Tanzania, Uganda zasaini MoU kutokomeza magonjwa ya mifugo

Waziri wa Mifugo wa Uganda, Bright Rwamirama, (kushoto) akikabidhiana hati ya makubaliano na Waziri wa Mifugo na Uvuvi wa Tanzania, Abdallah Ulega, baada yakusaini leo Septemba 7, jijini Dar es Salaam.
Muktasari:
- Tanzania na Uganda zimesaini makubaliano ya kusimamia mifugo ikiwa na lengo la kudhibiti magonjwa, kuendeleza miundombinu, teknolojia ya ufugaji, afya ya mifugo pamoja na kuandaa mipango ya pamoja ya tafiti kwa mifugo.
Dar es Salaam. Serikali za Tanzania na Uganda zimesaini makubaliano ya ushirikiano (MoU), kwaajili ya kusimamia afya za mifugo, lengo likiwa kutokomeza magonjwa kwa mifugo ambayo kimsingi yanavuka mipaka kupitia wanyama.
Makubaliano hayo yamesainiwa leo, Septemba 7, 2023, jijini Dar es Salaam na kushuhudiwa na Mawaziri wa Mifugo wa nchi hizo, Maofisa wa Wizara, Makatibu Wakuu pamoja na waandishi wa habari.
Akizungumza, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, amesema kutokana na sekta ya mifugo kuchangia asilimia ndogo kwenye uchumi wa nchi kutokana na sababu kama magonjwa kwa wanyama wameamua kuingia makubaliano hayo yatakayokomesha changamoto ya maradhi.
"Tunamifugo mingi mfano ng'ombe wapo milioni 36, mbuzi milioni 26, kondoo milioni 9, kuku milioni 97, Nguruwe milioni 3, lakinI mchango kwenye uchumi ni asilimia 7. Tafiti zinaonyesha wazi magonjwa ndio sababu kuu.
"Magonjwa hayo ni yale yenye kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine, tumeona lazima tufanye udhibiti wa haya magonjwa kwa kutoa chanjo," amesema Ulega.
Amesema kuna mpango wa miaka mitano ambao utakuwa na kampeni maalumu ya uchanjaji kukiwa na azimio ya kuyamaliza ndani ya muda huo.
Amesema Tanzania na Uganda zina ukanda wa mpaka wenye ukubwa wa kilometa 396 ambao kimsingi ni ngumu kudhibiti mifugo kuhama.
kwa upande wake Waziri wa Mifugo wa Uganda, Bright Rwamirama amesema wanafuraha kuingia makubaliano hayo yatakayosimamia afya za mifugo ambao hawajui kama kuna mipaka.
"Tunapaswa kufanya kazi kwa pamoja ambapo itasaidia hata kwenye soko la mifugo kitaifa na kimataifa," amesema Rwamirama.