Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mawaziri waanika AGRF utakavyoinufaisha nchi

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari kuhusu Mkutano Mkuu wa Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF) Ikulu jijini Dar es Salaam. Picha na Ikulu

Dar es Salaam. Serikali imeainisha na kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya wawekezaji wa sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi watakaovutiwa kuwekeza nchini baada ya Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF).

Kauli hiyo imetolewa Septemba 3, 2023 jijini hapa na mawaziri wa sekta za mifugo, uvuvi na kilimo katika mkutano na wahariri pamoja na waandishi wa habari uliofanyika Ikulu walipoeleza Tanzania itakavyotumia fursa ya Mkutano wa AGRF unaotarajia kuanza kesho hadi Septemba 8.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema tayari wameandaa mpango mahsusi wa kuwapeleka wajumbe wa mkutano wa AGRF katika maeneo wanayoweza kuwekeza na uratibu wake umeshaanza.

“Leo (jana) wengine wameshaondoka kwenda Bagamoyo (Pwani), Morogoro, Zanzibar na nyanda za juu kusini. Lakini tukimaliza AGRF kuna wengine pia watakwenda. Hatua hii imetokana na majadaliano yaliyofanyika katika mikutano ya nyuma iliyohudhuriwa na Rais, Samia Suluhu Hassan iliyozungumzia uwekezaji,” alisema Bashe.

Alisema ni vema Watanzania wakajua mazao yanayozalishwa nchini na kuhitaji masoko na uwezeshwaji.

“Mkutano huu wa AGRF ni nafasi ya kuonyesha fursa tulizonazo kwa watakaohudhuria mkutano huo na wale watakaotaka kuwekeza tunawakaribisha kwa mikono miwili na tumeweka mazingira bora” alisema

Naye Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alisema awali, mkutano AGRF ulikuwa maalumu kwa kilimo pekee, lakini safari hii umehusisha na sekta ya mifugo na uvuvi.

Waziri Ulega alisema Rais Samia ametumia fursa hiyo kuhakikisha sekta hizo zinakwenda pamoja ili kuleta matunda mazuri.

Alisema lengo lake ni kuona tija katika uwekezaji wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi na hivyo Mtanzania ananufaika kwa kiwango kikubwa

Waziri Ulega, alisema sekta hizo zinamgusa kila Mtanzania moja kwa moja na lengo la Serikali ni kuwainua kiuchumi.

“lengo la Rais Samia ni kutaka kuhakikisha sekta hizi zinazowagusa Watanzania wengi, zinapata mitaji katika masoko na teknolojia ili kuvuta makundi makubwa na kuleta tija, kimsingi hili ndilo dhumuni la mkutano huu ambao kwetu tunaona ni fursa ya kuitumia sasa kwa kuwatengenezea Watanzania mapito,” alisema Waziri Ulega.

Katika hatua nyingine, Ulega alisema wizara anayoiongoza imeshatenga maeneo watakayowapeleka wadau wa mkutano huo kuona sehemu gani wanaweza kuwekeza kulingana na mahitaji yao.

“Wizara ya mifugo na uvuvi tumeshaandaa maeneo ya kimkamati kwa ajili ya uwekezaji, lengo ni kuwaonyesha maeneo mahususi ya uwekezaji wa sekta za mifugo na uvuvi na kwa nini mtu aje kuwekeza nchini kwetu,” alisema Ulega.

Ikulu yaeleza faida

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus alisema Tanzania itanufaika na mkutano huo utakaoshirikisha mataifa zaidi ya 70.

Alisema mkutano huo unafanyika wakati Rais Samia anahimiza Taifa lihakikishe linajitosheleza kwa chakula sambamba na kuzitaka nchi nyingine za Afrika nazo zifanye hivyo ili kukuza uchumi.

Yunus alisema mkutano huu unafanyika wakati ambao Tanzania inatekeleza ajenda ya 10/30 inayolenga kuongeza mchango wa kilimo katika pato la Taifa.

