Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Biashara changa 30 kupewa fursa, kongamano la uwekezaji nchini

Muktasari:

  • Biashara 10 bora zitapewa nafasi ya kuwasilisha kwa wawekezaji biashara zao mbele ya washiriki wa kongamano hilo litakalofanyika kwa siku mbili kuanzia kesho jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Kongamano la uwekezaji wa biashara changa bunifu la Tanzania Impact Investment Forum 2025 (TIIF) litatoa fursa kwa biashara changa 30 za Kitanzania kwa ajili ya mafunzo maalumu ya kuwasilisha miradi yao.

Biashara 10 bora zitapewa nafasi ya kuwasilisha kwa wawekezaji biashara zao mbele ya washiriki wa kongamano hilo litakalofanyika kwa siku mbili kuanzia kesho jijini Dar es Salaam.

Kongamano hilo lililoandaliwa na Ubalozi wa Switzerland (Uswis) litashirikisha washiriki  zaidi ya 200  wa Tanzania na  wengine kutoka nje ya nchi.

Ofisa Mpango wa Kitaifa wa Uchumi wa Ubalozi wa Uswisi, Daniella Kwayu amesema mojawapo ya matukio muhimu katika jukwaa hilo ni kuwakutanisha pamoja wafanyabiashara changa na wawekezaji.

Amesema biashara changa 30 za Kitanzania zitachaguliwa kwa ajili ya mafunzo maalumu ya kuwasilisha miradi huku zile zitakazoingia kwenye 10 bora zitapewa nafasi ya kuwasilisha kwa wawekezaji hatua inayoweza kuwafungulia milango ya mitaji na fursa za kimataifa.

Akizungumzia kongamano hilo, Kwayu amesema litashirikisha wawekezaji, wajasiriamali wa kijamii, maofisa wa Serikali na wadau wa maendeleo likiwa na kaulimbiu, “Kuharakisha Mabadiliko Kupitia Uwekezaji na Ubunifu.”

Amesema mbali na kulitumia kongamano hilo kama fursa za uwekezaji, pia ni jukwaa la kupata suluhu ya matatizo yanayoikumba jamii na yanayoendana na Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia (SDG).

"Pia, litachambua namna ya uwepo wa mitaji shirikishi, upatikanaji wa fedha, ubunifu wa ujasiriamali vinavyoweza kuchochea ukuaji wa uchumi katika sekta muhimu kwa Watanzania.

"Pia, tunatengeneza mifumo mipya ya kufungua mitaji ambayo inajibu mahitaji halisi ya wajasiriamali wa Kitanzania, vijana, na jamii zao,” amesema Kwayu.

Amefafanua kwamba jukwaa hilo ni la vitendo, ambalo ni sehemu ya kutoa msaada kwa biashara changa zinazolenga kustawisha sekta ya biashara nchini.

Akielezea ushirikiano wa Uswisi na Tanzania, Kwayu amesema kwa miaka 45 iliyopita, Uswisi imekuwa mdau wa maendeleo nchini Tanzania kwa kupitia ubalozi wake uliopo nchini.

"Ushirikiano huu sasa unabadilika na kuwa wa kimkakati na kibunifu," amesema akigusia miradi mbalimbali kama Daraja Impact Fund na Impact-Linked Finance Fund aliyoitaja kusaidia biashara changa za Kitanzania zinazoangazia sekta muhimu kama kilimo, mabadiliko ya tabianchi, afya ya teknolojia na fedha.

 Amesema vituo vya ubunifu vinavyoungwa mkono na ushirikiano wa Uswisi pia vinachangia katika kujenga mazingira bora ya ujasiriamali.

Miongoni mwa vituo hivyo ni Ifakara Innovation Hub iliyopo Morogoro na AfroGreen ClimAccelerator ya Arusha.

"Ifakara Innovation Hub wamejikita katika masuluhisho ya afya kwa kutumia teknolojia, wakati AfroGreen ClimAccelerator  inawawezesha wajasiriamali wa biashara wanaofanya shughuli zinazohusiana na mazingira kupata msaada wa kukuza biashara zao,” amesema.

Amesema Katika kongamano hilo, mada kuu zitahusu kilimo endelevu, ujasiriamali kwa vijana, uwekezaji unaozingatia usawa wa kijinsia, na uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi ambavyo vyote ni maeneo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

"Kwa kuwezesha mazungumzo ya moja kwa moja kati ya sekta binafsi na ya umma, jukwaa hili litaonesha namna mbinu jumuishi za kifedha zinaweza kuziba pengo la uwekezaji nchini," amesema.