Tanzania ruksa chanjo ya majaribio ya Marburg

Dar es Salaam. Serikali imesema itaanza kutoa chanjo ya Marburg kwa majaribio endapo usalama wa chanjo hiyo utathibitishwa na wataalamu wa ndani.
Majaribio hayo ni wito wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kutaka majaribio ya chanjo ya ugonjwa huo yafanyike hapa nchini.
Wito huo umetolewa ikiwa mwezi mmoja tangu ugonjwa huo ulipuke katika Mkoa wa Kagera na kuua watu watano na wengine kadhaa kulazwa huku wengine wakiwekwa karantini kuzia usisambae.
“Bado hakuna chanjo ya Marburg, lakini ipo inayofanyiwa majaribio, tumepata ombi kutoka WHO wakituomba turidhie majaribio ya chanjo ya Maburg, hili nimepeleka kwa wataalamu wanishauri tukubali au tusikubali.
“Jambo la kusisitiza pale ambapo chanjo imethibitishwa rasmi na WHO na kamati yetu itaona ni salama, Tanzania si kisiwa tutaikubali,” alisema Waziri wa Afya Ummy Mwalimu.
Waziri Ummy alitoa kauli hiyo jana Dar es Salaam katika hafla ya kupokea msaada wa majokofu ya kuhifadhi chanjo, vifaa vya mnyororo wa baridi na maboresho ya majengo mbalimbali, iliyotolewa na Taasisi ya Clinton Health Access Innitiative ya Marekani (CHAI), Kampuni ya Vodacom pamoja na Serikali ya Japan.
Alisema wakati Tanganyika ikipata uhuru kulikuwa na chanjo tatu pekee hapa nchini, lakini sasa kuna chanjo zaidi ya 10, hivyo suala la chanjo ni jambo endelevu.
Akizungumzia msaada wa majokofu 390 ya kuhifadhia chanjo yaliyotolewa na Serikali ya Japan, Ummy alisema yamegharimu Sh3.27 bilioni na tayari yameshaanza kusambazwa katika mikoa 13 nchini pamoja na Zanzibar.
Baadhi ya mikoa ambayo imenufaika na majokofu hayo ni Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Shinyanga, Kigoma pamoja na Songwe.
“Tuna uhitaji wa majokofu ya kisasa 5,822 kwa ajili ya kuhifadhi chanjo, Serikali imenunua 2,012 bado majokofu 3,810 ambayo tutashirikiana na wadau wakiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na watoto (UNICEF),” alisema.
Akizungumzia msaada wa vyumba sita vya kuhifadhi mnyororo wa baridi uliofadhiliwa na Vodacom kwa thamani ya Sh690 milioni na mingine kutoka Chai, Ummy alisema itaifanya nchi kupunguza gharama katika uhifadhi wa chanjo na usambazaji wake kwa kiwango kikubwa.
Meneja Mpango wa Taifa wa Chanjo, Dk Florian Tinuga alisema kabla ya ujenzi wa vyumba sita na vingine vitano vya kuhifadhia chanjo, walikuwa na vyumba vitano pekee.
“Manufaa ya vyumba hivi 16 ni kuongeza nafasi ya utunzaji wa chanjo ngazi ya Taifa kutoka kwenye lita 84,000 hadi 130,000,” alisema.
Mkurugenzi wa Fedha wa Vodacom, Hilda Bujiku alisema msaada huo unalenga kuisaidia Serikali kufanikisha upatikanaji wa chanjo salama kwa wananchi.
Balozi wa Japan nchini, Yushashi Misawa alisema msaada wa majokofu hayo ni mwendelezo wa misaada inayotolewa na Serikali ya nchi yake.
Alisema kupitia mradi wa Covax Japan imetoa msaada wa Dola 30 milioni kwa nchi za Afrika na Amerika kwa ajili ya kuhamasisha chanjo ya Uviko-19 na Tanzania imenufaika na majokofu hayo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Chai, Dk Ester Mtumbuka alisema msaada wao ulilenga katika kuwafadhili madereva kupata ujuzi wa namna sahihi ya kusafirisha salama chanjo,kutengeenza mfumo wa njia ya mtandao wa kufuatilia magari yanayobeba chanjo na mafuta yanayotumika kwenye magari hayo pamoja na kununua magari maalumu kwa ajili ya usambazaji wa chanjo.