Alisema mkutano wa AGRF ni fursa nzuri kwa viongozi wa nchi za Afrika, watendaji wa Serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali wadau wa mnyororo wa thamani katika kilimo na uvuvi kukutana na kuangalia njia bora za kuendsha shughuli zao.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, Katibu mkuu wa wizara hiyo, Balozi Samwel Shelukindo alisema utalii wa mikutano ni sehemu muhimu katika kuimarisha diplomasia ya uchumi.

“Kinachofanyika sasa hivi (AGRF) ni utekelezaji wa dhamira ya Rais Samia , huu ni mkutano wa pili mkubwa kufanyika Tanzania kwa mwaka huu. Tunategemea fedha nyingi za kigeni zitaingia katika uchumi wetu, ndio maana ya utalii wa mikutano,” alisema Balozi Shelukindo.

Balozi Shelukindo alisema mkutano huo ni mkubwa na viongozi wakubwa watahudhuria kutokana na umuhimu wa kilimo, mifugo na uvuvi.

Alisema hadi sasa marais saba wamethibitisha kushiriki huku wengine wakiendelea na mchakato wa kupeleka maombi.

“Kuna wengine watawakilisha marais na mawaziri wakuu, kupitia Kituo cha Kimatiafa cha Mikutano cha Arusha (AICC), tuna mpango wa kujenga kituo kingine cha mikutano kinaweza kuwa cha pili au cha tatu Afrika.

Matarajio

Akizungumzia matarajio ya Tanzania, Yunus alisema mkutano huo umelenga kuleta matokeo muhimu kati ya Tanzania na nchi nyingine za Afrika.

Alisema matokeo yanayotarajiwa ni kuongezeka kwa uwekezaji katika sekta za kilimo nchini, kukuza utalii na kuimarika kwa mazao ya kilimo na teknolojia.

“Mkutano huu pia ni fursa ya utalii kwa hoteli zetu za Dar es Salaam na Zanzibar zinataraji kupata watalii wa kutosha, sambamba na sekta za usafirishaji na ukarimu,” alisema.

Yunus alisema wageni zaidi ya 3,000 watahudhuria mkutano huo kutoka mataifa 70 ulimwenguni wakiwemo wakuu wa nchi, watu maarufu na watunga sera, wafanyabiashara, wawekezaji na wakulima.

Wakati huohuo, katika mkutano huo, Bashe aligusia namna wizara yake ilivyojipanga katika kuinua na kuboresha zao la alizeti akisema mwaka huu wametoa tani zaidi ya 1,000 za mbegu za ruzuku kwa wakulima wa Singida na Dodoma.

Bashe alisema Mkoa wa Singida ulipewa tani 500 za mbegu bora za alizeti na matokeo yameanza kuonekana kwa uzalishaji wa zao hilo kuongezeka kutoka tani 600,000 hadi 800,00.

Mwezi uliopita akifunga maonyesho ya Nanenane yaliyofanyika kitaifa katika viwanja vya John Mwakangale mkoani Mbeya, Rais Samia alisema Tanzania imepata fursa ya kuandaa mkutano wa AGRF hivyo Watanzania na kampuni za nje zilizopo nchini kujiandikisha katika mkutano huo.

Zanzibar haijabaki nyuma

Waziri wa Uchumi wa Buluu, Zanzibar Suleiman Masoud Makame, ambaye alikuwapo kwenye mkutano uliofanyika Ikulu, alisema maana ya uchumi wa buluu ni namna rasilimali za bahari, mito na maziwa zitakavyotumika kwa usahihi.

“Miradi yote inayotekelezwa na wizara hii inalenga kuwasaidia vijana katika maeneo ya taaluma kwa shughuli wanazozifanya, mitaji na masoko,” alisema

Masoud alisema miongoni mwa miradi ambayo vijana wananufaika nayo ni utekelezaji wa fedha za Uviko-19 zilizowawezesha vijana waliogawanywa katika makundi ya wavuvi wadogo na wakulima wa mwani ambapo takribani vikundi 500 vilinufaika.