Chalamila awahakikishia usalama wageni mkutano wa chakula Dar

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amewahakikishia usalama wageni wote watakaohudhuria Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF-2023), utakaofanyika kuanzia Septemba 5 hadi 8 Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini humo.
Chalamila ameyasema hayo leo Ijumaa Septemba 1, 2023, kwenye mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mkutano huo utakaokutanisha zaidi ya wageni 3,000.
Mkuu huyo wa mkoa amesema anashukuru Dar es Salaam kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo na kuwahakikishia wahudhuriaji kuwa watakuwa salama katika kipindi chote watakapokuwepo jijini humo.
"Kwa kuwa mkutano huu utafanyikia Dar es Salaam, nautangazia umma kuwa tumejiandaa vizuri katika suala zima la usalama hivyo wananchi wana kila sababu ya kujitokeza kutumia fursa ya uwepo wake ili kuweza kujipatia uzoefu na ujuzi katika sekta ya kilimo, mifugo na biasahara," amesema Chalamila.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), Ephraim Mafuru, amesema kama kituo wamejipanga vizuri kuwahudumia wageni hao, ambapo mpaka sasa waliojisajili ni zaidi ya 3,000.
Mafuru amesema maandalizi ya mkutano huo, yaliyogharimu Sh2.5 bilioni, fedha yake inaingia kwenye mnyororo wa thamani wa uchumi wa fedha ambazo sio faida kwa serikali bali na wananchi kwa ujumla kwa kuwa nao watakuwa wakitoa huduma mbalimbali kwa wateja ikiwemo malazi na kuwalisha kipindi chote cha mkutano.
"Kwa hali hii, niwaombe wale wajasiriamali ambao watabahatika kuhudhuria mkutano huo kutumia fursa hiyo vizuri ili kuweza kupata soko la bidhaa zao na kukamilisha ndoto ya Rais Samia Suluhu Hassan Tanzania kulisha soko la dunia,” amesema Mafuru.