.
Dar es Salaam. Chanjo ya majaribio ugonjwa wa Ebola inayotengenezwa na watafiti waliohusika na chanjo ya Uviko-19, inatarajiwa kuanza ndani ya miezi miwili hadi mitatu kuanzia sasa.
Tayari majaribio ya chanjo hiyo kwa wanyama yameanza ikiwa ni juhudi za kukabiliana na kuenea kwa ugonjwa huo.
Mkuu wa Kitengo cha Kinga katika Taasisi ya Sayansi ya Magonjwa ya Mlipuko ya Chuo Kikuu cha Oxford, Teresa Lambe amesema wanatumia teknolojia sawa na waliyotumia kutengeneza chanjo ya Uviko-19 kutengeneza chanjo ya kirusi cha Ebola aina ya Bundibugyo.
Kupitia video hiyo iliyochapishwa na Shirika la Habari la Uingereza la Reuters, Lambe amesema kwa kawaida utengenezaji wa chanjo na majaribio huchukua miaka mitano hadi 10 kukamilika.
Amesema sasa kinachofanyika ni juhudi za haraka kutafuta chanjo ya virusi hivyo.
“Kama mambo yatakwenda kama tulivyotarajia, tunategemea majaribio ya chanjo yataanza ndani ya miezi miwili hadi mitatu kuanzia sasa,” amesema.
Kulingana na watafiti hao, majaribio ya chanjo hiyo kwa wanyama yameanza na yanatarajiwa kuendelea katika maeneo mengine.
Chanjo hiyo ikifanikiwa kupita hatua za majaribio kwa binadamu, inaweza kuwa miongoni mwa zana muhimu katika kudhibiti na kuzuia maambukizi ya Ebola siku zijazo.
Takwimu za ugonjwa wa Ebola, kulingana na Shirika la Marekani la Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC), hadi Mei 25, 2026, jumla ya visa vinavyotokana na ugonjwa wa Ebola vilivyoripotiwa ni 906 na watu waliogundulika kuwa na ugonjwa huo ni 105, huku watu 223 waliohisiwa kuwa na Ebola wakipoteza maisha.
Pia, watu 10 ambao walithibitika kuwa na virusi hivyo walipoteza maisha na nchini Uganda watu saba walibainika kuwa na ugonjwa huo, mmoja akipoteza maisha.
CDC imetoa onyo kuhusu kuenea kwa ugonjwa huo katika mataifa 11 ikiwemo Angola, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Zambia, Tanzania na Uganda, ambayo tayari imepata maambukizi.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, Ebola ni ugonjwa adimu lakini hatari unaosababishwa na virusi vinavyoweza kuambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu.
Dalili zake huanza kujitokeza kati ya siku mbili hadi 21 baada ya maambukizi.
Mgonjwa huanza kupata homa kali, maumivu ya kichwa, uchovu na baadaye kutapika pamoja na kuharisha.
Kadri ugonjwa unavyoendelea, unaweza kusababisha viungo vya mwili kushindwa kufanya kazi na wakati mwingine kutokwa damu ndani na nje ya mwili.